Dar es Salaam. Mkali wa Hip-Hop nchini Frida Amani ameteuliwa kuwa Balozi wa Mazingira Duniani kupitia Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP) kwa kupewa wadhifa wa “Advocate for Ecosystem Restoration”.
Kwa mujibu wa shirika hilo jukumu kubwa la msanii huyo ni kutumia sanaa, utamaduni na sauti yake yenye ushawishi kuhamasisha vijana wa kizazi kipya na wananchi kuchukua hatua za kuzuia uharibifu wa mazingira sambamba na kulinda asili ya mazingira yetu barani Afrika na duniani kote.
Hii inakuwa mara ya kwanza kwa Shirika la Mazingira duniani (UNEP) kumtangaza msanii kutoka Tanzania au Afrika Mashariki kwa wadhifa huu. Uteuzi huu unasisitiza umuhimu wa vijana, ubunifu na ushiriki wa jamii kwenye mazingira.
Kwa kutangazwa huku na Umoja wa Mataifa, Frida ambaye ameshiriki na kuendesha kampeni na miradi mbalimbali yenye kutangaza na kuhamasisha uhifadhi na utunzaji wa mazingira akiungana na Mabalozi wengine wa Shirika hilo Duniani kama Jason Momoa, Don cheadle, Dia mirza, Rocky dawuni na Antoinette Taus.
Aidha kwa upande wa Frida ameweka wazi kuwa kupitia sauti yake na ubunifu wake ataelimisha na kuhamasisha jamii kutunza mazingira kwa hapa Afrika na nje ya Afrika.
“Ninayo furaha kubwa kupata heshima hii, na ninakubali rasmi uteuzi huu kama Balozi wa kwanza wa UNEP katika kusimamia urejeshwaji wa Mifumo ya Ikolojia. Heshima hii ni kubwa kuliko ninavyoweza kueleza. Mazingira yamekuwa msingi wa ustawi wetu na kuyaona yakidhoofika kumezidi kuniaminisha kuwa kila mmoja wetu, mimi nikiwemo, tuna jukumu la kurejesha tunachopoteza.
“Ninaishukuru UNEP kwa kuniamini na kunipa nafasi hii muhimu kwa kutambua nguvu ya sanaa, utamaduni na vijana katika kuleta mabadiliko ya kimazingira. Kupitia nafasi hii najitoa kutumia sauti yangu, jukwaa langu na ubunifu wangu kuelimisha jamii, kuhamasisha utunzaji wa mazingira, na kuhamasisha hatua ndani ya Afrika na zaid,”ameeleza Frida
Aidha ameongezea kwa kueleza “Nitaendelea kuwaunga mkono wanawake, kuinua vijana na kuhamasisha utunzaji wa mazingira katika kila kazi ninayofanya kuanzia muziki hadi miradi ya jamii. Huu si tu utambulisho ni mwito wa kutumikia. Pamoja, tutarejesha mifumo ya ikolojia, kulinda mustakabali wetu, na kujenga kizazi kinachoelewa kuwa kuirudisha asili katika uhai si hiari ni wajibu,” ameeleza