KAMA ulidhani Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limemtupa aliyekuwa kocha wa Taifa Stars, Hemed Suleiman ‘Morocco’, basi unakosea kwani ameandaliwa mpango mzito.

Taarifa kutoka TFF zinasema, licha ya Morocco kutolewa katika nafasi hiyo ya kuinoa Stars, shirikisho hilo litampeleka nje ya nchi kuongeza ujuzi zaidi.

Kiongozi mmoja wa TFF aliliambia gazeti hili kuwa, sio Morocco peke yake, wapo makocha wengine ambao watapata fursa hiyo ya kwenda kujiendeleza zaidi kisha kuja kupewa timu za taifa hapo baadaye.

Ikumbukwe tu, TFF wiki iliyopita ilimuondoa Morocco kuifundisha Stars kwa makubaliano ya pande mbili na kumpa nafasi kocha wa Singida Black Stars, Miguel Gamondi kwa muda ili aiongoze timu hiyo itakayoshiriki Fainali za Mataifa Afrika (AFCON) zikazofanyika kuanzia Desemba mwaka huu huko Morocco.

MORO 02

“Msione kama Morocco ametupwa, hapana…bado tunakwenda kumuendeleza zaidi, tutamtafutia kozi za kwenda kusoma Ulaya, ili baadaye arudi kwenye majukumu haya haya.

“Morocco atakuwa wa kwanza tu, lakini huu ni mpango endelevu, kuna wenzake wengine watafuata au kuungana naye huko, mchakato huo umeshaanza na unafanyiwa kazi na idara ya ufundi ya TFF,” kilisema chanzo.

Morocco ambaye ana leseni ya ukocha inayomfanya kuiongoza timu yoyote ya klabu na taifa katika mashindano ya kimataifa, ujuzi anaokwenda kuongeza ni wa kiufundi.

Akizungumzia mipango hiyo, Rais wa TFF, Wallace Karia wakati akizungumza na televisheni ya shirikisho hilo, amesema katika mambo ambayo yatakuwa kwenye mpango wake ni kuwaongezea ujuzi makocha wazawa.

MORO 01

“Katika mpango ambao ninao kwenye uongozi wangu sasa ni kuhakikisha makocha wazawa wanaongezewa ujuzi ili kufundisha timu zetu za Taifa,” amesema Karia.

Morocco aliyeinoa Stars kama kaimu kocha mkuu kwa muda kwa mwaka mmoja na miezi 10 tangu Januari, 2024 na ndiye aliyeiwezesha timu hiyo kutinga fainali hizo za Afcon 2025 pia kucheza fainali za CHAN 2024 na kufika robo fainali ikiwa ni rekodi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *