Mkutano huo umelenga kuimarisha mifumo ya pamoja chini ya azimio la Baraza la Usalama namba 2719 (2023), lililopitishwa kusaidia operesheni za amani zinazoongozwa na Afrika na kushughulikia migogoro inayoendelea.

“Ushirikiano kati ya Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika haujawahi kuwa imara hivi,” amesema Parfait Onanga-Anyanga, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa Muungano wa Afrika.

Ameongeza kuwa “Umejengwa juu ya maadili na matarajio tuliyo nayo kwa pamoja na juu ya utambuzi kwamba changamoto zinazokabili Afrika zinahitaji hatua za pamoja na zenye uratibu.”
 

Alisema ushirikiano huo unaonesha uelewa wa pamoja kwamba uthabiti wa bara hilo unategemea ushirikiano katika ngazi zote, akisisitiza kuwa Umoja wa Mataifa na UA lazima “ziende sambamba ili kuhakikisha amani na usalama vinadumu”.

Parfait Onanga-Anyanga, Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu katika Pembe ya Afrika akitoa maelezo kwa mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu kudumisha amani na usalama wa kimataifa.

UN Photo/Eskinder Debebe

Parfait Onanga-Anyanga, Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu katika Pembe ya Afrika akitoa maelezo kwa mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu kudumisha amani na usalama wa kimataifa.

Mageuzi na utawala bora ndiyo msingi wa ushirikiano

Bwana Onanga-Anyanga amesisitiza kwamba mageuzi katika sekta ya usalama na uimarishaji wa utawala bora ni vipengele muhimu vya ushirikiano kati ya Umoja wa Mataifa na UA.

“Ili kufikia amani ya kudumu, lazima tushughulikie chanzo cha migogoro, siyo dalili zake pekee,” amesema.

Mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa ametaja mafanikio ya miradi ya upokonyaji wa silaha, ujumuishwaji na urejeshaji DDR, hususan katika Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, akisema ni “uthibitisho kwamba suluhu za Kiafrika zinaweza kufanya kazi pale zinapoungwa mkono na ushirikiano wa kweli.”

Kuendeleza operesheni za amani za pamoja

Onanga-Anyanga pia amesifu ushirikiano unaoendelea kati ya Umoja wa Mataifa, Muungano wa Afrika na mashirika ya kikanda katika kuimarisha operesheni za amani zinazoongozwa na Waafrika.

“Mipango madhubuti na usimamizi bora wa operesheni za UA ni muhimu,” amesema, akibainisha kuwa mashirika hayo mawili yanaimarisha utayari wa kiutendaji kutekeleza azimio la 2719.

Azimio hilo linaweka mfumo wa ufadhili, upangaji na usimamizi wa operesheni za amani za UA zitakazoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.

Martha Ama Akyaa Pobee, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Afrika katika Idara za Siasa na Masuala ya Ujenzi wa Amani na Operesheni za Amani akitoa muhtasari wa mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu kudumisha amani na usalama wa kimataifa.

UN Photo/Eskinder Debebe

Martha Ama Akyaa Pobee, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Afrika katika Idara za Siasa na Masuala ya Ujenzi wa Amani na Operesheni za Amani akitoa muhtasari wa mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu kudumisha amani na usalama wa kimataifa.

Maendeleo na changamoto katika utekelezaji wa Azimio 2719

Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya Afrika, Bi. Martha Ama Akyaa Pobee, ameliarifu Baraza la Usalama kuhusu maendeleo yaliyopatikana chini ya azimio hilo.

Ametaja mafanikio katika upangaji wa pamoja, msaada wa operesheni na mifumo ya uwajibikaji, “lakini akaonya kwamba changamoto bado zipo.”

Pobee amesisitiza kuwa uelewa wa pamoja na matarajio halisi miongoni mwa washirika ni muhimu kwa mafanikio.

“Ushirikiano wa kweli unategemea uwazi, uaminifu na uwajibikaji,” ameongeza.

AU yataka msaada wa kimataifa kwa udhibiti wa kikanda

Mohamed Fathi Ahmed Edrees, Mwakilishi wa Kudumu wa Muungano wa Afrika kwenye Umoja wa Mataifa, aameonya kwamba “Afrika inakabiliwa na wimbi lisilokuwa na kifani la vitisho vya usalama kuanzia Sahel hadi Somalia, kutoka Sudan hadi Msumbiji.”

Amesema ushirikiano wa karibu na nchi za Karibea kupitia kundi la A3+ umesaidia kuibua vipaumbele vya usalama vya Afrika katika mijadala ya Baraza la Usalama.

Amesema “Uthabiti wa Afrika lazima uchochewe na suluhu za Kiafrika, zikiungwa mkono na mshikamano wa kimataifa”.

Kuimarisha ushirikiano kwa amani Afrika

Katika mkutano huo washiriki wote walikubaliana kwamba ushirikiano kati ya Umoja wa Mataifa na UA unabaki kuwa nguzo kuu ya ujenzi wa amani wa kimataifa barani Afrika.

Wakati migogoro ya kimataifa ikiendelea kukandamiza rasilimali na umakini, Onanga-Anyanga amesisitiza umuhimu wa nia ya umoja.

Amehitimisha kwa kusema kuwa “Wakati Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika wanapofanya kazi pamoja, Afrika na dunia kwa ujumla inakuwa imara zaidi.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *