Taarifa ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu na Msaada wa Dhaura OCHA iliyotolewa Alhamisi imesema kwamba Vikosi vya Msaada wa Haraka RSF vilifyatua risasi Jumanne na Jumatano wiki hii katika Hospitali ya Saudi na msikiti wa eneo hilo, ambako familia zilizokimbia makazi yao zilikuwa zikipata hifadhi.
OCHA imesema kupitia mtandao wake wa X kwamba Hospitali ya Saudi “ndiyo kituo pekee cha afya kinachofanya kazi mjini humo, kikihudumia maelfu ya watu waliokumbwa na vita.”
Huduma za afya chini ya mashambulizi
OCHA “imepinga vikali mashambulizi hayo na mengine yaliyotekelezwa hivi karibuni na RSF mjini El Fasher eneo la mwisho linalodhibitiwa na serikali ya Khartoum katika jimbo la Darfur, ambako njaa imetangazwa tangu mwaka jana.
“Raia hawapaswi kushambuliwa kamwe,” OCHA imesisitiza. “Tunarejea wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa kusitisha mapigano mara moja.”
Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu na Afya ya Uzazi UNFPA limesema shambulio la Jumanne lililenga wodi ya wajawazito na kuua watu 12 na kuwajeruhi wengine wengi, wakiwemo wagonjwa na wahudumu wa afya.
“Shambulio hili ni la tatu dhidi ya hospitali hiyo ndani ya wiki moja,” Shirika la UNFPA limesema, likitoa wito wa “kusitishwa mara moja kwa mapigano, ulinzi wa raia na vituo vya afya, na upatikanaji salama wa misaada ya kibinadamu kwa walio katika mahitaji ya dharura.”
Umoja wa Mataifa unatoa msaada wa chakula kwa jamii ambazo zimelazimika kukimbia makazi yao.
Wakazi wa El Fasher wako katika hofu
Kwa mujibu wa Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stéphane Dujarric, wakazi wa El Fasher “wamenaswa katika vita, wanaishi kwa hofu na wametengwa na misaada, huku tumaini lao la mwisho la huduma za afya likiwa hatarini.”
Ameongeza kuwa, “bila hata kusema, kulenga hospitali ni tendo la kulaaniwa na halikubaliki kamwe.”
El Fasher imekuwa chini ya mzingiro kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Katika miezi ya hivi karibuni, RSF ambayo hapo awali ilikuwa jeshi la Janjaweed lililotuhumiwa kufanya ukatili dhidi ya jamii zisizo za Waarabu mwanzoni mwa miaka ya 2000 imeongeza mashambulizi ya mizinga na ndege zisizo na rubani katika juhudi za kuuteka mji huo.
Vita vya wenyewe kwa wenyewe vyazidisha maafa
Zaidi ya Darfur, nchi nzima ya Sudan inaendelea kugubikwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoanza Aprili 2023, na kusababisha moja ya migogoro mikubwa ya kibinadamu duniani, ambapo zaidi ya watu milioni 30 wanahitaji msaada.
Takribani watu milioni 12 wamelazimika kuyahama makazi yao, wakiwemo zaidi ya watu milioni 4 waliokimbilia nchi jirani kama Chad na Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Oktoba 7 na 8, timu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji IOM liliripoti watu 250 waliokimbia mji wa Kernoi, karibu na mpaka wa Chad, kufuatia mapigano ya kikabila kati ya wanachama wa kabila la Zaghawa, moja ya makabila makubwa yasiyo ya Kiarabu katika eneo hilo.
Mwanamke anapekua mabaki yaliyoteketezwa ya makazi yake katika kambi ya watu waliokimbia makazi yao huko Darfur, Sudan.
Maelfu wakimbia El Fasher na kambi za wakimbizi
Raia wanaendelea kukimbia El Fasher na kambi ya wakibizi wa ndani ya Zamzam, ambako idadi ya watu imepungua kwa asilimia 70 katika kipindi cha miezi sita iliyopita.
Wahudumu wa kibinadamu wanakadiria kuwa idadi ya watu katika eneo hilo imepungua kutoka 700,000 mwezi Machi hadi 200,000 mwezi Septemba.
Maelfu ya familia zimekimbilia miji jirani kama Tawila, ambayo sasa inahifadhi takribani watu 600,000 waliopoteza makazi.
Wakati Umoja wa Mataifa na washirika wake wakiendelea kujitolea kusaidia watu wa El Fasher na Sudan kwa ujumla, Bwana Dujarric amesisitiza umuhimu wa upatikanaji salama wa misaada ya kibinadamu, ulinzi wa raia, na kusitishwa kwa mapigano mara moja ndani na nje ya jiji hilo.