London, England. Alejandro Garnacho ameendelea kuthibitisha kuwa Chelsea hawakupoteza pesa walipomsajili kwa pauni milioni 40 kutoka Manchester United, baada ya kuibuka shujaa katika ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Wolves kwenye dimba la Stamford Bridge Jumamosi.

Bao la kwanza la Chelsea lilifungwa na beki Malo Gusto, ambaye alipiga kichwa kilichompa bao lake la kwanza kabisa katika mechi yake ya 165 kwa klabu na timu ya taifa.

Garnacho ndiye aliyetoa krosi hiyo, kabla ya kuongeza pasi nyingine kwa Pedro Neto aliyefunga bao la tatu na kufunga hesabu ya mechi.

Nyota huyo wa Argentina mwenye umri wa miaka 21 alionyesha kasi, ubunifu na utulivu, akitoa michango miwili ya mabao kwa mara ya kwanza katika Ligi Kuu.

Makocha na mashabiki walisema wazi kama ataendelea kwa kiwango hiki, thamani yake itadhihirika kuwa ni dili la bei nafuu kwa Chelsea.

Wakati mashabiki wakimshangilia kinda wa Kibrazil Estevão Willian, aliyetoa pasi ya bao dakika moja tu baada ya kuingia uwanjani, Garnacho ndiye aliyebeba mzigo mkubwa wa ushindi huu uliowapeleka The Blues hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi.

Palmer kurejea

Kabla ya mechi kuanza, Cole Palmer alionekana akitembelea vyumba vya waandishi wa habari Stamford Bridge.

Chelsea wana matumaini atarejea uwanjani mwishoni mwa mwezi huu, ikiwezekana kabla ya mechi dhidi ya Barcelona katika Ligi ya Mabingwa Ulaya au Arsenal katika Premier.

Urejeo wake unatarajiwa kumpunguzia mzigo Joao Pedro, ambaye licha ya kufunga bao la pili jana, ameonekana kuchoka kutokana na kucheza mechi nyingi mfululizo huku akiwa na majeraha madogo.

Kocha Enzo Maresca amekuwa akisisitiza kuwa Pedro bado hajakuwa fiti kabisa, lakini hana mbadala mwingine katika nafasi hiyo ya namba 10.

Delap ashindwa kuonyesha makali

Liam Delap, ambaye alitolewa kwa kadi nyekundu kwenye mechi ya Kombe la Carabao dhidi ya Wolves wiki iliyopita, alipata nafasi nyingine kuanza kikosini.

Hata hivyo, alishindwa kufanya lolote la maana, kabla ya nafasi yake kuchukuliwa na Estevão, ambaye alitoa pasi ya bao ndani ya dakika moja tu baada ya kuingia.

Kiwango cha mchezaji huyo kiliwafanya mashabiki wamshangilie kwa nguvu, wakimtaka aanze mechi zijazo.

Disasi arudi uwanjani

Katika upande mwingine, beki wa Kifaransa Axel Disasi aliyenunuliwa kwa paundi milioni 39 alichezea kikosi cha vijana wa Chelsea (U-21) dhidi ya Reading, akiongoza timu hiyo kama nahodha kwenye ushindi wa 4-1.

Inaelezwa kuwa klabu inamwandaa kupata mechi zaidi kabla ya dirisha la usajili la Januari, ili iwe rahisi kumuuza au kumtoa kwa mkopo.

Kwa sasa, safu ya ulinzi ya Chelsea inaonekana imara zaidi ikiwa na Wesley Fofana na Trevoh Chalobah, ambao wamecheza kwa ufanisi mkubwa dhidi ya Wolves.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *