Tumbuizo za  nyimbo za kihindu zikiendelea, na makumi ya maelfu ya watu wameminika kwenye sherehe hii ambayo hufanyika katika jimbo la Bengal Magharibi nchini India. Hapa ibada kwa mungu wao Durga huunganishwa na sanaa pamoja na ujumbe wa kijamii. Maonesho hufanyika kwenye mabanda maalum. 

Mnamo mwaka 2021, UNESCO ilitambua Puja Durga kama sehemu ya turathi za dunia za tamaduni zisizoshikika . Puja Durga ilianza kama ibada ya kifamilia, lakini sasa huko Kalkuta imegeuka kuwa sherehe ya mji mzima inayochangamka – pengine sherehe kubwa zaidi ya sanaa duniani.”

Urithi huu ni jadi hai – inayobuniwa upya kila mwaka kwa kutumia maudhui na mawazo mapya, kama asemavyo Shombi Sharp, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini India.

“Tumetembelea eneo moja lililokuwa la kufumbua macho sana kuhusu manusura wa mashambulizi ya tindikali – onesho linalotunza sio tu utu wao bali pia kuheshimu nguvu yao. Na kufikiria kuwa mamilioni ya watu wanapokea ujumbe huu, inabadilisha fikra zao, na kuwafanya wafikirie upya.”

Eneo lingine la onesho liitwalo Neer, lina mada ya uhifadhi wa maji, likiwa na birika za maji zilizotengenezwa kwa udongo, hili liliwavutia sana wageni vijana, kama asemavyo mmoja wa wakazi wa Kalkuta, Tithi Ghosh.

“Wakati wageni wanapewa ujumbe kama kuhifadhi maji, watu huanza kuelewa umuhimu wake na kujitahidi kutoyatumia vibaya.”

Hema lingine limejikita kwenye akili bandia au akili unde, ikimuonesha mungu wa kike Durga katika umbo lake la kitamaduni, lakini kwa nyuma kulikuwa na miundo ya kidijitali, michoro ya maumbo ya mzunguko na sanamu za roboti. Ujumbe ulikuwa wazi – imani na teknolojia vinaweza kuishi pamoja. Mkazi mwingine wa hapa Kalkuta Sumitam Shoum anasema,

“Akili mnemba inaweza kufanya mambo makubwa, lakini pia ina hatari. Picha bandia na udanganyifu vinaweza kuongezeka. Teknolojia inapaswa kutumiwa kwa uwajibikaji.”

Hema lingine liitwalo Shabdo  au sauti kwa kiswahili, limelenga sauti zinazopotea za asili – kelele za ndege, mshindo wa majani, na milio ya vyura. Hata ni tafakari yenye nguvu kuhusu upotevu wa mazingira na kupotea kwa sauti ya asili mijini. Mkazi kutoka Kalkuta, Raja anasema..

“Tulichagua mada hii kwa sababu ndege hawaonekani tena kama zamani. Hema hili linatufanya tufikirie jinsi ya kurejesha mazingira ya asili.”

Hema lililorejesha zaidi ya miaka 100 iliyopita limemulika kilimo endelevu. Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa India, Shombi Sharp anasema,

“Mwaka huu, mada zimekuwa za kuhamasisha sana – unaona Mungu wa kike Durga akiwa nyuma yetu akisherehekea mifumo ya chakula ya asili na kilimo endelevu. Kwa kawaida, Mungu wa kike Durga huonekana akishinda uovu, lakini hapa ‘uovu’ anaoshinda ni dawa za kuua wadudu na mbinu zisizoendelevu za kilimo. Hivyo ni uzoefu wa kuvutia sana.”

Kwa ujumla, Puja ya Durga inathibitisha kuwa urithi si wa zamani tu – bali pia ni njia ya kuunda maisha ya baadaye.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *