
KOCHA wa 15 de Agosto ya Guinea ya Ikweta, Sinforosa Eyang Nchama amesema anatamani kuandika historia ya kubeba ubingwa akiwa na kikosi hicho kinachoshiriki kwa mara ya kwanza kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake.
Mwanamama huyo alikuwa mmoja wa nyota waliocheza mashindano ya Kombe la Dunia 2011 nchini Ujerumani akiwakilisha taifa la Guinea ya Ikweta katika hatua ya makundi dhidi ya timu kama Brazil, Norway na Australia.
Alicheza pia Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON), ambapo Guinea ya Ikweta ilifanikiwa kutwaa ubingwa mara mbili miaka ya 2008 na 2012.
Nchama amesema timu mbili kutoka ukanda huo Malabo Kings na Hurricanes zimecheza mashindano hayo na upande wao wamejipanga kuhakikisha wanaendeleza rekodi nyingine.
Ni heshima kubwa sana kwetu kufuzu si mafanikio ya 15 de Agosto pekee, bali ni hatua kubwa kwa maendeleo ya soka la wanawake nchini Guinea ya Ikweta.Kuwa klabu ya tatu kutoka kwetu kufika hatua hii, baada ya Malabo Kings na Hurricanes ni ishara tosha ya maendeleo na sisi tunatamani kuweka rekodi zaidi ili soka letu lifike mbali,” anasema kocha huyo na kuongeza:
“Hii ni mara yetu ya kwanza lakini sio kinyonge na tumekuja kuonyesha kuwa Guinea ya Ikweta ni miongoni mwa nchi zenye vipaji na zinazoanza kukua kisoka.”
Hii ni mara ya tatu kwa nchi za Afrika ya Kati kuingiza timu tatu tofauti tangu michuano hiyo iaznsihwe mwaka 2021. Malabo Kings walifika nusu fainali mwaka 2021, Hurricanes wakashiriki kwa mara ya kwanza mwaka 2023 na sasa 15 de Agosto.