Mchezaji wa JKT Queens, Elizabeth Chenge amesema msimu huu amepanga kufanya vizuri ili kujihakikishia nafasi ya kucheza kwenye kikosi hicho kilichojaa nyota wakali.

Chenge alisajiliwa msimu uliopita akitokea Alliance Girls ya Mwanza ambako alilelewa tangu anaanza soka 2021.

Akizungumza na Mwanaspoti Chenge amesema msimu uliopita ulikuwa wa kujifunza na kupata uzoefu kwenye timu kubwa kama JKT ambayo imejaa wachezaji wenye ushindani mkubwa.

Aliongeza kuwa msimu huu amejipanga kitofauti na anataka kuonyesha uwezo wake ili kuwa sehemu ya wachezaji watakaokuwa na mchango mkubwa kwa timu hiyo.

“Msimu uliopita nilikuwa najifunza mambo mengi jinsi ya kucheza chini ya presha, nidhamu ya kikosi na mbinu za walimu. Sasa najiona niko tayari natamani kucheza mechi nyingi na kusaidia timu kupata matokeo,” amesema Chenge.

Nyota huyo mwenye kipaji cha kucheza nafasi zote za kiungo, amesema anatambua ushindani ndani ya kikosi cha JKT Queens ni mkubwa lakini amejipanga kupambana kwa bidii kwenye mazoezi.

“Wachezaji wengi ni wana uzoefu mkubwa, wameshacheza timu ya taifa na mashindano makubwa, na nimekuwa nikijifunza vitu vingi kutoka kwao kabla sijajiunga hapa,” amesema mchezaji huyo.

Chenge amesema ndoto yake ni kuona anafika mbali kisoka na kuichezea Timu ya Taifa ya Wanawake, Twiga Stars kwa mafanikio huku akisisitiza kuwa JKT ni sehemu bora ya kukuza vipaji kwa wachezaji chipukizi kama yeye.

“Ninataka kufanya vizuri hapa JKT kwanza, halafu nitafute nafasi Twiga Stars ingawa nimeshacheza mashindano kama WAFCON, Naamini kwa kazi na nidhamu yote yanawezekana.”

Tangu kocha Ester Chabruma hadi Abdallah Kessy wote wamekuwa wakimpa nafasi ya kuanza kinda huyo na msimu uliopita alicheza mechi zote za Ligi Kuu na mashindano mengine.

Chenge alisajiliwa wakati ambao Joyce Lema aliyekuwa anacheza nafasi hiyo alipoumia na alikaa nje ya uwanja kwa takriban msimu mzima akiuguza jeraha la goti.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *