BEKI wa kati wa Simba, Wilson Nangu, amesema licha ya kupewa heshima na wengi wanaoiona kazi yake uwanjani, lakini haimfanyi abweteke badala yake anaona ana safari ndefu ya kupambana ili huduma yake iendelee kuifaa klabu hiyo.
Beki wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Amir Maftah amesema kuna kitu anakitengeneza meneja mkuu wa klabu hiyo, Dimitar Pantev akisaidiana na Selemani Matola akibainisha pacha ya Nangu na Rushine De Reuck itakuja kuwa tishio kwa timu pinzani kadri muda unavyokwenda.
“Niliwahi kusema mapema Nangu ni tunu ya Simba kwa baadaye, bado anahitaji muda zaidi, anapewa nafasi anaonyesha kiwango kizuri, jambo la msingi anapaswa kujua kitu ambacho makocha wanakitaka kwake, mfano hiyo pacha wanayojaribu kuitengeneza baina yake na Rushine, maana ni kama Matola na Pantev wanaonyesha wanaiandaa timu ya kushambulia pembeni na kati,” amesema.
Kiungo wa zamani wa Yanga, Pato Ngonyani na sasa anamiliki kituo cha soka cha kukuza vipaji vya vijana kinachojulikana kama Hanga Sports Academy, amesema: “Nangu ni beki mzuri na siyo tu ataisaidia Simba, bali pia timu ya taifa, kikubwa aendelee kupambana na kukilinda kiwango chake na azingatie lengo la kocha kwake ni kitu gani.”
MSIKIE MWENYEWE
Nangu amesema bado ana safari ndefu ya kuendelea kupambana na kila nafasi anayopewa na makocha anatamani iache alama ya kuaminiwa zaidi katika mechi zilizopo mbele yao.
“Kila ninapopata nafasi ya kuwepo uwanjani, kwangu ina tafsiri kitu kikubwa cha kuhakikisha nafanya kazi ambayo makocha watazidi kuniamini na kunipa muda zaidi wa kucheza, Simba ina wachezaji wazuri na wenye ushindani wa juu, unaonisaidia nijitume kwa bidii,” amesena Nangu na kuongeza;
“Kuhusu kuifunga timu niliyokuwa naichezea kabla ya kuja Simba, wakati najiandaa na mechi nilitambua JKT Tanzania ina wachezaji wazuri ila nahitaji kupambania nilipoajiriwa kitu kilichonisaidia kutokuwa na presha.”
Msimu wa 2024-2025 akiwa JKT Tanzania, Nangu alifunga mabao mawili na asisti mbili, huku 2025-2026 ndani ya Simba amefunga bao moja la CAF dhidi ya Nsingizini, Wanamsimbazi wakiibuka na ushindi wa mabao 3-0 ugenini na bao la Ligi Kuu kaifunga JKT Tanzania.