Ripoti hizo zinaonesha kuwa China inaibuka kama msukumo mkuu wa upanuzi huo duniani, ikiwa na asilimia 43 ya ongezeko la uzalishaji wa umeme wa jua na asilimia 44 ya ongezeko la uzalishaji wa umeme kwa kutumia upepo.

Nishati mbadala ilifikia hatua ya kihistoria katika nusu ya kwanza ya mwaka 2025 kwa kufidia kikamilifu ongezeko lote la mahitaji ya umeme duniani, kulingana na ripoti ya karibuni kutoka kituo cha utafiti cha Ember. na shirika la kimataifa la nishati, IEA.

Ufanisi huu wa kipekee unathibitisha mchakato wa mpito wa nishati duniani na kuonesha uwezo wa nishati safi kukuza uchumi bila kuongeza uzalishaji wa hewa chafu kutoka sekta ya umeme.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, amekaribisha taarifa hizo akisema kupitia mitandao ya kijamii kuwa, “Lazima tuitumie fursa hii ya kihistoria na kuendesha mabadiliko ya kimataifa kuelekea mustakabali bora kwa wote.”

Ripoti hiyo, iliyochapishwa Jumanne Oktoba 7, 2025, inaonesha kuwa uzalishaji wa umeme kwa kutumia jua na upepo uliongezeka kwa asilimia 12 ikilinganishwa na mwaka uliopita katika miezi sita ya mwanzo wa mwaka, na kutoa ziada ya terawati  1,023.

Ongezeko hili lilizidi mahitaji yote mapya ya umeme duniani, ambayo yalikuwa terawati 1,020 ukilinganisha na kipindi kama hicho mwaka 2024.

China, injini ya mabadiliko

Dave Jones, ambaye ni Mkurugenzi wa Mipango ya Kimataifa Ember amesema, “Tunashuhudia mchakato wa kuondoa hewa chafu kwenye sekta ya umeme ukiwa unaendelea kwa wakati halisi – hatua muhimu kuelekea kufikia malengo ya kimataifa tabianchi.”

Ripoti inasisitiza kuwa ukuaji huu ulitokea licha ya changamoto kama vile ukame Amerika Kusini — ulioathiri uzalishaji wa umeme kwa kutumia maji — na kupungua kwa ukuaji wa kiuchumi katika baadhi ya masoko.

Mwanamke kijana nchini Côte d'Ivoire akiwa ameinua paneli ya sola ikiwa ni sehemu ya masomo yake ya nishati mbadala.

© UNICEF/Frank Dejongh

Mabadiliko ya mtazamo

Takwimu zinathibitisha kuwa huu ni mwelekeo wa kimfumo: mwaka 2024 ulikuwa mwaka wa kwanza ambapo nishati mbadala ilifidia kikamilifu ongezeko la mahitaji ya umeme duniani, na mwaka 2025 unaendeleza hali hiyo. Asilimia ya nishati safi katika mchanganyiko wa uzalishaji wa umeme duniani sasa imefikia asilimia 41, ikilinganishwa na asilimia 39 katika nusu ya kwanza ya 2024.

“Tunakabiliwa na mabadiliko ya msingi,” ameeleza Jones, akiongeza kwamba, “Mpito wa nishati umefikia hatua ya mabadiliko ambapo nishati mbadala si tu kwamba inaongeza uwezo, bali inaongoza mfumo mzima. Hii inatupa matumaini ya kweli kwamba sekta ya umeme inaweza kufikia kiwango cha kutotoa kabisa hewa chafu ifikapo 2040.”

Ushindani wa gharama waendelea kuwa kichocheo kikuu

Ukuaji huu unaenda sambamba na makadirio ya Shirika la Kimataifa la Nishati (IEA), ambalo katika ripoti yake ya Renewables 2025, linatabiri kuwa uwezo wa uzalishaji wa nishati mbadala duniani utaongezeka kwa asilimia 30 mwaka 2025, ukifikia gigawati 6,300.

Ukuaji huu — ambao ni wa haraka zaidi kuwahi kurekodiwa — unathibitisha kuwa ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, nishati safi itakuwa chanzo kikuu cha umeme duniani, ikizidi makaa ya mawe.

Vichocheo vikuu vya ukuaji wa kimataifa

IEA inatambua vichocheo kadhaa vya ukuaji huu wa kihistoria. Mbali na ushindani wa kiuchumi, inataja pia uungwaji mkono wa kisiasa katika zaidi ya nchi 130, huku China, Muungano wa Ulaya, Marekani na India zikiwa vinara.

Ripoti hiyo inasisitiza pia mchango wa masoko kwenye nchi zinazoibuka kiuchumi,  ambapo Brazil, India na nchi za Kusini Mashariki mwa Asia zinaonesha ukuaji wa kasi wa nishati mbadala.

Mtazamo chanya

Ripoti inatabiri kuwa mwaka 2025 huenda ukawa mwaka wa kwanza ambapo uzalishaji wa nishati kutoka mafuta ya kisukuku utashuka kwa kiasi kikubwa, hata kama uchumi wa dunia utaendelea kukua kwa utulivu. Maendeleo haya yanaiweka dunia karibu zaidi na lengo la kuongeza mara tatu uwezo wa nishati mbadala ifikapo mwaka 2030, kama ilivyowekwa kwenye mkutano wa 28 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi,  COP28.

Hata hivyo, kama ambavyo Umoja wa Mataifa umekuwa ukisisitiza, licha ya mafanikio haya, mabadiliko haya bado hayatoshi kwa kasi wala kwa usawa. Kuna haja ya kuongeza kasi zaidi ili kufikia lengo la kuzuia ongezeko la joto duniani lisizidi nyuzi joto 1.5 katika kipimo cha Selsiyasi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *