Ismailia, Misri. JKT Queens inarusha karata yake ya kwanza leo kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ikiikabili Gaborone United ya Botswana katika Uwanja wa Canal Suez, Ismailia kuanzia saa 1:00 usiku kwa muda wa Tanzania.

Sababu mbili za msingi zinailazimisha JKT Queens kuibuka na ushindi katika mchezo huo ambao ni wa kundi B la mashindano hayo.

Kwanza ni ipate pointi tatu ambazo zitaifanya iwe na mwanzo mzuri katika mashindano hayo na kuiweka katika mazingira mazuri ya kutinga hatua ya nusu fainali.

Lakini sababu ya pili ambayo inailazimisha JKT Queens kuhakikisha haiondoki kinyonge kwenye mechi ya leo ni kufuta nuksi ya mwak 2023 ambapo ilipoteza mchezo wa kwanza wa kundi lake kwenye mashindano dhidi ya Mamelodi Sundowns kwa mabao 2-0.

Katika mchezo wa leo, silaha kubwa ya JKT Queens ni safu yake ya ushambuliaji ambayo inaundwa na nyota watatu ambao wana uwezo mkubwa wa kufumania nyavu ambao ni Stumai Abdallah, Jamila Rajabu na Winfrida Gerard.

Wawakilishi hao wa Tanzania wanaingia katika mechi hiyo wakiwa katika hali nzuri kisaikolojia kutokana na mafanikio ambayo wameyapata katika miezi ya hivi karibuni kitaifa na kimataifa.

Mwezi uliopita walitwaa ubingwa wa Ngao ya Jamii kwa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania baada ya kuichapa Simba Queens kwa mabao 2-1 na kabla ya hapo ilitwaa ubingwa wa mashindano ya CECAFA ya kuwania kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kocha wa JKT Tanzania, Kessy Juma amesema kuwa wachezaji wake wapo sawa kisaikolojia kupeperusha bendera ya nchi leo.

“Mashindano haya ni zaidi ya ushindani wa kimichezo. Ni fursa ya kuonyesha namna soka la wanawake kwa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati limepiga hatua na kuendelea kujifunza.

“Maandalizi ni msingi wa kutimiza malengo yetu ambayo ni kupata ushindi. Tunajua ugumu wa mashindano na ubora wa timu pinzani lakini tuko tayari kushindana,” alisema Kessy.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *