Kufuatia kutangazwa makubaliano ya kusimamisha vita na kubadlishana mateka kati ya Israel na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas), Itamar Ben -Gvir Waziri wa Usalama wa Ndani wa utawala wa Kizayuni ametangaza kupinga vikali makubaliano hayo na kutishia kulimbaratisha baraza la mawaziri la Netanyahu.
Itamar Ben- Gvir amesema kuwa Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni alimuahidi kuwa angeivunja Hamas na kusema: Kama hilo halitafanyika yeye na mawaziri wenzake watalivunja baraza lake la mawaziri.
Inaonekana kuwa migogoro ya nyuma ya pazia imepamba moto ndani ya baraza la mawaziri la wapenda vita la utawala wa Kizayuni baada ya kupasishwa makubaliano ya kusimamisha vita na kubadilishana mateka kati ya Israel na Hamas ambapo hivi sasa Ben -Gvir ametishia wazi kuivunja serikali ya mseto ya Israel.
Ametoa makataa ya wazi ambapo amesisitiza kuwa harakati ya Hamas inapasa kuvunjwa kama sharti la kusalia mamlakani baraza la mawaziri la Netanyahu; la sivyo, chama cha Jewsih Power kitajitoa kwenye serikali hiyo ya mseto; tishio ambalo si tu linamkabili Netanyahu bali limeuweka muundo wote wa kisiasa wa Israel katika zilzala tarajiwa ya kisiasa. Hasa ikizingatiwa kuwa kura yake ya hapana pamoja na Bezalel Smotrich Waziri wa Fedha wa utawala lwa Kizayuni mwenye misimamo mikali dhidi ya makubaliano hayo imeanika wazi hitilafu kubwa za kiadiolojia zilizopo ndani ya utawala huo.
Smotrich amesema kuwa Israel inapasa kuiharibu Gaza kikamilifu baada ya kuachiwa huru mateka wa Kizayuni kutoka Gaza.
Mivutano hii mikubwa si tu inaashiria kutoafikiana kimbinu kuhusu makubaliano ya kusitisha vita katika Ukanda wa Gaza, bali ni ishara ya kuwepo mzozo mkubwa baina ya malengo ya kiitikadi ya mrengo wa kulia wa Israel na uhakika wa mambo wa maidanini na katika uga wa kisiasa.
Mrengo wa kulia wenye itkadi kali wa Israel ambapo Ben-Gvir ni mwanachama mwenye ushawishi mkubwa humo, unanyoosha kidole cha lawama si tu dhidi ya Netanyahu pekee, bali dhidi ya doktrini nzima ya kijeshi na kisiasa ya Israel, lengo lake likiwa ni kuendeleza uvamizi na kuharibu misingi yote ya muqawama; doktrini ambayo kivitendo inachochea kuendelezwa vita vya pande zote ambavyo hadi sasa havijakuwa na manufaa yoyote ghairi ya kusababisha uharibifu na kutengwa Israel kimataifa.

Kwa hakika vitisho vya Beb-Gvir ni mchezo wa utunishaji misuli wa pande mbili; kwa upande mmoja, anajaribu kumlazimisha Netanyahu kuchukua msimamo mkali zaidi dhidi ya Hamas ili kulinda nafasi yake ya kura, na kwa upande mwingine, kwa kuibua mgogoro huu, amekusudia kumkwamisha kimkakati Netanyahu; hatua ambayo hatimaye itadhoofisha nafasi ya Netanyahu na kuandaa uwanja wa kurithiwa nafasi yake na shakhsiya mwingine mwenye mielekeo ya mrengo wa kulia. Uchukuaji maamuzi huu wa pande mbili za sarafu moja ni sababu kuu ya kusambaratika kutokea ndani utawala wa Israel. Baraza la mawaziri la Netanyahu limegawanyika katika sehemu mbili; mosi, kuna kundi ambalo linafahamu wazi kuwa hakuna njia nyingine ila kufanya mazungumzo ili kuwarejesha nyumbani mateka, na kundi jingine ni lile linaloongozwa na Ben-Gvir na Smotrich ambalo linaamini kuwa hatua yoyote ya kusalimu amri na kuachana na malengo yaliyotangazwa ina maana ya kusaliti malengo ya itikadi yao. Wamesema kuwa wako tayari kuisukuma Israel kuelekea uchaguzi wa mapema na hivyo kuvuruga uthabiti wa utawala huo. Lengo la mwisho ni kuisambaratisha Hamas; suala ambalo limeshupaliwa na Ben-Gvir. Jambo hilo si lengo la kimbinu bali ni dharura ya kiaidiolojia ambayo hata kama ni vigumu kuitekeleza lakini kutowezakena huko kunakozungumziwa ni kadi ya turufu iliyowekwa mezani hivi sasa na Ben-Gvir.
Hitilafu zote zinazoshuhudiwa ndani ya utawala wa Israel si tu kuwa zinaonyesha udhaifu wa baraza la mawaziri la utawala huo lakini pia zinathibitisha kushindwa kwa operesheni kubwa ya kijeshi huko Gaza; ingawa Netanyahu anajaribu kila awezalo kuiridhisha Washington, kudhihirisha kwamba muungao huo bado upo na pia kuzuia kuvunjika baraza la mawaziri, hata hivyo makundi yenye itikadi kali kama vile chama cha Jewish Power kinaamini kuwa usitishaji vita wowote wa kudumu unamaanisha mwisho wa uwepo wao katika muungano huo.