
Ofisi ya Waziri Mkuu wa Somalia leo imetoa taarifa na kukadhibisha vikali Somalia kwamba imefikia makubaliano ya siri na Sweden kuhusu kuwarejesha nyumbani raia wa Somalia kutoka Sweden ukiwemo pia mpango wa msaada wenye masharti kwa Somalia.
Taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu wa Somalia imeeleza kuwa: Somalia haina mpango wowote wa siri au wenye masharti uliofikia na mshirika wake yoyote kuhusu kuwarejesha nchini raia wa Somalia au kuhusiana na utoaji misaada ya maendeleo.
Ripoti za vyombo vya habari zinadai kuwa Somalia imekubaliana na Sweden kuwapokea raia wa Somalia waliofukuzwa Sweden mkabala wa Somalia kupatiwa misaada ya maendeleo.
Ofisi ya waziri Mkuu wa Somalia imekadhibisha madai yote haya na kuyataja kuwa ya uwongo, yasiyo na msingi na yenye kupotosha.
Taarifa ya serikali ya Somalia imeongeza kuwa misaada ya maendeleo kwa nchi hiyo imekuwa ikiratibiwa kupitia mifumo iliyo wazi ikiwemo Benki ya Dunia, mashirika ya Umoja wa Mataifa na mfumo wa fedha wa serikali ya Somalia.
Takwimu za Sweden zinaonyesha kuwa, hadi mwaka jana, raia wa Somalia karibu 70,000 walikuwa wakiishi nchini Sweden.