Miaka miwili baada ya Israel kuanza operesheni yake ya kijeshi dhidi ya wanamgambo wa Kipalestina wa Hamas katika Ukanda wa Gaza wachambuzi wanasema Hamas imedhoofika kidogo lakini bado haijadhibitiwa kikamilifu, huku Jeshi la Israel likisisitiza imelishinda kundi hilo.
Marina Miron, mtafiti katika idara ya utafiti wa vita katika chuo cha Kings mjini London ameiambia DW kwamba Hamas imeshambuliwa mno na Israel na kupata changamoto kubwa kijeshi lakini bado ina uwezo wa kujipanga upya na pia bado ina uwezo na udhibiti wa hali ya juu.
“Naweza kusema kuna ripoti tofauti linapokuja suala la nguvu za Hamas katika Ukanda wa Gaza. Hamas imepitia changamoto nyingi za kijeshi lakini bado ina uwezo wa kujipanga upya na pia inaendelea kudhibiti na kutoa amri katika eneo hilo.” amesema Miron.
Kabla ya vita vinavyoendelea Gaza vilivyochochewa na shambulizi lililofanywa na Hamas Kusini mwa Israel mnamo Oktoba 7, 2023 na kusababisha mauaji ya Waisraeli I,200 kundi hilo la wanamgambo lilikadiriwa kuwa na wapiganaji kati ya 25,000 hadi 30,000. Lakini ndani ya miaka miwili iliyopita Jeshi la Israel lilisema limewaangamiza kati ya wanamgambo 17,000 na 23,000 wa Hamas.
Serikali hiyo hadi sasa haijatoa ushahidi wowote unaothibitisha imewaangamiza kwa idadi hiyo wapiganaji wa Hamas, na wachambuzi wanasema idadi ya waliouwawa huenda ikawa ndogo.
Mwaka mmoja baada ya vita hivyo, ripoti ya Jeshi la Israel kuhusu mauaji ya wanamgambo hao ilijumuisha mambo mengi kuanzia muda, maeneo na operesheni ya kulidhibiti kundi hilo. Taasisi ya uangalizi wa vita iliyoko Marekani ya “The Armed Conflict Location and Event Data,” ACLED iliripoti Oktoba 2024 kwamba wapiganaji 8,500 waliuwawa. Idadi hiyo ilijumuisha makundi mengine ya wanamgambo.
Hii inamaanisha asilimia 80 ya zaidi ya watu 65,000 waliouwawa katika mgogoro huo hadi sasa ni raia.
Maelfu bado wanajisajili kujiunga na Hamas
ACLED ilipendekeza kuwa Hamas huenda iliwasajili wapiganaji zaidi katika kipindi cha miaka miwili iliyopita na mapema mwaka huu maafisa wa ujasusi wa Marekani waliiambia Reuters kwamba wanaamini kundi hilo limewasajili wapiganaji wapya kati ya 10,000 hadi 15,000.
Leila Seurat, mtafiti katika taasisi moja ya kiarabu ya masuala ya sera iliyoko Paris, Ufaransa amesema kuna viashiria hasa katika mitandao ya kijamii kwamba vijana wadogo wa kipalestina wasiokuwa na mafunzo yoyote wamekuwa wakijiunga na tawi la kijeshi la Hamas, Al-Qassam Brigade na kuendelea kushambulia.
Lakini licha ya atiati iliyopo kuhusu idadi kamili ya wapiganaji wa Hamas waliouliwa, jambo moja linabakia kuwa wazi kabisa kwamba Israel ilifanikiwa kuwaua viongozi wa juu wa kundi hilo na kwa sasa ni kamanda mmoja tu mkuu aliyebakia wa Baraza la kundi hilo lililopanga mashambulizi ya Oktoba 7
Vipi kuhusu utawala wa kiraia wa Gaza?
Kitu kinachojadiliwa kwa sasa ni je Hamas ina udhibiti mkubwa kiasi gani katika Ukanda wa Gaza?
Kundi hilo lina tawi la kijeshi linalopambana na Jeshi la Israel. Lakini kundi hilo lililo na mamlaka katika eneo hilo la pwani ya Gaza tangu mwaka 2007 pia liliwahi kuwa na mamlaka kwa serikali ya raia Gaza.
Wafanyakazi wa umma walilipwa kwa pesa taslimu ambazo Hamas ilikuwa imeihifadhi kwa ajili ya dharura, lakini fedha hizi huenda zinakaribia kumalizika. Jeshi la Israel pia limeendelea kuwashambulia watu binafsi na mashirika au maeneo yanayoaminika kufungamana na kundi hilo kwa lengo la kulivunja nguvu na kuung’oa utawala wake huko Gaza.
Afisa mmoja wa usalama wa ndani Gaza aliiambia BBC hivi karibuni kwamba Hamas imepoteza udhibiti wa takriban eneo zima la GazaAmesema pengo la usalama limejazwa na makundi ya wahalifu na ya kikabila.
Hamas inapambana na makundi hasimu ndani ya Gaza, kukiwa na ripoti za hivi karibuni za Israel kupata uungwaji mkono wa Wapalestina wasiowaunga mkono Hamas, lakini licha ya hayo bado wachambuzi wanasema haitakuwa rahisi kulitokomeza kundi hilo na kile inachoweza kujivunia Israel ni kulidhoofisha tu.
