
Ni Jane Doe, mmoja wa wanawake waliothubutu kuvunja ukimya. Akiwa ametoka kwenye ndoa yenye changamoto na dhuluma, alipata msaada kupitia bingwa wa kijamii katika kijiji chao
Kwa kushirikiana na wadau wa mashinani kama Samburu Women Trust, CREAW ambacho ni kituo cha haki, elimu na ulimishaji, Kituo cha Sheria, na Chuo Kikuu cha Egerton pamoja na juhudi za wanawake binafsi simulizi za ukandamizaji kama alioupitia Jane zinageuka kuwa hadithi za ushindi. Huduma za msaada wa kisheria zinawafikia waliokuwa wamesahaulika, na elimu ya sheria inazalisha mawakili wa kizazi kijacho wenye maono ya mabadiliko.
Jane anasimulia alivyopata msaada,
“Huko Kijijini, nilikutana na mchechemuzi mmoja nikazungumza naye, na akaniambia kuhusu CREAW. Nilimweleza changamoto niliyokuwa napitia, naye akanipa mawaidha ambayo yalinisaidia sana. Kwa kweli nilikuwa nimefika kiwango cha kujitoa uhai. Baadaye nilipata fursa ya kujiunga na mradi ambao nilipata mtaji wa kuanza biashara”
Hadithi za mabadiliko haziishii hapa. CREAW inaongoza juhudi katika kukabiliana na ukatili wa kijinsia. Jane Anaongezea,
“Baada ya kesi ya mahakamani kuamuliwa,mume wangu alipewa maagizo ya kumlea mtoto na kufanya yale mahakama iliyosema.Nimefurahi kwa sababu nikitaka kula vizuri, nitakula chochote nitakachotaka. Mtoto wangu ana furaha, nami naishi vizuri. Nina uwezo wa kifedha, na moyo wangu umejaa furaha. Mungu awabariki sana.”
Mnufaika mwingine ni Jessica Nekesa ambaye msaada wa kisheria umemsaidia kutetea haki yake ya kumiliki ardhi, na anasema,
“Mwaka 2001, mwezi wa sita, mume wangu aliaga dunia. Wakati huo nilikuwa nyumbani, kisha nikaja mjini kuangalia shamba tulilokuwa tumenunua pamoja na marehemu . Nilipofika, nilikuta mashemeji zangu tayari wameliuza, na mtu mwingine alikuwa ameshajenga nyumba ndani ya hilo shamba. Tuliwasiliana na shirika la haki za binadamu , tukafuatilia hadi kufika kwenye kikao cha wazee. Hapo ndipo nilipopata kibali cha kurudi katika shamba langu baada ya kupigania haki yangu kwa miaka ishirini.”
Vilevile, Chuo Kikuu cha Egerton, ambacho ni Chuo cha Sheria, kinaandaa wanasheria wa baadaye wa Kenya kwa kuunganisha nadharia na huduma za bure za kisheria zenye athari chanya. Joys Nyokabi aliyefaidia na huduma hiyo anasema
“Nilikumbwa na changamoto ya kupata msaada wa kisheria na ufuatiliaji wa haki zangu za umiliki wa ardhi baada ya mume wangu kufariki dunia. Wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Egerton walitufundisha kuhusu masuala ya kisheria. Baadaye, nilifikishwa mahakamani, lakini sikuwa na uwezo wa kifedha kuajiri wakili. Hata hivyo, nilipata msaada mkubwa kutoka kwao, jambo lililonipa faraja na furaha sana. Mawakili walinisaidia kwa ukamilifu na kushughulikia matatizo yangu yote. Kwa sasa, nina hati miliki ya ardhi hiyo, ambayo imeandikishwa kwa jina langu pamoja na ya watoto wangu”.