KWA hiyo aliamini angeweza kuyatengeneza maisha yake katika bara hilo na pindi atakaporudi nchini apate nafasi ya kuwatambia watu waliokuwa wakimbeza.
Muddy aliamini akirudi Tanzania angekuwa na maisha mazuri sana akilimiliki magari ya kifahari kama haitoshi angeweza kurudi na mwanamke wa Kizungu.

********
“IKO siku mtaniheshimu humu ndani pindi mambo yangu yatakapokaa sawa,” alisema Muddy kwa hasira akilalamika baada ya kurudi nyumbani na kukuta ndugu zake wameshamaliza chakula chote cha usiku.
Siku hii hakuwa na budi ya kulala njaa kwa kuwa chakula kilikuwa kimekwisha na utaratibu wa familia hiyo kila mmoja alitakiwa kuwapo nyumbani kuanzia saa mbili kasarobo za usiku ili kula chakula cha pamoja. 
Ulikuwa ni utaratibu waliojiwekea wao wenyewe, kwamba usipokuwapo nyumbani muda huo na lako halipo, inakuwa imekula kwako, utakuta watu wameshakwangua mpaka sufuria na kumaliza hadi ukoko.
Ndugu hao ni kama walikuwa wakikomoana pale walipogundua mmoja wao hayupo, walichokuwa wakifanya walihakisha chakula hakibaki hata kama wameshiba watalazimshana kukimaliza kwa lengo la kumkomoa mhusika ili aheshimu ratiba walizojiwekea.
Watu pekee ambao wangeweza kuachiwa chakula pindi wanapokosekana nyumbani ni mzee Tuesday Manyara na mkewe kwa sababu wao ndiyo waliokuwa wakiihudumia nyumba hiyo kwa kutoa pesa na kupanga bajeti nzima ya chakula.
Lakini kama mtoto yeyote angekosekana, hakuna mtu ambaye angehangaika kumuwekea chakula. 
Ndivyo ilivyotokea kwa Muddy, ambaye alilazimika kulala njaa huku akihesabu mabati na kupiga miayo usiku mzima.
Siku inayofuata Muddy aliamka na njaa ikiwa inamkwangua, lakini hakutaka kuiendekeza, wazo la kwanza aliloamka nalo ni kuwashawishi ndugu na wazazi wake waiuze nyumba yao ili kila mmoja akatafute maisha yake mbele ya safari.
Katika fikra zake aliamini nyumba hiyo ingeuzwa na yeye angepata mgao wake, mambo yake yangemnyookea kwa kuyatengeneza maisha yake na kuwa bora zaidi.
Kwanza angehakikisha anapata hati ya kusafiria passport na pia angekuwa na uhakika wa safari yake ya Ulaya kwenda kutafuta maisha bora zaidi kutokana na pesa ambazo angebaki nazo.
“Ni heri kila mtu afe na chake,” aliwaza huku akipiga hesabu za kuwashawishi ndugu na wazazi wake wakubaliane na wazo lake la kuuza nyumba.
Muddy alianza ushawishi wake kwa ndugu zake kwa kumfuata mmoja baada ya mwingine na kuwaeleza sera zake, lakini kwa bahati mbaya hakuna aliyemwelewa.
Hata alipowaita wote kwa pamoja na kujaribu kuwaelewesha ilikuwa kazi bure. Hoja zake ziligonga mwamba.
“Kaka tafuta kazi ya kufanya, tuna nyumba yetu maisha ni magumu, tukiuza tutakuwa wageni wa nani?” dada yake aitwae Maisha alimtolea uvivu.
“Nikiwa Ulaya nitakuwa nawatumia pesa za matumizi na ninaweza kuwanunulia nyumba na nikaijenga ghorofa,” alijaribu ushawishi wake.
“Wakati ukiwa Ulaya siye tutakuwa tunaishi wapi? Dada yake mwingine aitwaye Mina alimuuliza. 
“Unajua hili eneo letu la Kariakoo ni hot cake, wafanyabiashara wengi wanalihitaji,” Muddy alisema na kumeza mate.
“Kama tukitangaza kuuza wafanyabiashara wataligombea, hivyo tutapata pesa nyingi za kutosha kila mmoja wetu kununua nyumba yake katika maeneo ambayo nyumba sio ghali sana kama Mwananyamala, Mbagala, Chamazi, Chanika na kwingineko. Pia pesa nyingine miye nitaweza kwenda Ulaya…” alijibu kwa kujiamini.
“Unadhani baba na mama watakubali tuuze nyumba halafu tukaishi huko unakosema?” mdogo mwingine wa kiume aitwaye Meja naye alihoji.
“Ndio maana nimewaita nyie kwanza letu likiwa moja hakuna kitakachoshindikana, wale ni wazee na maisha yao yanaelekea ukingoni, sio vibaya wakienda kuishi maeneo ya pembeni kidogo ya mji kama Kigamboni au Mkuranga, Pwani ili kuwaepushia hizi kelele nyingi za honi za magari na bodaboda za Kariakoo.”
“Nani akakae nje ya mji? Tangu lini mtoto wa mjini akaenda kukaa shamba huko?” Meja aliendelea kumpinga kaka yake.
Muddy hakuwa akipatana na ndugu yake mwingine aitwaye Kizanda, huyu naye aliupinga mpango huo.
“Kuuza nyumba ni kukata tamaa ya maisha, ni dalili ya kushindwa na kutafuta njia ya mkato, alisema Kizanda.
“Nani uliyemuona amefanikiwa kwa kuuza nyumba? Wangapi tumewaona wameuza nyumba zao na kuishia kuabika hapa mjini?” aliendelea kusema Kizanda na kumtaka ndugu yake huyo akatafute kazi ya kufanya. 
Pamoja na ushawishi wake, Muddy hakupata ushirikiano wa kile alichokuwa akikitaka. Ndugu zake walimshinda kwa hoja. Na hata habari hizo za kutaka kuuza nyumba zilipowafikia wazazi wake, zilikutana na pingamizi jingine kali zaidi.
“Subiri miye nife ndio ufikirie mpango huo wa kuuza nyumba,” mama yake Bi Faudhia alimwambia.
“Tumekutafutia kazi umekataa, unashindwa kutafuta mtaji wa ndoto zako unafikiria kuuza nyumba,” mama yake aliongeza.
“Mtaji gani tena mama, wakati hii nyumba ndio mtaji wenyewe kwa sababu iko eneo zuri la kibiashara huu ndio urithi wa maisha yetu…?”
“Ndio maana nakwambia subiri hadi mimi na baba yako tufariki dunia ndio upate huo urithi unaoutaka,” aliongeza mama yake na kumwambia urithi huwa hauji hivi hivi.
“Huwezi kurithi nyumba bila ya kumwaga machozi ya uchungu…” alisema mama yake bila ya kumfafanulia. 
Baba yake mzee Tuesday Manyara alikuwa ndani na aliyasikia maneno yote yaliyokuwa yakizungumzwa na mkewe pamoja na mwanaye, akashindwa kuyavumilia maneno ya mwanawe akatoka nje akiwa amechukizwa na hatua hiyo aliyofikia mwanawe.
“Kama alivyokwambia mama yako, hapa hakuna nyumba ya kuuzwa,” mzee Tuesday Manyara alisema na kuendelea 
“Kama unataka kuuza nyumba jenga yako kwanza, hii hapa haiuzwi,” alisema mzee huyo na kumwambia mwanaye hadi amefikia umri aliokuwa nao hakupaswa kuendelea kuwa tegemezi katika familia hiyo na alipaswa kuondoka na kwenda kuishi maisha yake.
“Ndio maana nilitaka urithi wangu mapema, nikajitegemee…” alijitetea Muddy.
“Unajua ugumu wa urithi wewe? Urithi wa mali za wazazi wako hauji hivi hivi mama yako amekwambia urithi ni hadi umwage machozi,” alisema mzee Manyara.
“Katika maisha yangu sikuwahi kutegemea urithi wa baba yangu, nilitafuta mali yangu mwenyewe, nawe nenda katafute yako,” ndivyo mzee Manyara alivyohitimisha ndoto za Muddy za kutaka kuuza nyumba ya familia.
Baada mpango wa huo kukutana na pingamizi na kukatisha ndoto zake za kutaka kuuza nyumba, Muddy alifikiria njia nyingine ya kutafuta pesa ya kumiliki hati ya kusafiria kwanza.
Hatua ya kwanza, aliachana na kucheza mpira na muda mwingi akautumia kufanya jitihada za kutafuta kazi, kitu kilichomwingia akilini mwake haraka ni kuwa dereva.
Aliwatafuta watu waliokuwa wakimiliki magari aliokuwa akiwafahamu na kuwaomba ajifundishe kuendesha na akaweka mkazo katika ujuzi huo akaenda kusoma katika chuo cha udereva hadi akapata leseni ya udereva.
Muddy akaanza kuendesha daladala kwa muda mrefu, hapo alipata mafanikio kwa kiasi fulani lakini baadaye akaachana na kazi hiyo na kuanza kuendesha teksi.
Mtu aliyemuamini na kumpa gari yake kuendesha alikuwa ni rafiki wa baba yake, mzee Mangushi ambaye alikuwa akiishi katika kitongoji hicho cha Gerezani.
Baada ya kuipata gari hiyo na kuendesha kwa ajili ya biashara ya teksi, maisha ya Muddy yalibadilika na akawa anajitegemea katika chakula na hata baadhi ya mambo mengine ya msingi.

Hakuwa tena mtu wa kusubiri kengele ya chakula cha familia, wakati mwingine yeye ndiye aliyekuwa akiisaidia familia kununua chakula cha nyumbani kwao pindi mambo yalipokuwa yakienda kombo.
Kwa kiasi kikubwa maisha yake yalibadilika na watu wakaanza kumsifu kwa kumuona alikuwa na akili kuliko watoto wengine wote wa mzee Manyara.
Baba yake alimsifu sana mwanaye kwa kuwa na akili baada ya siku moja kuingia chumbani mwake.
“Umeona sasa umekuwa na akili, unafanya kazi yako na unajipatia kipato chako… hivyo ndivyo mwanaume anatakiwa kuwa… sio kufikiria kuuza nyumba…” baba yake aliwahi kumwambia.
Kitendo cha kuonekana kujituma na kujitafutia mkate wake wa kila siku kilimpa heshima kubwa Muddy nyumbani kwao na baba yake akampa chumba cha peke yake tofauti na ndugu zake wengine waliokuwa wakilala wawili kwenye chumba kimoja.
Kwa kipindi kifupi akiwa dereva wa teksi, Muddy alipata mafanikio makubwa sana na kitu cha kwanza alichokifanya ni kutafuta hati ya kusafiria baada ya kudunduliza pesa alizokuwa akizipata.
Pamoja na kuwa na mawazo ya kutaka kusafiri, pia hakuacha kukikarabati chumba alichopewa na wazazi wake, alimwita fundi akamtengenezea madirisha makubwa ya alminium kisha akamwita fundi wa kupiga plasta na baadaye akamalizia na fundi rangi.
Chumba kilipigwa rangi nyeupe iliyokuwa iking’ara na kuvutia huku chini ukipigwa mkanda wa rangi nyeusi.
Baada ya hapo, ndipo aliponunua samani za ndani kama kitanda chenye ukubwa wa sita kwa sita, kabati la nguo, redio na runinga kubwa. Kama haitoshi, Muddy hakuacha kukipamba chumba chake kwa taa za rangi mbalimbali za kuvutia.

Inaendelea…

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *