Washington imeyaweka kwenye orodha ya “ugaidi wa kimataifa” makundi manne ya mrengo wa kushoto yenye misimimamo mikali ya barani Ulaya.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imetangaza kwamba itayaarifisha makundi manne ya Ulaya yanayojiita ya kupinga ufashisti kama Mashirika ya Kigeni ya Kigaidi. Marco Rubio, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani amesema katika taarifa yake kwamba kundi la “Antifa Ost” lenye makao yake Ujerumani pamoja na makundi mengine matatu ya huko Ugiriki na Italia yamearifishwa kama kama “Magaidi Maalumu wa Kimataifa”; hatua aliyoitaja kuwa inakwenda sambamba na dhamira ya Trump ya kukabiliana na kampeni za ukatili wa kisaisa za Antifa. 

Antifa Ost ni vuguvugu la siasa za mrengo wa kushoto dhidi ya ufashisti na ubaguzi wa rangi.

Trump na washirika wake wa chama cha Republican wamezidi kulituhumu kundi hilo la Antifa kuwa linachochea ghasia za kisiasa tangu kuuawa kwa Charlie Kirk mwezi Septemba. Septemba 22 mwaka huu Trump aliliweka rasmi Vuguvugu la Antifa kwenye orodha ya makundi ya kigaidi ya ndani baada ya kutoa dikrii ya kiutendaji iliyoitambua Antifa kama taasisi ya kigaidi ya ndani. Hii ni katika hali ambayo wachambuzi wengi wa mambo nchini Marekani wamesisitiza kuwa tamko hilo halina msingi madhubuti wa kisheria, kwa sababu sheria za sasa za Marekani kimsingi hazijaainisha utaratibu wa wazi wa kuyataja makundi ya ndani kama taasisi za kigaidi.

Pamoja na hayo, katika miezi ya karibuni Rais wa Marekani amejaribu kuonyesha kuwa Antifa si vuguvu la upinzani bali ni adui aliyejipanga, na amebadili anga ya kisiasa ya Marekani kwa maslahi yake. Hivi sasa pia kuwekwa makundi kadhaa ya Ulaya kwenye orodha ya ugaidi ya Marekani, zaidi ya kuwa matokeo ya tathmini ya taasisi za usalama, ni sehemu ya mradi wa kisiasa wa Trump wa kukuza tishio la Antifa na kuimarisha riwaya yake kuhusu kile anachokiita ukatili wa mrengo wa kushoto wenye siasa kali. Ni wazi kuwa, uamuzi huu unaoambatana na kulipa jina “Antifa yenye kupenda ghasia,” ni wenzo wa mashinikizo ya kisiasa na sio tathmini sahihi na za kiufundi za usalama.

Wafuasi wa Vuguvugu la Antifa barani Ulaya 

Trump ameitaja Antifa kuwa vuguvugu la ugaidi  kwa malengo kadhaa: Mosi, ni kuwa anataka kudhihirisha kuwa Marekani iko chini ya mashinikizo ya mrengo wa kushoto wenye misimamo mikali ili kuwavutia zaidi wafuasi wake. Pili ni kuwa, anataka kupotosha fikra za waliowengi nchini Marekani kuhusu hatari halisi ya mrengo wa kulia na kuwaelekeza kwa kile anachodai ni vurugu na ukatili wa mrengo wa kushoto. Tatu ni kuwa, amechukua hatua hiyo ili aweze kukandamiza maandamano ya kupinga ubaguzi wa rangi na mikusanyiko muhimu na kuyaarifisha kama harakati zinazoungwa mkono na “magaidi wa Antifa.”

Hakuna shaka kuwa serikali ya Trump miaka iliyopita ilifanya kila iwezalo kukuza maana halisi ya “tishio” kwa kiwango cha kimataifa hata kama hatua hiyo inatatiza uhusiano wa Marekani na waitifaki wake na kuwasababishia gharama za kisiasa. 

Hatua hii pia inaonyesha kuwa utawala wa Trump uko tayari kulazimisha ajenda yake ya ndani kwa sera ya kigeni ya Marekani bila kujali hisia za kisiasa au kiusalama za washirika wake. Lebo ya “ugaidi wa kimataifa” inayotumika kwa makundi ambayo shughuli zake ni za ndani ya Marekani ni kielelezo cha utashi huu wa kisiasa.

Kuarifishwa makundi ya Antifa huko Ujerumani, Italia, na Ugiriki kama taasisi za kigaidi, kwa hakika ni mwendelezo wa mkakati wa ndani wa Trump; mkakati ambao umejikita katika kukabiliana na vuguvugu la mrengo wa kushoto ambao sasa umevuka mipaka ya kijiografia ya Marekani. Ni wazi kuwa Trump amekusudia kubadilisha neno “Antifa” kuwa dhana sawa na “tishio la kimataifa” mbele ya maoni na fikra za walimwengu bila kutoa ushahidi wa kutosha.

Nukta muhimu ni kuwa, wataalamu wengi wa masuala ya sheria wanaamini kuwa uamuzi huu unatiliwa shaka kisheria. Antifa haina taasisi rasmi, na kuyataja makundi yenye muundo kama huu katika kalibu ya  “ugaidi wa kigeni” kunakabiliwa na pingamizi za kisheria. Katika upande mwingine, vyombo vya habari vya Ulaya pia vimeitaja hatua hiyo kuwa ni katika fremu ya sera binafsi za Trump. 

Matokeo ya sera kama hiyo sio kuimarisha usalama, bali ni kuzidisha hali ya kutoaminiana, hasa ikizingatiwa kuwa   hatua za aina hii zitaufanya ushirikiano wa siku zijazo kati ya Marekani na Ulaya kuwa mgumu zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *