Mamady Doumbouya, jenerali aliyeongoza jeshi la Guinea kuchukua madaraka kupitia mapinduzi ya kijeshi mnamo mwaka 2021, ameapishwa kuwa rais wa nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Sherehe ya kuapishwa Doumbouya ambayo ilifanyika jana Jumamosi mbele ya maelfu ya wafuasi wake na kuhudhuriwa pia na wakuu kadhaa wa nchi, inafuatia kutangazwa mshindi jenerali huyo wa jeshi la Guinea katika uchaguzi wa mwezi uliopita.

Uchaguzi wa Desemba ulikuwa wa kwanza kufanyika nchini humo tangu Doumbouya alipompindua Rais Alpha Conde miaka minne iliyopita.

Japokuwa baada ya kunyakua madaraka, awali Doumbouya aliahidi kutogombea urais lakini hatimaye alibadilisha msimamo na kuwania kiti hicho dhidi ya wagombea wengine wanane. Hata hivyo, wapinzani wake mashuhuri walibaki uhamishoni, na upinzani nao ukatoa wito wa kususiwa uchaguzi huo.

Mahakama Kuu ya nchi hiyo ya Afrika Magharibi baadaye ilitangaza kuwa Doumbouya alipata asilimia 86.7 ya kura.

Huku akiwa amevalia vazi la kiutamaduni, Doumbouya aliapa kuilinda katiba – ambayo ilikuwa imebadilishwa hivi karibuni ili kumruhusu agombee urais – wakati wa sherehe iliyochukua muda wa saa moja katika Uwanja wa Jenerali Lansana Conte nje kidogo ya mji mkuu, Conakry.

Viongozi wakuu wa Rwanda, Gambia, Senegal na nchi zingine kadhaa za Afrika walihudhuria hafla hiyo, pamoja na makamu wa rais wa China, Nigeria, Ghana na Guinea ya Ikweta, na vilevile maafisa kutoka Ufaransa na Marekani.

Assimi Goita, jenerali ambaye anaongoza nchi jirani ya Mali tangu jeshi lilipotwaa madaraka mwaka 2020, naye pia alihudhuria sherehe ya kuapishwa Doumbouya…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *