
Rais wa Marekani Donald Trump ametoa wito siku ya Jumatano, Oktoba 8, wa kufungwa jela kwa Meya wa Chicago Brandon Johnson na Gavana wa Illinois JB Pritzker, akiwatuhumu wabunge hao wawili wa chama cha Democratic kwa kushindwa kuwalinda maafisa wa polisi ya Uhamiaji (ICE).
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
“Meya wa Chicago anapaswa kuwa gerezani kwa kushindwa kulinda maafisa wa ICE! Vivyo hivyo kwa Gavana Pritzker!” ameandika kwenye mtandao wake wa Truth Social.
Wanajeshi mia mbili wa Walinzi wa Kitaifa wamewasili karibu na Chicago, afisa wa ulinzi wa Marekani alitangaza siku ya Jumanne, Oktoba 7, baada ya rais kuelezea mji huo mkubwa wa kaskazini kama “eneo la vita.”
Donald Trump aliidhinisha kutumwa kwa wanajeshi 700 wa Walinzi wa Kitaifa mwishoni mwa wiki hii, lakini upinzani kutoka chama cha Democratic ulipinga uhalali wa agizo hilo mahakamani, ukimtuhumu bilionea huyo kwa “kuadhibu maadui zake wa kisiasa.” Upinzani unadai kuwa utawala wa Trump unatumia maandamano nje ya kituo cha ICE katika kitongoji cha Chicago kama “kisingizio” cha kuhalalisha kutuma askari.
Kutokubaliana kwa Mahakama na utawala wa Trump
Jaji wa shirikisho anayesimamia kesi hiyo amepanga kusikilizwa kwa kesi hiyo siku ya Alhamisi. Mwishoni mwa wiki hii, jaji alizuia kwa muda kutumwa kwa wanajeshi hao huko Portland, mji mwingine ambao ni ngome ya chama cha Democtaric. Upinzani wa chama cha Democratic ulidai kuwa “hakukuwa na uasi huko Portland au tishio kwa usalama wa taifa,” kinyume na madai ya utawala wa Trump.
Donald Trump amekuwa akilenga Chicago kwa wiki na ameibua uwezekano wa kutumia Insurrection Act, mkusanyiko wa sheria za karne ya 18 na 19. Hii inaruhusu tamko la hali ya hatari kuidhinisha matumizi ya vikosi vya kijeshi dhidi ya raia wa Marekani, ambayo ni marufuku kimsingi.
Rais tayari ametuma wanajeshi wa walinzi wa kitaifa katika miji ambay ni ngome za chama cha Democratic ya Los Angeles, Washington, na Memphis, kila wakati dhidi ya ushauri wa viongozi wa miji hiyo.