Akihutubia Jumanne katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Trump amesema nchi zenye nguvu duniani zinapaswa kuangazia juhudi za kuhakikisha mateka wanaoshikiliwa Gaza wanaachiliwa huru.

Ameonya kwamba kutambuliwa pekee kwa taifa la Palestina ni sawa na kulipa zawadi kundi la wanamgambo wa Kipalestina la Hamas kwa ukatili wake mbaya ilioufanya, kwani hawapaswi kusahamu mashambulizi ya Oktoba 7, 2023. Trump ameishutumu Hamas kwa kukataa kuwaachia huru mateka na kukataa mapendekezo ya amani yenye tija.

Hamas yakanusha madai ya Trump

Hata hivyo, Hamas imekanusha madai hayo ya Trump kwamba imekataa mapendekezo ya kusitisha mapigano Gaza, ikisema katika taarifa yake kwamba imeweka wazi vipengele vyote vinavyohitajika. Kundi hilo limemshutumu Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu kama mtu pekee anayezuia majaribio yote ya kufikia makubaliano.

Trump alivizungumzia pia vita vya Urusi nchini Ukraine, akisema ushuru mkubwa utakomesha umwagaji damu, na amerudia wito wake kwa nchi za Ulaya kuacha kununua mafuta kutoka Urusi. Amezishutumu China na India kwa kufadhili vita vya Urusi na Ukraine kwa kununua mafuta kutoka Urusi.

Bureij 2025 | Wapalestina waliokimbia kutoka Gaza City wakiwa kwenye kambi ya wakimbizi
Hamas yakanusha madai ya Trump kwamba imekataa mapendekezo ya kusitisha mapigano GazaPicha: Eyad Baba/AFP/Getty Images

Mbali na kuzungumzia mabadiliko ya tabianchi, Trump ametumia sehemu kubwa ya hotuba yake kuzungumzia uhamiaji, ambapo amesema Marekani imechukua hatua madhubuti kudhibiti uhamiaji haramu. Amesema nchi za Ulaya zinaharibiwa kutokana na uvamizi wa wahamiaji haramu, kwani hazifanyi juhudi kupunguza uhamiaji.

Licha ya juhudi zake za kumaliza vita nchini Ukraine na Gaza, Trump ameweka wazi kwamba anataka kutunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobel, kutokana na mara kwa mara kutoa madai kwamba ”amemaliza vita saba duniani” tangu aliporejea tena madarakani.

Trump akutana na viongozi mbalimbali

Baada ya kuhutubia Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa, Trump alikutana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres na kumuhakikishia kuwa Marekani iko nyuma ya chombo hicho cha kimataifa kwa asilimia 100.

Aidha, rais huyo wa Marekani amekutana pia na viongozi na maafisa wa nchi kadhaa za Kiislamu, ikiwemo Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu, Misri, Jordan, Uturuki, Indonesia na Pakistan kujadiliana kuhusu hali ya Gaza na kufikia makubaliano ya kudumu ya kusitisha mapigano.

Trump amesema mkutano huo ulikuwa wenye ”mafanikio makubwa” na wadau wote wakubwa isipokuwa Israel, ingawa hilo litafuata.

New York, Marekani 2025 | Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa
Picha: Ludovic Marin/AFP

Viongozi wengine waliohutubia Jumanne katika Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa ni pamoja na Rais wa Brazil, Luiz Inacio Lula da Silva, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, Rais wa Korea Kusini Lee Jae Myung, Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, na Mfalme Abdullah II wa Jordan.

Kwa upande wake Rais Lula da Silva amesema vipaumbele vya jumuiya ya kimataifa lazima vigeukie kupunguza matumizi ya silaha, kuongeza misaada ya maendeleo, kupunguza madeni kwa nchi maskini zaidi na kuweka ushuru wa chini duniani ili matajiri wengi walipe ushuru zaidi kuliko wafanyakazi.

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Rais Ramaphosa amesema ulimwengu unapigana vita vinavyosababisha vifo na uharibifu mkubwa wakati wanapaswa kupambana na umasikini na kuboresha maisha ya watu walioko katika mazingira hatarishi.

Amebainisha kuwa lazima wachukue hatua madhubuti kukomesha mapigano na kujenga miundombinu ya kijamii inayoboresha maisha ya wananchi ili kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu.

Rais Macron ameonya kuhusu kuongezeka kwa mizozo na uwajibikaji wa pamoja, huku akiitolea mfano Gaza, Ukraine, Sudan na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Kwa mujibu wa Macron, hawatakiwi kuchoka wala kushindwa katika kukabiliana na mizozo hiyo.

(AFP, DPA, AP, Reuters)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *