
Nazhat Shameem Khan, Naibu Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), amelituhumu kundi la Rapid Support Forces (RSF) kuwa limechimba makaburi ya halaiki ili kuficha “uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu” uliofanywa katika eneo la Darfur, magharibi mwa Sudan.
Jana Jumatatu Shameem Khan aliliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupitia mkutano wa video kwamba Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai imehitimisha kwamba “uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu ulifanywa huko El Fasher” (mji mkuu wa Jimbo la Darfur Kaskazini), hasa mwishoni mwa mwezi Oktoba mwaka jana wakati mji huo ulipozingirwa kikamilifu na wapiganaji wa RSF.
Kutokana na vikwazo vya Marekani dhidi ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, Naibu Mwendesha Mashtaka wa mahakama hiyo ametoa taarifa yake kupitia video, na kusema kwamba hitimisho la Mwendesha Mashtaka limetegemea “ushahidi wa sauti na video na picha za setalaiti zinazoonyesha mauaji ya halaiki na jitihada za kuficha uhalifu kwa kuchimba makaburi ya halaiki.”
Naibu Mwendesha Mashtaka wa mahakama ya ICC amesema “ukatili uliofanywa huko El Geneina (mji mkuu wa Jimbo la Darfur Magharibi) mwaka wa 2023 ulikaririwa huko El Fasher mwaka wa 2025.” Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanakadiria kwamba wapiganaji wa Rapid Support Forces (RSF) wameua kati ya watu 10,000 na 15,000 huko El Geneina, wengi wao wakiwa kutoka kabila la Masalit.
RSF ilianza kuzingira El Fasher mnamo Mei 2024 kabla ya kuidhibiti kikamilifu Oktoba 2025, huku kukiwa na tuhuma kwamba vikosi hivyo vilifanya mauaji ya halaiki na uhalifu dhidi ya binadamu.
Ikumbukwe kwamba vita kati ya jeshi la Sudan na waasi wa RSF vilivyoanza Aprili 2023 vimesababisha mauaji ya makumi ya maelfu ya watu, na kulazimisha wengine wasiopungua milioni 11 kuwa wakimbizi. Vita hivyo pia vimesababisha mgogoro wa njaa na maafa makubwa ya binadamu kiasi kwamba Umoja wa Mataifa unasema ndio mgogoro mbaya zaidi duniani.