Mataifa ya Marekani, Saudi Arabia, nchi ya Falme za Kiarabu na Misri, zinataka usitishwaji vita nchini Sudan kwa miezi mitatu, ili kuwezesha misaada ya kibinadamu kuwafikia mamilioni ya watu wanaothiriwa na vita kati ya jeshi na wanamgambo wa RSF.

Imechapishwa:

Dakika 1 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Mataifa hayo pia, yanataka kipindi hicho cha miezi mitatu cha usitishwaji wa vita, kifuatwe na uwepo wa mkataba wa kudumu utakaositisha vita.

Pamoja na hilo, nchi hizi pia zinapendekeza uwepo wa serikali ya mpito ya miezi tisa, itakayopelekea uundwaji wa serikali ya kiraia.

Katika taarifa ya pamoja, iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya nje ya Marekani, mataifa hayo manne, yamesisitiza kuwa hatua hizo ni lazima zifanyike kwa utulivu na kutanguliza maslahi ya wananchi wa Sudan.

Mapendekezo haya yanakuja, wakati huu vita vikiendelea kati ya jeshi na wanamgambo wa RSF kwa mwaka wa tatu sasa tangu Aprili mwaka 2023 na kusababisha maelfu ya watu kupoteza maisha na mamilioni kuyakimbia makaazi yao, kwa mujibu wa ripoti za Umoja wa Mataifa.

Haijafahamika iwapo pande zote mbili, zitakubali mapendekezo haya. Kumekuwa na jitihada kama hizi na Jumuiya za kikanda kujaribu kutatua mzozo huu, chini ya Shinikizo la Kimataifa bila mafanikio.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *