Ikulu ya White House imetangaza majina ya wajumbe wa linaloitwa baraza la amani litakaloongozwa na Rais wa Marekani Donald Trump na kusimamia utawala wa eneo la Palestina la Ukanda wa Ghaza. Orodha hiyo inajumuisha waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mark Rubio, mjumbe maalumu wa Trump Steve Witkoff, mkwe wa Trump Jared Kushner, na waziri mkuu wa zamani wa Uingereza Tony Blair.

Taarifa iliyotolewa na Ikulu ya White House imesema: “kamati ya kitaifa ya uendeshaji wa Ghaza itaongozwa na Dkt. Ali Shaath. Yeye ni shakhsia mteknokrati anayeheshimika sana. Atasimamia mchakato wa urejeshaji wa huduma za msingi za umma, ujenzi mpya wa taasisi za kiraia, na kupatikana utulivu katika maisha ya kila siku huko Ghaza.”

Taarifa hiyo imedai pia: “viongozi watendaji wa bodi ya amani ni watu wenye uzoefu mkubwa katika diplomasia, maendeleo, miundombinu, na mkakati wa kiuchumi. Watu hao ni pamoja na: waziri wa mambo ya nje Mark Rubio, Steve Witkoff, Jared Kushner, Sir Tony Blair, Marc Rowan, Ajay Banga, na Robert Gabriel. Watakuwemo pia Jasper Jeffers, kamanda wa Kikosi cha Kimataifa cha kuleta Utulivu huko Ghaza, washauri wakuu wa bodi hiyo, Aryeh Lightstone na Josh Gruenbaum, pamoja na Nickolay Mladenov, mjumbe wa Baraza Kuu la Utawala wa Ghaza, atakayekuwa mwakilishi wa ngazi ya juu”.

Trump alitangaza kuundwa kwa chombo hicho kinachoitwa ‘Bodi ya Amani’ ya Gaza siku ya Ijumaa, akisema  wajumbe wa baraza hilo watatambulishwa hivi karibuni.

Katikati ya Novemba, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio lililopendekezwa na Marekani linalounga mkono mpango wa Trump wa uendeshaji wa Ghaza. Russia na China hazikupigia kura azimio hilo…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *