
Rais Masoud Pezeshkian amesema kuwa, matukio ya hivi karibuni nchini Iran yalikuwa mwendelezo wa njama zilizofeli za Marekani na utawala wa Kizayuni katika vita vya siku 12 dhidi ya taifa hili.
Daktari Pezeshkian amesema hayo katika mazungumzo yake kwa njia ya simu na Shehbaz Sharif Waziri Mkuu wa Pakistan na kubainisha kwamba, “mahudhurio ya kihistoria ya mamilioni ya wananchi Iran katika kuwalaani waendesha machafuko waliofunzwa na vibaraka kwa mara nyingine tena yalisambaratisha njama na mipango michafu ya maadui wa Iran.
Katika mazungumzo haya, Rais Pezeshkian huku akithamini uungaji mkono na usaidizi wa mara kwa mara wa Pakistan kwa misimamo halali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, aliashiria matukio ya hivi karibuni nchini Iran yaliyokuwa na mkono wa Marekani na utawala wa Kizayuni na akasema: “Tangu mwanzo wa kukubali kukubali kwetu majukumu, juhudi zetu zote zimekuwa ni kuleta umoja miongoni mwa makundi yote, vyama, makabila na dini ndani ya nchi na kuimarisha ushirikiano, urafiki na uhusiano wa kindugu na kukuza uhusiano katika kiwango bora na nchi jirani na za Kiislamu.
Katika mazungumzo haya ya simu, Shehbaz Sharif Waziri Mkuu wa Pakistan pia alitangaza mshikamano wa serikali ya Pakistan na watu wake na serikali ya Iran na akasema: “Tumekuwa tukifuatilia kwa karibu matukio ya hivi karibuni nchini Iran kwa sababu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina umuhimu wa kipekee kwetu si tu kama jirani bali pia kama nchi muhimu na yenye ushawishi katika eneo hili na dunia kwa ujumla.”