Kushuka kwa ufadhili wa miradi ya kibinaadamu duniani kumeifanya WFP kutoa kipaumbele wa msaada wa chakula kwa takriban theluthi moja ya wale wanaohitaji, ikilenga watu milioni 110 walio katika hatari kubwa ya kukumbwa na baa la njaa.

Hiyo inamaanisha shirika hilo litahitaji dola bilioni 13 kutimiza wajibu wake huo lakini likaonya kuwa ufadhili unaoonekana kwa sasa huenda ukalikosesha hata nusu ya fedha hizo zinazohitajika. 

Mfadhili mkubwa wa shirika hilo ni Marekani ambayo chini ya Rais Donald Trump, imepunguza msaada wa nje, ikiwa ni pamoja na taasisi za Umoja wa Mataifa. Mwengine anayechangia fedha katika mfuko wa msaada wa WFP ni Mataifa ya Ulaya ambayo pia yamepunguza bajeti zao kuelekea msaada wa nje wa kibinaadamu. 

WFP imesema watu milioni 318 wanaokumbwa na njaa kali ni zaidi ya mara mbili ya idadi iliyoripotiwa mwaka 2019, huku migogoro, mabadiliko ya tabia nchi na uchumi unaoyumba ikichangia hli kuwa mbaya zaidi. 

Gaza na Sudan ni baadhi ya maeneo yanayokabiliwa na njaa kubwa

Mashirika ya Umoja wa Mataifa mwaka huu yalitangaza njaa katika Ukanda wa Gaza na maeneo tofauti ya Sudan, jambo ambalo mkurugenzi mtendaji wa WFP Cindy McCain alilitaja kuwa halikubaliki hasa katika karne hii ya 21. 

Tizama namna Wapalestina wanavyopambania mkate

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Cindy McCain amesisitiza kuwa majibu ya dunia katika masuala ya ufadhili bado ni mdogo na uliogawika. Amesema kwa sasa wamepunguza misaada katika miradi yao yote na wameamua kuwahudumia wale walio na mahitaji makubwa.

Haiti, Mali, Palestina, Sudan Kusini, Sudan na Yemen ni miongoni mwa nchi zilizo katika hali mbaya zaidi. Miongoni mwa nchi zilizowekwa kwenye orodha ya “kutia wasiwasi mkubwa” ni Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Somalia, Nigeria, Chad, Burkina Faso, Afghanistan, Syria na Myanmar. 

Wiki iliyopita WFP na Shirika la Chakula na Kilimo, FAO yalionya kuwa mamilioni ya watu kote duniani huenda wakakumbwa na njaa. kufuatia hali hiyo ya kukatwa kwa ufadhili, kunakoifanya hali ambayo tayari ni mbaya, kuwa mbaya zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *