
Ripoti hiyo iliyotolewa hivi karibuni, inaonyesha taswira ya kutisha kuhusu jinsi vitendo hivi haramu kama rushwa, udanganyifu wa biashara, ukwepaji kodi na bidhaa bandia, vinavyovua rasilimali zilizokusudiwa kutoa huduma muhimu kama elimu, afya na miundombinu. Kupitia mbinu za udanganyifu wa biashara, ambapo bidhaa hupunguzwa au huongezewa thamani kwa makusudi ili kukwepa ushuru au kutakatisha fedha, mabilioni ya pesa hutoweka kila mwaka kutoka kwenye uchumi wa taifa.
Biashara ya magendo ambayo mara nyingi huingizwa kama sukari, na ambayo huwa haitolewei maelezo ya kina pindi inapowasili katika bandari ya Mombasa, imekuwa ikiwagharimu walipa kodi, huku wakati mwingine bidhaa hizo zikiwa hazina viwango vinavyokidhi matumizi ya binaadamu na zisizo salama.
Katika sekta ya madini, mitandao ya usafirishaji haramu wa dhahabu imebainika kuiba mamilioni ya dola kupitia mauzo yaliyopunguzwa thamani na kuinyima serikali mapato na ushuru. Patrick Nyangweso,Afisa Mkuu Mtendaji wa Chama cha Walipa Ushuru nchini kenya, anasema hata kwenye sekta yenye faida kubwa ya mafuta, mashirika ya uangalizi yamebaini bei zinazotiliwa shaka, ishara ya uvujaji wa mfumo.
”Hizi fedha zote, ambazo taifa linapoteza kila mwaka, iwapo zingetumika vizuri, zingeboresha upatikanaji wa huduma bora, haswa kwenye sekta ya afya, elimu, masuala ya ulinzi wa jamii na pia miundombinu.”
Udhaifu wa utekelezaji wa sheria ni sababu ya rushwa kuzidi Kenya
Mashirika ya kiraia yaliyohusika katika utafiti huu yanabainisha kuwa ufisadi na mzunguko haramu wa fedha si makosa ya kiuchumi tu yasiyoonekana, bali hujitokeza moja kwa moja katika hospitali zilizojaa, shule zisizo na walimu wa kutosha na barabara hatari zisizokarabatiwa. Fedha zinazopotea kila mwaka zingeliweza kufadhili huduma ya afya kwa wote,kuboresha shule za umma au kujenga miundombinu endelevu katika majimbo. Badala yake, zinatoweka kwenye mitandao ya maafisa wala rushwa, wafanyabiashara wasio waaminifu na mabenki ya kimataifa yanayolinda fedha chafu.
Matokeo ya ripoti hiyo pia yanaonyesha kwamba udhaifu wa utekelezaji wa sheria, kuingiliwa kisiasa na mianya katika utawala wa kodi vimeunda mazingira mwafaka ya kuendeleza mtiririko huu haramu. Mifumo isiyo imara ya Kenya inatoa nafasi kwa mashirika ya kimataifa kutumia mianya ya kisheria, huku bidhaa bandia zikijaa sokoni na kudhoofisha viwanda vya ndani na kuinyima serikali mapato, kama anavyoeleza James Kinywa, afisa wa Mamlaka ya Mapato nchini Kenya.
”Kwa upande wetu tumekuwa tukizuia mzunguko wa fedha haramu kuingia na kuhakikisha kuwa kila mtu analipa kodi. Utafiti huu umebainisha sehemu ambazo tunastahili kukaza mkanda ili kunufaika na utafiti huu na kuziba nakisi ya taifa.”
Mashirika ya Oxfam Kenya na Transparency Internationalyanatoa mwito wa kuchukua hatua thabiti, ikiwemo kuweka kanuni kali zaidi kudhibiti udanganyifu wa biashara, kusimamia utekelezaji wa sheria za kupambana na ufisadi kwa ukali, na kuongeza uwazi katika zabuni za serikali. Wanazisihi pia serikali kushirikiana kwa karibu na washirika wa kimataifa ili kuziba mianya ya kodi na kuhakikisha mashirika ya kimataifa yanalipa kodi stahiki. Shisia Wasilwa, DW, Nairobi.