Akili Mnemba, AI sasa imejiunga na orodha ya changamoto kubwa na tata zinazojadiliwa na viongozi wa dunia na wanadiplomasia katika kikao cha kila mwaka cha ngazi ya juu cha Umoja wa Mataifa wiki hii.
Tangu kuzinduliwa kwa ChatGPT takribani miaka mitatu iliyopita, teknolojia hii imeonyesha uwezo wa ajabu, huku kampuni za teknolojia zikiharakisha mashindano ya kutengeneza mifumo bora zaidi, wakati wataalamu wakionya kuhusu hatari zake.
Umoja wa Mataifa umetangaza mfumo mpya wa usimamizi wa AI, hatua inayochukuliwa kuwa kubwa zaidi hadi sasa ya kudhibiti teknolojia hii. Jitihada zilizopita kama vile mikutano mitatu ya kilele kuhusu AI iliyofanyika Uingereza, Korea Kusini na Ufaransa, ziliishia katika ahadi zisizofungamana kisheria.
Mwezi uliopita, Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa ulipitisha azimio la kuanzisha vyombo viwili muhimu: jukwaa la kimataifa na jopo la kisayansi huru la wataalamu. Hatua hiyo imechukuliwa kama mwendelezo wa juhudi za kuweka mfumo wa pamoja wa dunia kusimamia maendeleo ya AI.
Jumatano, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litafanya mdahalo wa wazi kuhusu jinsi AI inavyoweza kutumika kwa uwajibikaji, ikizingatia sheria za kimataifa, kusaidia michakato ya amani na kuzuia migogoro. Alhamisi, Katibu Mkuu António Guterres atazindua rasmi jukwaa jipya litakalojulikana kama Global Dialogue on AI Governance.
Majukwaa mapya na matarajio
Jukwaa hilo litakuwa sehemu ya ushirikiano kati ya serikali na wadau mbalimbali, likikusudia kubadilishana mawazo na masuluhisho. Mkutano wake wa kwanza rasmi umepangwa kufanyika Geneva mwaka ujao, na kisha New York mwaka 2027. Wakati huohuo, mchakato wa kutafuta wataalamu 40 kwa ajili ya jopo la kisayansi unaanza, likijumuisha wenyeviti wawili kutoka nchi zilizoendelea na zinazoendelea.
Isabella Wilkinson, mchambuzi wa taasisi ya ushauri ya Chatham House, anasema hatua hii ni “ushindi wa ishara” na ndiyo njia shirikishi zaidi ya kimataifa katika kudhibiti AI. Hata hivyo, ameonya kuwa mifumo mipya huenda ikawa haina nguvu za kutosha, akibainisha kwamba utendaji wa Umoja wa Mataifa unaweza usiwe wa haraka vya kutosha kulingana na mwendo wa teknolojia.
Kabla ya kikao, kundi la wataalamu mashuhuri limezitaka serikali kuafikiana juu ya “mistari myekundu” ya AI kufikia mwishoni mwa mwaka ujao, kwa lengo la kuweka ulinzi wa haraka dhidi ya hatari kubwa. Kundi hili linajumuisha wawakilishi wa OpenAI, DeepMind na Anthropic, na linataka makubaliano ya kimataifa yanayofungamana kisheria juu ya AI, sawa na mikataba ya kudhibiti majaribio ya nyuklia na silaha za kibayolojia.
Stuart Russell, profesa wa sayansi ya kompyuta kutoka Chuo Kikuu cha California, Berkeley, alisema: “Wazo ni rahisi sana. Kama tunavyofanya kwa dawa na mitambo ya nyuklia, tunaweza kuwataka watengenezaji kuthibitisha usalama kabla ya kupata ruhusa ya kuingia sokoni.”
Russell alipendekeza kuwa usimamizi wa Umoja wa Mataifa unaweza kufanana na kazi za Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO), ambalo linaratibu wadhibiti wa usalama kutoka nchi mbalimbali ili kuhakikisha wote wanatekeleza viwango sawa.
Wataalamu pia wanapendekeza mfumo wa mkataba wa kimataifa ambao ungalikuwa na unyumbufu wa kusasishwa kulingana na maendeleo mapya ya AI, badala ya kanuni ngumu zisizobadilika.
Chanzo: AP
