Shauri hilo lilianza kusikilizwa jana Jumatatu Oktoba 6, kufuatia ombi la mwaka 2023 la Bodi Tendaji ya shirika la Umoja wa Mataifa la Kazi duniani, ILO.

Mkataba huo ulipitishwa baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia na ni msingi wa sheria ya kimataifa ya kazi, ukiwapatia wafanyakazi na waajiri hakikisho la kuanzisha na kujiunga na chama wanachotaka.

Hata hivyo mkataba huo hauelezi au hautaji bayana migomo lakini wachechemuzi kwa muda mrefu wametafsiri uhuru wa kujiunga na kikundi kujumuisha haki ya kugoma.

Hapo jana Rais wa ICJ Yūji Iwasawa alianza mchakato kwa kusoma hoja rasmi ya majaji, akirejelea azimio la ILO na mamlaka ya ICJ ya mchakato huo.

Alitambua muundo wa utatu wa ILO, ambao unajumuisha wawakilishi wa serikali, waajiri na wafanyakazi.

Ombi nadra

Tomi Kohiyama, Mshauri wa Sheria wa ILO amerejelea kuwa ILO haijawahi kufika mbele ya ICJ kwa nafasi ya ushauri tangu mwaka 1982, akisema hilo linaonesha ombi la sasa kuwa ni tukio la nadra.

Amesema sekretarieti ya ILO haitaonesha msimamo wowote kwenye suala hilo, lakini itasaidia Mahakama kwa kutoa ufafanuzi wa muktadha wa taasisi na tafsiri ya mitazamo kwa mujibu wa Mkataba wa Vienna juu ya sheria za mikataba.

“Ushiriki wa vikundi vya waajiri na wafanyakazi, bila shaka ni kitendo cha kipeke katika historia ya ICJ,” amesema.

Sauti tatu kwenye ILO

ILO ilianzishwa mwaka 1919, na ina muundo wa kipekee ndani ya mfumo wa Umoja wa Mataifa kwa kuleta pamoja kile kinachoitwa utatu; wawakilishi wa serikali, waajiri na wafanyakazi katika kupanga viwango vya ajira.

Hata hivyo, mizania hii mara nyingine hukumbwa na mkwamo, hasa mwaka 2012 wakati vikundi vya waajiri vilipohoji iwapo Mikataba ya Kimataifa namba 87 na 89 inatambua haki ya kugoma.

Paapa Danquah, akizungumza kwa niaba ya Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Wafanyakazi, (ITUC), ameeleza migomo kama hatua isiyopitwa na wakati inayotumiwa na wafanyakazi kujieleza.

“Hatua ya mgomo imekuwa ndio mbinu yetu muhimu, ili kuimarisha mazingira ya kazina kulinda utu wetu wa kibinadamu,” alieleza Mahakam.

Amedai kuwa haki ya kugoma ni sehemu ya moja kwa moja ya uhuru wa kujiunga na kikundi na kwamba lazima itambuliwe kuwa inalindwa na Mkataba namba 87.

Kwa upande wake, Roberto Suárez Santos, kwa niaba ya Shirikisho la Waajiri, (IOE) alisisitiza kuwa ilhali haki ya kugoma si kanuni inayopingika, Mkataba namba 87 hautaji wazi au kwa kificho haki ya kugoma.

Alionya kwamba kuisoma ndani ya Mkataba kwa sasa kutaleta mfumo wa kisheria wa lazima – unaofafanua taratibu za mgomo – ambao unaweza kuvuruga mifumo ya kazi ya kitaifa iliyo ya kipekee na ya kina.

Badala yake alieleza kuwa njia sahihi ingekuwa ni muafaka ndani ya vyombo vya pande tatu vya ILO, na si kuinua viwango kwa uamuzi wa mahakama upande mmoja.

Maoni ya ushauri ya ICJ

Katika siku hizi tatu, nchi na mashirika 21 yanatarajiwa kutoa ushahidi, huku taarifa 31 za maandishi tayari zikiwa zimewasilishwa katika rejesta ya ICJ – jambo linaloonesha umuhimu wa kimataifa kuhusu uamuzi huo.

Maoni ya ushauri ya Mahakama, yanayotarajiwa kutolewa katika miezi ijayo, hayatakuwa na nguvu ya kisheria lakini yanaweza kuwa na athari kubwa kwa sheria za kazi za kimataifa na kitaifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *