KUNA kitu kimefanywa na Yanga kinachoweza kuwa mlima mgumu kwa timu nyingine, iwapo hazitaamua kukomaa ili kuifikia na hata kuivunja.

Achana na ile rekodi tamu ya kucheza mechi 49 mfululizo bila kupoteza iliyowekwa enzi ikiwa na Kocha Nasreddine Nabi, Yanga imeweka rekodi nyingi ya kucheza mechi kwa mwaka mmoja bila kuonja machungu ya kufungwa katika Ligi Kuu.

Ndiyo, juzi Yanga ilipata ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya KMC kwenye Uwanja wa KMC Complex,  Dar es Salaam na kuiweka timu hiyo kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo ikifikisha pointi 10 baada ya mechi nne, ikifunga mabao tisa na kufungwa moja.

YANG 02

Mabao ya mechi hiyo yalifungwa na Maxi Nzengeli na Pacome Zouzoua ambao kila mmoja alifunga moja huku mengine mawili yakitupiwa na Andy Boyeli, huku la KMC likifungwa na Daruweshi Saliboko.

Kama umesahau, ni mara ya mwisho kwa Yanga kupoteza katika Ligi Kuu ilikuwa ni Novemba 7 mwaka jana walipofumuliwa mabao 3-1 na Tabora United (sasa TRA United) na hadi sasa ukihesabu imetimia mwaka mmoja kwani ni siku 369.

Yanga ilikumbana na kipigo hicho kwenye Uwanja wa Azam Complex, kilichokuwa cha pili kwa timu hiyo baada ya awali kufungwa na Azam FC kwa bao 1-0 baada ya kucheza mechi nane mfululizo chini ya Miguel Gamondi tena bila kuruhusu bao lolote.

YANG 03

Mara baada ya mechi hiyo ya Nyuki wa Tabora, Gamondi alifungishiwa virago na kuletwa Saed Ramovic, kisha Miloud Hamdi kisha Roman Folz na sasa Pedro Goncalves, Yanga imekomaa na kutengeneza mtego ambao unaweza kuwatesa wapinzani wa timu hiyo katika ligi.

Katika kipindi hicho cha mwaka mmoja na siku tatu ambacho Yanga imefikisha bila kupoteza mechi ya Ligi Kuu, imeingia uwanjani katika mechi 24 za Ligi Kuu, ikipata ushindi mara 22 na imetoka sare katika michezo miwili tu ikiwamo dhidi ya JKT Tanzania msimu uliopita na Mbeya City kwa msimu huu.

Ushindi katika mechi 22 na sare mbili katika kipindi cha mwaka mmoja tangu ilipopoteza dhidi ya Tabora United ambayo sasa inaitwa TRA United, mabingwa hao watetezi wa taji la Ligi Kuu wamkusanya idadi ya pointi 68 ambapo 66 zimetokana na ushindi na mbili kwa sare.

YANG 04

Makali ya safau ya ushambuliaji yameonekana kuchangia kwa kiasi kikubwa Yanga kutamba Ligi Kuu Bara katika kipindi cha miezi 12 mfululizo kwani imefunga mabao 77 ikiwa ni wastani wa mabao 3.2 kwa mechi.

Haijaishia katika safu ya ushambuliaji tu kwani Yanga imekuwa bora katika safu ya beki na kipindi hicho imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara sita tu ikiwa ni wastani wa bao 0.3.

KMC imeonekana kuchangia idadi kubwa ya mabao ya Yanga ndani ya kipindi hicho kwani yenyewe pekee imefungwa mabao 10 na kuzitema pointi tisa, kama ilivyo kwa Pamba Jiji zikiwamo sita za msimu uliopita na tatu za juzi, huku Simba, Pamba Jiji zikiwa ni kati ya timu zilizoipa pointi sita kila moja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *