Kiongozi wa chama cha Yisrael Beiteinu, Avigdor Lieberman, ameonya kuhusu tishio linaloongezeka la Iran, akidai kwamba, makombora ya Iran yamebadilisha kanuni za vita na kutoa wito wa maandalizi ya kuhamisha vituo nyeti vya kimkakati kwa kutarajia mzozo wowote tarajiwa.

Gazeti la Israel Hayom limemnukuu Lieberman akisema wakati wa mkutano wa kundi lake la wabunge kwamba, hapo awali alikuwa ametaka kuweko maandalizi ya kujilinda dhidi ya Iran, lakini alikabiliwa na ukosoaji mkali na mashambulizi wakati huo.

Aliongeza: “Kichekesho ni kwamba nilisoma jana kwamba Waziri Mkuu mwenyewe aliomba kuahirishwa kwa shambulio dhidi ya Iran, akidai kwamba Israel haikuwa tayari. Hii ndiyo gharama ya kuahirisha uamuzi na kushindwa kuchukua hatua kwa wakati unaofaa.”

Lieberman alisema kwamba Iran, ikitokea mzozo, ingejaribu kulenga maeneo ya kimkakati ndani ya Israel, kama ilivyofanya hapo awali katika mashambulizi dhidi ya vituo nyeti. Alisisitiza kwamba kuhamisha malengo yote haiwezekani, lakini alisisitiza hitajio la kujiandaa kwa uhamishaji wa haraka na uliopangwa wa maeneo muhimu.

Katika upande mwingine Lieberman alinukuu ripoti ya hivi karibuni ya Mdhibiti Mkuu wa Serikali akifichua kwamba zaidi ya Waisraeli milioni tatu wanaishi bila ulinzi wa kutosha, pamoja na karibu wanafunzi nusu milioni wanaohudhuria shule bila usalama wa kutosha.

Kiongozi wa chama cha Yisrael Beiteinu amekosoa vikali utendaji wa taasisi ya usalama na uongozi wa kisiasa, akisema kwamba mapungufu yameendelea tangu vita vya mwisho bila hatua zozote halisi kuchukuliwa kushughulikia mapungufu hayo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *