Baada ya kutangazwa makubaliano ya usitishaji vita katika Ukanda wa Ghaza na ya kubadilishana mateka kati ya utawala wa Kizayuni wa Israel na Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS, vyombo vya habari na duru za kisiasa za ndani ya utawala wa kizayuni zimetoa lawama kwa kuashiria matokeo ya vita na kuendelea kubaki thabiti miundo na mihimili ya Muqawama ndani ya Ghaza.

Vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni vimetoa makala na maandiko kadha wa kadha vikionyesha kutoridhishwa na matokeo ya vita dhidi ya Ukanda wa Ghaza baada ya kufikiwa makubaliano ya usitishaji mapigano na vimepinga kuendelea kuwepo Muqawama wenye uwezo katika eneo hilo.

Yariv Levin, naibu waziri mkuu na waziri wa sheria wa utawala wa Kizayuni, ndiye aliyeko katika mstari wa mbele kwa wakosoaji na ameyaelezea makubaliano hayo kuwa ni kitu chenye “gharama kubwa mno” na akasema: “kuwaachilia huru Wapalestina kuna gharama kubwa mno. Sisi tutaendelea kufanya juhudi ili kuhakikisha Hamas haiwi tena na silaha wala udhibiti wa Ghaza”.

Katika mjibizo liliotoa kwa matamshi ya Levin, jukwaa moja la habari la utawala wa kizayuni limeandika: “hadithi ilianzia kwenye kuangamizwa Hamas hadi kupokonywa silaha… lakini kwa maneno mengine ni kwamba, Hamas inasalia Ghaza.” Jukwaa hilo limetumia lugha hiyo ya mafumbo na kejeli kutoa mjibizo kwa kauli ya naibu waziri mkuu huyo na waziri wa sheria wa utawala wa kizayuni.

Mchambuzi wa masuala ya Kiarabu Tsef Hezekili yeye ameeleza katika kutoa tathmini yake kwamba “Hamas haijatoweka na wala haijaangamizwa”. Kisha akauliza: “Je, sisi tumeshinda? Je, itikadi mbaya inayoua ya Hamas si tishio kwetu?”

Kwa upande mwingine, mwandishi wa habari wa magazeti wa Israel Baruch Yedid, yeye ameelezea kutoridhishwa na kifungu kinachohusu kuachiliwa huru Wapalestina wanaoshikiliwa kwenye magereza ya utawala wa kizayuni, na akaandika: Hamas itafanikiwa kuyafanya magereza yabaki matupu, wakati kiwango cha muda wake wa kusalia huko Ghaza bado hakijajulikana.

Avi Yassahroff, mchambuzi wa masuala ya Kiarabu katika gazeti la Yedioth Ahronoth yeye ameandika kuwa, Hamas imeushinda utawala wa Kizayuni katika ulingo wa kisiasa na kimataifa na akaongezea kwa kusema, uharibifu na idadi kubwa ya wahanga itazidisha chuki dhidi ya utawala wa Kizayuni, si huko Ghaza tu au Ukingo wa Magharibi, bali duniani kote. Hamas inasalia Ghaza na imeushinda utawala wa Kizayuni katika uga wa kisiasa na kimataifa, huku chuki dhidi ya utawala huo ikiongezeka, si Ghaza pekee au katika Ukingo wa Magharibi, bali ulimwenguni kote.

Yassahroff aidha amesisitiza kuwa, unapotembelea mji wowote wa Ulaya sasa hivi utakuonyesha hali tofauti za namna utawala wa Kizayuni ulivyoshindwa kisiasa.

Mwanahabari huyo wa kizayuni ameashiria mijumuiko na mikusanyiko ya kuonyesha mshikamano na Ghaza inayoshuhudiwa barani Ulaya, na kusema, anaamini kwamba Hamas imefanikiwa kuhamasisha umma mahali ambapo, kwa maelezo yake, baraza la mawaziri la utawala wa kizayuni limeshindwa.

Maandamano makubwa ya kuunga mkono Ghaza nchini Marekani

Avi Yassahroff ametahadharisha kwa kusema: “tatizo kubwa zaidi ni kushindwa waziwazi serikali ya Israel kubadilisha mwelekeo wa maoni ya umma nchini Marekani, wakiwemo Warepublican. Kutambuliwa rasmi nchi ya Palestina na nchi kubwa za Magharibi ni moja ya mafanikio ya kisiasa iliyopata Hamas, ambayo ni matokeo ya kutokuwa na mkakati serikali ya Israel”.

Misimamo yote hii tuliyoashiria ilitangazwa mara baada ya duru za Palestina pamoja na vyombo vya habari vya utawala wa kizayuni ikiwemo Chaneli ya 12 kutangaza mchana wa jana Alkhamisi kwamba usitishaji vita huko Ghaza ungeanza kutekelezwa saa sita mchana kwa saa za Ghaza kufuatia makubaliano rasmi yaliyofikiwa katika mazungumzo ya Sharm el-Sheikh nchini Misri. Hata hivyo, ofisi ya waziri mkuu wa utawala wa kizayuni ilikanusha utekelezwaji wa makubaliano hayo ikisema, hilo halitajiri ila baada ya uamuzi huo kuidhinishwa kwanza na baraza la mawaziri la Israel pamoja na bunge la utawala huo wa kizayuni Knesset…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *