Dar es Salaam. Mwimbaji wa Bongofleva, Jux anaendelea kuiwakilisha vizuri Afrika Mashariki, na sasa kupitia tuzo anaweza kujitambulika kama mwanamuziki namba moja katika ukanda huu kwa miaka hii miwili.

Jux, mwanzilishi wa chapa ya African Boy, kati ya Januari 2025 hadi Januari 2026, ameshinda tuzo nne za kimataifa ambazo zinamtaja kama Msanii Bora Tanzania na Afrika Mashariki 2025.  

Wikiendi iliyopita, mkali huyo wa kibao cha Nisiulizwe (2024), aliibuka mshindi katika tuzo za All Africa Music Awards (AFRIMA) zilizofanyika Lagos, Nigeria, ambako pia anatokea mkewe Priscilla Ojo.

Jux alishinda kipengele cha Msanii Bora wa Kiume Afrika Mashariki 2025, ikiwa ni baada ya kuwashinda wakali kama Bien (Kenya), Diamond Platnumz (Tanzania), Element Eleen (Rwanda).

Wengine ni Marioo (Tanzania), Joshua Baraka (Uganda), Mbosso (Tanzania), Bruce Melodie (Rwanda), Sat-B (Burundi), na Yared Negu (Ethiopia).

Tuzo za AFRIMA zilianzishwa mwaka 2014 na Mike Dada kutokea Nigeria, na hufanyika kila mwaka na hushirikisha wasanii kutoka nchi zote za Afrika, chini ya ushirikiano na Umoja wa Afrika (AU).

Lengo kubwa lake ni kutambua na kuthamini vipaji vya muziki barani Afrika pamoja na wanamuziki wa asili ya Afrika, ili wao na kazi zao zipewe nafasi na heshima kwenye soko la dunia.

Kabla ya AFRIMA, mnamo Novemba 2025, Jux alishinda tuzo ya Jayli zilizofanyika jijini Abidjan nchini Ivory Coast, huku napo alishinda kama Msanii Bora wa Kiume Afrika Mashariki 2025.

Ushindi huo unatokana na wimbo wake, Ololufe Mi (2024) akiwa na Diamond, mwanzilishi wa WCB Wasafi ambaye hapo awali awalisharikiana katika nyimbo, Sugua (2019) na Enjoy (2023).

Hapa Jux aliwabwaga Marioo (Nairobi), Diamond (Nitafanyaje), Willy Paul (Keki), Abigail Chams (Me Too), Harmonize (Furaha), Zuchu (Antena), Joel Lwaga (Olodumare), Mbosso (Pawa) na Barnaba (Salama).

Tuzo za Jayli hutolewa kila mwaka zikiwa na lengo la kusherehekea ubora wa muziki, ubunifu, na kuunga mkono sekta za ubunifu wa sanaa barani Afrika kupitia ushindani wa tuzo.

Mbali na kutoa tuzo, Jayli huandaa mafunzo na majadiliano wakiwakutanisha wasanii na wataalamu wa tasnia ya muziki ili kazi zao ziweze kufikia viwango vya kimataifa zaidi.

Kabla ya kushinda Jayli, mnamo Aprili 2025, huko Lagos, Nigeria, Jux alishinda tuzo ya The Headies, aking’ara tena katika kipengele kile kile ila awamu hii ni cha Msanii Bora Afrika Mashariki.

The Headies hawakugawa kipengele hiki kijinsia, na hapa washindani wa Jux walikuwa ni Bien (Kenya), Diamond (Tanzania), Bruce Melodie (Rwanda) na Azawi (Uganda).

Ikumbukwe tuzo za The Headies zilianza kutolea Machi 2006 na Jarida la Hip Hop World la Nigeria ili kutambua mafanikio katika tasnia ya muziki ya Nigeria na baadaye Afrika nzima.

Tuzo hizo ambazo hurushwa live kupitia kituo cha HipTV, zimetengenezwa nchini Uingereza na kufunikwa kwa dhahabu ya karati 21, na pia zimechanganya aina nyingine za madini.

Katika vipengele alivyoshinda Jux kama Msanii Bora Afrika Mashariki, kuna wasanii wawili waliojitokeza kote, nao ni Diamond na Bien, mwanachama wa zamani wa kundi la Sauti Sol kutokea Kenya.

Na kabla ya The Headies, mnamo Februari 2025, Jux alishinda tuzo za Trace zilizofanyika Zanzibar akitakata katika kipengele cha Msanii Bora wa Kiume Tanzania, huku Nandy akishinda kama Msanii Bora wa Kike.

Hata hivyo, haikuwekwa wazi walikuwa wanashindana na kina nani, bali walikabidhiwa tu tuzo hizo hapo Machi 2025 katika hafla maalumu iliyofanyika Dar es Salaam baada ya ile ya Zanzibar kukumbana na changamoto ya hali ya hewa.

Trace Awards, ni tuzo za muziki zilizoanzishwa na Trace Group kuadhimisha miaka 20 ya Trace TV, na kwa mara ya kwanza zilifanyika Rwanda katika ukumbi wa BK Arena hapo Oktoba 2023.

Lengo lake kuu ni kuyatambua mafanikio bora katika muziki na utamaduni wa Kiafrika pamoja na ule uliochochewa na muziki wa Afrika duniani kote.

Ikumbukwe msimu wa 2025 ambao umempatia Jux tuzo hizo, alifanya vizuri na nyimbo zake nyingi ukiwemo ‘God Design’ ambao ulijumuishwa katika EP yake ya kwanza, A Day To Remember (2025).
 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *