Dar es Salaam. Kwa watu wengi sana  Utamaduni na Sanaa kwao huchukuliwa kama burudani tu.  Mbegu ya kudharau utamaduni  na sanaa zetu, ilipandwa toka enzi ya  ukoloni, na bahati mbaya mmea  huo bado unaendelea kustawi miaka mingi sana baada ya kuondoka kwa ukoloni mkongwe.

Wakoloni walijua kuwa moja ya nguzo muhimu  za kututawala kwa urahisi ni kuvunja imani yetu katika utamaduni wetu.  Nguvu za ziada zilitumika, baadaye elimu ilitumika kuhakikisha kuwa wananchi wanaamini kuwa utamaduni wao si kitu chenye thamani.

Na hakika walifanikiwa sana. Wananchi wakaanza kuona kuwa asiye achana na utamaduni wake wa asili,  basi huyo ni ’mshamba’. Waliojiona wameelimika zaidi wakahakikisha wanajiweka mbali na utamaduni wao kadri ilivyowezekana.

Katika hotuba ya Mwalimu Julius Nyerere, mwishoni mwa mwaka 1962 alipokuwa akitangaza kuundwa kwa Wizara ya Sanaa ya Taifa na Vijana, baadhi ya maneno ambayo Mwalimu alisema yalikuwa haya, ‘…….. mambo ya sanaa ndio roho ya Taifa lolote, nchi bila utamaduni ni mkusanyiko wa watu tu ambao hauna roho.

Katika madhambi yote yaliyofanywa na ukoloni, hakuna dhambi kubwa zaidi, kuzidi jitihada iliyofanywa kutufanya kuamini kuwa hatukuwa na mambo yetu ya sanaa ya Kiafrika, au kwamba kama yalikuwapo yalikuwa ni mambo ya kishenzi, ambayo yanafaa kutufanya tuone haya, sio ya kutufanya tuone fahari.

Tulipata elimu ya kizungu, tulifanya jitihada kubwa sana, kuwaonyesha watawala wetu wa kikoloni kwamba tumestaarabika. Na kustaarabika maana yake ilikuwa ni kuacha mambo yote ya aslil yetu na kuiga mambo ya kizungu.

Jitihada kubwa ya vijana wetu hata hivi leo sio jitihada ya kuwa Waafrika wenye elimu ya kisasa, bali ni jitihada ya kuwa wazungu weusi……Tulipokuwa shuleni tulifundishwa nyimbo za kizungu wangapi tulifundishwa nyimbo za Kinyamwezi na Kihehe? 

Wengi wetu tunaweza kucheza ngoma ziitwazo rumba, chachacha, rockin roll, twist na hata waltz, foxtrot na mengineyo. Ni wangapi kati yetu ambao tumewahi kucheza au kusikia ngoma iitwayo gombesugu, mangala, konge, nyamumi, kiduo, lelemama, na mengineyo?’ 

Hii ni hotuba iliyotolewa mwaka 1962, miaka sitini na nne iliyopita, ukiisikiliza utadhani inaongelea hali ilivyo leo hii.

Kukosekana kwa msisitizo katika utamaduni wetu ndio chanzo kimojawapo cha kukosekana kwa yanayoitwa  ‘maadili ya Kitanzania’. Maadili hufundishwa, hayatoki hewani tu, na maadili yanatokana moja kwa moja na utamaduni.

Utamaduni unabeba, mila, taratibu, sanaa na hata michezo. Katika kutekeleza vizuri utamaduni ndipo unapata maadili mazuri ya jamii, Mwalimu Nyerere alisema mwaka 1962  ‘Taifa lisilo la utamaduni ni mkusanyiko wa watu usio na roho’.  

Katika zama hizi, kuanzia kwenye ngazi ya familia, mambo ya ‘utamaduni’  yanapuuzwa. Wazungu weusi kwa mamia wanatengenezwa, limekuwa si jambo la kushangaza kukuta familia ya Kitanzania inazungumza  Kiingereza tu, Kiswahili kinaguswaguswa tu kama kuna wageni. 

Watoto wadogo kuanzia shule za awali wanafundishwa nyimbo na michezo kutoka mataifa mengine  hasa ya magharibi.

Si ajabu kabisa ukakuta hata uangaliaji wa TV ya familia inaongozwa na mtoto mdogo ambaye kutwa nzima anaangalia katuni za kizungu. Mara chache akikemewa kwa woga na wazazi wake, ‘ Beyonce give remote to daddy please, he wants to watch the news.’

Mtoto akisema ‘No’ mada inafungwa. Jambo la ajabu ni kuwa kuna shule tena vijijini zinatoa adhabu kwa wanafunzi watakaosikika wanaongea kwa lugha yao ya asili kwenye maeneo ya shule!!!!.

Hakuna shaka kabisa kuwa vyombo vya utangazaji viko mstari wa mbele kuendeleza ‘ Uzungu weusi’. Watangazaji wengine wanashindwa hata kumaliza sentensi mbili bila kuweka neno la Kiingereza lakini wanaruhusiwa kuendesha vipindi bila tatizo lolote.
 
Si rahisi siku hizi kusikia nyimbo za Kiasili kwenye vyombo vya utangazaji, labda iwe ni sehemu ya taarifa ya habari.  Vipindi vya watoto pia huwa ni kama vile watoto wale si Watanzania kwani sanaa zinazotumiwa kwa sehemu kubwa ni za kutoka nje.

Mara nyingine unabaki kucheka unapoona watoto wamefundishwa kucheza ngoma za asili kutoka Botswana wakati kuna makabila zaidi ya mia moja na ishirini hapahapa nchini ketu.  

Katika mazingira kama haya, ni vigumu kupata wasanii ambao watalinda na kuendeleza utamaduni wetu, na pia ni wazi kusisitiza Utanzania katika sanaa yako kunakuondoa kwenye soko au ajira ya kazi zako. 

Kauli mbiu moja maarufu inatangaza kuwa ‘Sanaa ni biashara, sanaa ni ajira’,  kwa haraka haraka ni kauli mbiu inayoonekana imejaa busara lakini ina mapungufu.  Sanaa ni zaidi sana ya ajira na biashara. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *