
Kwa mujibu wa UNHCR, idadi hii ni ongezeko la takriban asilimia 66 ndani ya miaka mitano tu, kutokana na usalama duni, athari za mabadiliko ya tabianchi, na kupungua kwa huduma za kijamii na fursa za kujikimu.
“Kiwango na kasi ya wakimbizi katika Ukanda wa Sahel ni cha kutisha. Watu wanakimbia makazi yao kutokana na ukosefu wa usalama, njaa, na athari za mabadiliko ya tabianchi,” amesema Abdouraouf Gnon-Konde, Mkurugenzi wa Kanda wa UNHCR kwa Afrika Magharibi na Kati, akizungumza leo mjini Geneva.
Ameongeza kuwa “Tunahitaji tahadhari na mshikamano wa kimataifa mara moja kwani watu wa Sahel hawawezi kukabiliana na janga hili peke yao.”
Ukosefu wa usalama na katili unaokumba wanawake na watoto
Wanawake na watoto ni asilimia 80 ya waliokimbia makwao, na UNHCR inaripoti ongezeko kubwa la ukatili wa kijinsia, usajili wa kulazimishwa, na uwekwaji kizuizini usio wa haki.
“Ukosefu wa usalama unawapotezea watoto elimu na usalama, na wanawake huchukuliwa huru wao na heshima,” amesema Gnon-Konde. Hadi sasa, zaidi ya shule 14,800 zimefungwa, zikiacha watoto milioni 3 bila elimu, huku zaidi ya zahanati 900 pia zikiwa zimefungwa.
UNHCR imesisitiza kuwa kufungwa kwa shule na zahanati kumeongeza mateso ya familia zilizokimbia, na wengi wanachukua safari hatari kwenda nchi za jirani kutafuta usalama na fursa.
“Wakati watu wanapokosa elimu na huduma za afya, matumaini hupotea na kukosa matumaini kunasababisha wakimbizi wengi zaidi,” ameongeza.
Chakula haba na athari za tabianchi vinaongeza wakimbizi
UNHCR inasema kuwa ukosefu wa chakula umekuwa sababu kubwa ya wakimbizi kuhama, huku idadi ya watu waliokimbia makwao wakirejelea njaa kama sababu yao ya kuhama ambayo imeongezeka mara mbili katika miaka ya hivi karibuni. Athari za tabianchi, ikiwa ni pamoja na ukame na mafuriko, UNHCR inasema pia zinazidisha ushindani wa rasilimali chache kama ardhi na maji, na kudhoofisha mshikamano wa kijamii.
“Mabadiliko ya tabianchi si tatizo la mazingira tu katika Ukanda wa Sahel ni janga la kibinadamu. Familia zinafanywa kuchagua kati ya njaa na kukimbia,” amesema Gnon-Konde na kuongeza kuwa “Tunahitaji kuimarishamnepo ili watu waendelee kuishi karibu na makazi yao na kuepuka safari hatari.”
Upungufu wa rasilimali unatishia huduma muhimu
Licha ya mahitaji kuongezeka, mashirika ya kibinadamu katika Ukanda wa Sahel yamekosa rasilimali muhimu.
Kati ya dola za Marekani milioni 409.7 zinazohitajika kufidia mahitaji ya kibinadamu mwaka 2025, asilimia 32 tu ndio zimekusanywa.
Upungufu huu umefanya UNHCR kupunguza shughuli muhimu kama usajili, huduma za afya, elimu, na makazi.
Zaidi ya wakimbizi na waomba hifadhi 212,000 nchini Burkina Faso, Mali, na Niger bado hawajasajiliwa hali inayowafanya kuwa hatarini zaidi, ikiwa ni pamoja na kuwekwa kizuizini bila haki na unyanyasaji. Limesema shirika hilo la wakimbizi.
“Bila usajili sahihi, watu hawa hawaonekani na kutokuonekana kunamaanisha hatari,” Gnon-Konde amesisitiza.
Jamii zinatoa ushindi hata katika hali ngumu
Licha ya hali ya hofu, UNHCR imeangazia mnepo na mshikamano wa ajabu unaooneshwa na jamii za wenyeji katika eneo la Sahel.
Nchini Mali, asilimia 90 ya waliokimbia wameripoti kuhisi ujumuishwaji na jamii za wenyeji zinazoshirikiana nao rasilimali chache.
Nchini Burkina Faso, mfumo wa jadi umewezesha kudhibiti mizozo kati ya wakimbizi na wenyeji.
“Roho ya ukarimu tunayoiona katika jamii hizi ni ya ajabu. Wanajitahidi sasa jamii ya kimataifa lazima pia itoe msaada wake,” amesema Gnon-Konde.
Wito: ushirikiano wa kimataifa uendelee
UNHCR inataka mshikamano wa kimataifa kwa Sahel, ikisisitiza kuwa nchi husika zote zilizo chini ya Mkataba wa Wakimbizi wa 1951 na Mkataba wa Kampala haziwezi kushughulikia janga hili peke yake.
Imeongeza kuwa “Kulinda mamilioni ya familia waliokimbia makwao kunahitaji zaidi ya maneno, kunahitaji hatua za pamoja na endelevu,” ameongeza Gnon-Konde.
Amebainisha kuwa asilimia 75 ya wakimbizi bado wako ndani ya nchi zao, na wengi hawana uwezo wa kuvuka mipaka kutokana na ukosefu wa usalama au vikwazo.
Amehitimisha kwa kusema kuwa Watu hawataki kuondoka wanataka usalama. Ni jukumu letu sote kuhakikisha wanapata.”