KIUNGO wa Simba, Neo Maema amefichua jambo kwa kusema alizipotezea ofa za Kaizer Chiefs na Orlando Pirates za nyumbani kwao Afrika Kusini ili kuungana na aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Fadlu Davids kwa mkopo wa mwaka mmoja.

Fundi huyo ambaye ametua Simba msimu huu akitokea Mamelodi Sundowns, amefichua kwanini aliamua kucheza soka la kulipwa nje ya Afrika Kusini na wala hajutii uamuzi huo licha ya Fadlu kutokuwa sehemu ya kikosi hicho siku chache baada ya msimu kuanza.

Ikumbukwe kuwa kocha huyo raia mwenzake wa Afrika Kusini, alitimkia Morocco baada ya kupata ofa ya kurejea Raja Casablanca, ikiwa ni baada ya kuiongoza Simba kucheza mechi mbili, Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga na kupoteza, kisha hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Gaborone aliposhinda 1-0 ugenini.

MAE 01

“Nilifanya uamuzi wa kuondoka Afrika Kusini kwa ajili ya afya ya akili yangu. Nilihitaji sehemu mpya ambayo ni nje ya nchi ili kukumbana na changamoto mpya za soka. Nilielezwa kwamba kulikuwa na ofa kadhaa lakini tulikaa na baba yangu, nikawa-ambia siamini kama kuhama mtaa mmoja ingekuwa na tija,” alisema.

Akasema kile alichokitaka ni mazingira mapya kabisa ambayo yangemtoa katika mzunguko ule ule wa kushindwa kupata nafasi ya kutosha.

MAE 02

“Miaka miwili kwangu haikuwa na muendelezo wa kucheza mara kwa mara. Nikasema kama kutakuwa na ofa kutoka nje ya nchi, basi hiyo ndiyo nitakayochukua. Simba walipokuja, nilihisi ndio muda wangu,” alisema mchezaji huyo.

Kuhamia Tanzania kwa nyota huyo lilikuwa jambo ambalo alikuwa akilifikiria kwa muda mrefu. Aliamini kucheza angalau msimu mmoja au miwili nje ya Afrika Kusini kunaweza kuongeza kitu kwenye soka lake.

MAE 03

Tangu ajiunge na Simba, licha ya mabadiliko ya benchi la ufundi, Maema amekuwa akipata nafasi, akicheza mechi mbili kati ya nne za mchujo katika Ligi ya Mabingwa Afrika. Na sasa, akiwa na timu hiyo, wameshatinga hatua ya makundi na kupangwa Kundi D sambamba na Esperance ya Tunisia, Stade Malien ya Mali na Petro de Luanda ya Angola.

Kwa upande wa Ligi Kuu Bara, amecheza mechi zote huku ya mwisho dhidi ya JKT Tanzania ambayo Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 akicheza kwa dakika 60, mechi ya kwanza dhidi ya Fountain Gate alicheza kwa dakika 26, ya pili dhidi ya Namungo akicheza kwa dakika 45.  Katika mechi hizo, ametoa asisti moja kwenye mechi dhidi ya Namungo ambapo aliingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Elie Mpanzu na kuisaidia Simba kuibuka na ushindi wa mabao 3-0.

Novemba 23, 2025, Simba itakuwa na mechi ya kwanza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Petro de Luanda ya Angola kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es Salaam.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *