Matamshi ya Umit Özdag mwanasiasa wa Uturuki kuhusu Palestina yameibua radiamali kubwa katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Umit Ozdag, kiongozi wa Chama cha Ushindi cha Uturuki, amesema: ‘Mosul na Kirkuk ni muhimu zaidi kwetu kuliko Palestina.’ Matamshi ya kiongozi huyo ambaye ni mmoja wa wapinzani wa serikali ya Rais Recep Tayyip Erdogan, kuwa suala la Palestina halina umuhimu wa kitaifa kwa Uturuki yameibua kampeni haribifu dhidi yake ambapo wakosoaji wamemtuhumu kuwa anaunga mkono utawala wa Israel.
Amesema: ‘Wananituhumu kwa sababu nilisema kwamba Palestina si suala la kitaifa kwa Uturuki. Palestina hata haichukuliwi kuwa suala la pamoja kwa ulimwengu wa Kiarabu. Quds pamoja na maeneo yake matakatifu ina umuhimu maalum kwa Waturuki, lakini sio suala letu kuu la kitaifa.”
Ozdaq amekosoa undumakuwili wa serikali ya Uturuki kuhusu suala la Palestina na kusema: “Wakati wananchi wa Palestina huko Gaza wanakabiliwa na mauaji ya umati na kufukuzwa kwenye makaazi yao, lakini bado biashara ya Uturuki na utawala wa Israel inaendelea kuimarika. Wale wanaodai kuwa Palestina ni suala lao la kitaifa hawafanyi chochote isipokuwa kuzungumza na kuendeleza biashara kama kawaida.”
Kiongozi huyo wa chama cha “Ushindi” cha Uturuki amesisitiza kuwa “Mosul na Kirkuk, kama ardhi ya Waturuki na sehemu ya eneo la zamani la serikali ya Ottoman, ni muhimu zaidi kwa Waturuki kuliko Palestina. Pia ameorodhesha vipaumbele vya kitaifa vya chama chake na kusema: “Uzingatiaji wetu ni juu ya maslahi ya taifa la Uturuki. Hii ni pamoja na masuala kama vile Kirkuk na Mosul, Turkestan Mashariki (eneo linalojiendesha lenyewe la Uyghur nchini Uchina), Mediterania ya Mashariki, uhuru wa Jamhuri ya Uturuki ya Cyprus Kaskazini, Thrace ya Magharibi (kaskazini mashariki mwa Ugiriki na inayopakana na Uturuki), visiwa vya Uturuki vinavyokaliwa na Ugiriki katika Bahari ya Aegean na kujenga Jamhuri ya Uturuki yenye nguvu, iliyoungana na isiyo na dini.

Katika duru za kisiasa na vyombo vya habari vya Uturuki, ukosoaji mkubwa umefanywa dhidi ya serikali ya Erdogan kuhusu suala zima la Palestina. Moja ya ukosoaji mkubwa unaofanywa dhidi ya Rais wa Uturuki kuhusu kuendelea mauaji ya kimbari na jinai za utawala wa Kizayuni huko Gaza ni uhusiano wake wa kibiashara na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Kwa ujumla, katika miaka ya hivi karibuni, siasa za Uturuki kuhusu kadhia ya Palestina zimeambatana na migongano ya wazi. Wakati serikali ya Erdogan imekuwa ikikosoa jinai za utawala ghasibu wa Israel huko Gaza na kujionyesha kuwa ni muungaji mkono wa taifa la Palestina, uhusiano wake wa kiuchumi na kidiplomasia na Tel Aviv umekuwa ikiendelea kunawiri bila kikwazo chcochote. Tabia hii ya kinafiki imefanya wachambuzi na wakosoaji wengi kuchukulia madai ya uungaji mkono wa Uturuki kwa Palestina kuwa hatua za kipropaganda tu.
Serikali ya Uturuki imekuwa ikiutuhumu mara kwa mara utawala wa Israel kwa kukiuka haki za binadamu katika vikao vya kimataifa, vyombo vya habari na hotuba rasmi na kutaka kusitishwa mashambulizi dhidi ya Gaza, huku takwimu za kibiashara zikionyesha kuwa uuzaji na uagizaji wa bidhaa nje ya nchi kati ya Uturuki na utawala wa Kizayuni haujasimama, si tu katika miaka ya hivi karibuni, bali pia umeongezeka katika baadhi ya vipindi. Tofauti hii kati ya hotuba za kisiasa na mienendo ya kiuchumi ya viongozi wa serikali ya Uturuki ni moja ya sababu kuu zinazofanya uungaji mkono huo wa kidhahiri kuwa wa kipropaganda tu.
Suala la Palestina katika anga ya kisiasa ya ndani ya Uturuki pia limekuwa chombo cha kuchochea hisia za kidini na kitaifa. Chama cha Haki na Maendeleo, chini ya uongozi wa Recep Tayyip Erdogan, hutumia madai ya kuunga mkono kwa Palestina wakati kinapokumbwa na changamoto au wakati wa chaguzi za kisiasa kwa ajili ya kuimarisha nafasi yake miongoni mwa raia wa nchi hiyo. Hii ni katika hali ambayo hatua eti za kuwaunga mkono Wapalestina mara nyingi huishia tu kwenye propaganda za kisiasa zinazoenezwa kwenye vyombo vya habari. Nchi nyingi za Kiarabu na Kiislamu pia zinachukulia madai ya uungaji mkono wa serikali ya Uturuki kwa Palestina kuwa yasiyo ya kweli na kuwa ni pozi za kidiplomasia tu.
Jamii ya Waturuki, hasa makundi ya vijana wa Kiislamu, inashughulishwa sana na suala la Palestina. Ili kudumisha umaarufu miongoni mwa makundi haya, serikali inalazimika kuchukua misimamo ya kimaonyesho na kipropaganda tu kuhusu kadhia ya Palestina. Misimamo hiyo mara nyingi huonekana katika mfumo wa tweet za kihisia, hotuba kali au kuhudhuria mikutano ya kuchangisha misaada ya kibinadamu, lakini pamoja na hayo haipewi uzito wowote wa maana katika kiwango cha sera kuu za nchi.
Siasa za Uturuki kuhusu Palestina, kabla ya kuegemea kwenye msingi wa stratijia madhubuti, ni chombo tu kinachotumiwa na wanasiasa kwa ajili ya kuvutia maoni ya umma, kuendesha mashindano ya ndani kisiasa na kudumisha nafasi ya kidiplomasia ya Ankara katika ulimwengu wa Kiislamu. Ingawa mtazamo wa kisiasa na kipropaganda wa serikali ya Uturuki kuhusu Palestina, huenda ukafanikiwa katika kipindi cha muda mfupi, lakini bila shaka utapelekea itibari yake ya kidiplomasia katika eneo kukabiliwa na changamoto kubwa katika kipindi cha muda mrefu.