
Gazeti la Politico la nchini Italia limeripoti kuwa chama tawala nchini humo cha Brothers of Italy kimesema, kinapanga kuwasilisha mswada bungeni wa kupiga marufuku wanawake wa Kiislamu kuvaa vazi la burqa na niqabu katika maeneo ya umma, kikitaja sababu ya kufanya hivyo kuwa ni kupinga ilichokiita “utengano wa Kiislamu”.
Mbunge Andrea Delmastro, mmoja wa waanzilishi wa mswada huo ameandika kwenye ukurasa wake wa Facebook: “uhuru wa kidini ni kitu kitakatifu, lakini lazima utumiwe hadharani, kwa kuonyesha heshima kamili kwa katiba yetu na kanuni za taifa la Italia”.
Burqa ni vazi la baibui mwili la mwili mzima linalomfunika mwanamke kuanzia kichwani hadi miguuni na linajumuisha kizoro cha tundutundu kwenye macho; na niqabu ni kitambaa kinachoziba uso na kuacha wazi eneo karibu na macho.
Endapo itapitishwa kuwa sheria, marufuku hiyo itakataza watu kuvaa mavazi hayo katika maeneo ya umma kama vile maduka, skuli na ofisi; na atakayekaidi kutekeleza amri hiyo atatozwa faini ya kuanzia yuro 300 hadi 3,000 ($349 hadi $3,491).
Pendekezo hilo ni sehemu ya mswada mpana ambao chama tawala cha mrengo wa kulia cha Waziri Mkuu Giorgia Meloni kimeuita kama mpango wa kukabiliana na “utengano.”
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, Sara Kelany, mkuu wa masuala ya uhamiaji katika chama cha Brothers of Italy amesema: “ni mswada unaolenga kudhibiti ufadhili wa misikiti na kupiga marufuku vazi linaloziba uso mzima. Pia unalenga kukabiliana na ndoa za kulazimishwa na utayataka makundi ya kidini yasiyotambuliwa na serikali kufichua ufadhili wa fedha yanayopata kutoka nje”…/