Serikali ya China imetangaza kuwa inapinga vitisho vya ushuru vilivyotolewa na Rais wa Marekani dhidi ya nchi zinazoshirikiana kibiashara na Iran.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, serikali ya China imeeleza bayana kwamba inapinga vitisho vyovyote vya ushuru vinavyotolewa na Rais wa Marekani Donald Trump dhidi ya nchi zinazoshirikiana kiuchumi na Iran.

Trump alitangaza jana kwamba nchi yoyote itakayofanya biashara na Iran itatozwa na Marekani ushuru wa 25%.

Msimamo huo mpya wa Beijing umetangazwa katika hali ambayo, katika mkutano aliofanya na waandishi wa habari hapo jana, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo Mao Ning alijibu vitisho vilivyotolewa na Trump dhidi ya Iran na kusema: Beijing imepinga kuingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine na kutumia nguvu au vitisho katika mahusiano ya kimataifa.

“Siku zote tumekuwa tukiamini kwamba hakuna washindi katika vita vya ushuru, na China italinda kwa dhati haki na maslahi yake halali”, amesisitiza Ning na akaongezea kwa kusema: “tunaamini kuwa, mamlaka ya kujitawala na usalama wa nchi zote lazima ulindwe kikamilifu kwa msaada wa sheria za kimataifa”.

Mwanadiplomasia huyo wa China amebainisha pia kwamba, Beijing inatoa wito kwa pande zote kufanya juhudi zaidi ili kudumisha amani na utulivu katika Asia Magharibi.

Mao Ning ameendelea kueleza kwamba, Beijing inafuatilia kwa karibu hali ya nchini Iran, na akaongezea kwa kusema: “tuna uhakika kwamba Tehran itayashinda matatizo na utulivu utadumishwa nchini humo”…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *