India. Zaidi ya miaka 30, muziki wa Bollywood umejengwa juu ya muunganiko wa sauti na video zenye hisia baina ya wanamuziki na waigizaji.
Lakini katika historia ya filamu za India, wachache waliwahi kutengeneza muunganiko wenye nguvu kama ule wa muigizaji wa Bollywood, Shah Rukh Khan na mwimbaji mkongwe Udit Narayan.
Kwa takribani miaka 30 sauti ya Udit ndio imekuwa ikitumika kwenye tamthilia mbalimbali za India na kupata umaarufu mkubwa, lakini wengi hawamfahamu kwa vile hakutokea kwenye video ya ngoma zake.
Badala yake alitumiwa Shah Rukh Khan kwa kule India wanamwita mchawi wa kideoni yaani kila inapokuwa kamera mbele yake basi tarajia jambo kubwa kutoka kwa mfalme huyo wa Bollywood akiigiza kwa hisia.
Lakini huo ni kama utaratibu wa India, yaani waimbaji (playback singer) wanarekodi nyimbo na baadaye kampuni za kusambaza muziki India kama Set India, Sony Music na nyinginezo zinatafuta waigizaji wenye mionekano na ushawishi mkubwa kuigiza humo ili ngoma hizo zipate watazamaji wengi.
Na hapo ndipo sauti ya Udit na SRK zilipoungana, ni ushirikiano uliobadilisha si tu sura ya filamu za mapenzi India, bali pia safari ya mafanikio ya SRK katika tasnia yake.
Yaani kiufupi ni kama umaarufu na utajiri wa SRK umechangia kwa kiasi kikubwa na uwepo wa sauti ya Udit na kufanya baadhi ya mashabiki waamini ngoma hizo ziliimbwa na Shah.
PACHA YAO ILIPOANZA
Wakati Shah Rukh Khan anaingia kwenye tamthilia za Bollywood mwanzoni mwa miaka ya 1990, filamu za India zilikuwa zikitawaliwa na majina makubwa kama Aamir Khan na Salman Khan.
Hivyo, SRK alihitaji kuonyesha kitu cha tofauti na kitambulisho cha kipekee sauti ambayo ingeendana na sura yake, mwili wake, hisia zake na nguvu ya uigizaji wake na hapo ndipo Udit akaingia.
Udit alianza kuimba mwaka 1980 akiwa na sauti ya kipekee, nyororo, yenye hisia na mwangaza wa kimapenzi. Sauti hiyo ilimfungulia Shah Rukh Khan (SRK) mlango wa kutambulika kama mfalme mpya wa filamu za mahaba.
NGOMA ZA UDIT, SRK AKIIGIZA
1. Dilwale Dulhania Le Jayenge (1995)
Hii ni filamu ya kwanza iliyoanza kumpa umaarufu Shah Rukh Khan, Udit alitoa sauti laini yenye mapenzi mazito, iliyoendana kikamilifu na uigizaji wake hususan tabasamu lake na mwendo wake wa polepole unaotambulika hadi leo.
Hapa ndipo uchawi wa Udit Narayan na Shah Rukh Khan ulipoanza. Nyimbo kama ‘Tujhe Dekha To’ na ‘Ruk Ja O Dil Deewane’ zilianza kumjenga kama nembo ya mwanaume wa ndoto za wanawake.
Kuanzia filamu yenyewe hadi ilipotolewa nyimbo rasmi Shah Rukh Khan aliigiza na Kajol na Amrish Puri ukafanya ngoma hiyo ipendwe zaidi kutokana na uhusika wa watatu hao.
2. Dil To Pagal Hai (1997)
Hii ni ilikuwa filamu ya pili iliyowakutanisha tena wakali hao wawili ikafanya baadhi ya mashabiki waamini SRK aliimba na kuigiza kwenye filamu hiyo baada ya kuigiza kwa hisia kubwa.
Katika filamu hiyo, zilitengenezwa nyimbo kama ‘Bholi Si Surat’ na ‘Dil To Pagal Hai’ zilizoonyesha upande mwingine na mguso wa SRK kama mhusika anayeteseka kwenye mapenzi.
Sauti ya Udit iliifanya tabia ya Shah Rukh Khan kuwa ya kuvutia zaidi, ikimjengea umaarufu miongoni mwa watazamaji wa rika zote si vijana wala wazee.
3. Mohabbatein (2000)
Hii ni filamu nyingine ambayo Shah Rukh Khan aliendelea kupewa nafasi chini ya muongozaji Aditya Chopra.
Katika filamu hiyo SRK aliigiza na mkongwe Amitabh Bachchan pamoja na mwanadada Aishwarya Rai, Uday Chopra, Jugal Hansraj, Jimmy Shergill, Shamita Shetty, Kim Sharma na Preeti Jhangiani.
Baada ya filamu hiyo kufanya vizuri na kipande cha Udit alichoimba na mwanamama Lata Mangeshkar kuwavutia mashabiki wengi ukatolewa tena wimbo kama wimbo.
Video ya ngoma hiyo ilitoka Oktoba 28, 2014 na SRK akapata shavu tena la kuigiza ngoma hiyo akiwa na Aishwarya na kuigiza kwa hisia kana kwamba aliimba yeye na kilichowachanganya zaidi mashabiki kuona sauti ile ile ya Udit ikijirudia katika wimbo wa tatu.
Ni kati ya nyimbo zilizofanya vizuri na hadi sasa ikiwa na zaidi ya miaka 10 imetazamwa zaidi ya mara milioni 433 kupitia kampuni ya usambazaji wa muziki wa YRF.
Ngoma iliitwa ‘Humko Humise Chura Lo’ na SRK aliigiza kama mwanaume mwenye historia ya kupigwa matukio kwenye mapenzi, ngoma iliimbwa kwa hisia kiasi cha baadhi ya mashabiki kuamini SRK alikuwa anapitia kipindi cha maumivu.
4.Kuch Kuch Hota Hai (1998)
Ulimwengu ulimfahamu Shah Rukh Khan kupitia filamu ya Kuch Kuch Hota Hai iliyotoka mwaka 1998 na hadi leo ukiitaja mafanikio ya sanaa ya India basi hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa.
Kama kawaida Shah Rukh Khan alipewa scene na muongozaji maarufu wa India, Karan Johar wakati huo akiwa wa moto kweli kweli kama ilivyo kwa staa wa Bollywood.
Filamu hiyo ilipata umaarufu mkubwa kwanza kutokana na wahusika waliocheza humo, SRK na Kajol waliokuwa na pacha nzuri kideoni wakishirikiana na Rani Mukerji.
Baada ya mafanikio makubwa ukatolewa wimbo, Udit akishirikiana na mkongwe mwanamama Alka Yagnik humo Shah Rukh Khan aliyekuwa mwanaume pekee aliyeigiza na marafiki wawili wa kike Kajol na Rani alionyesha uchawi kwa mara nyingine tena.
Kampuni ya Sony Music ikaiboresha video ya ngoma hiyo mwaka 2009 ikapata watazamaji zaidi ya milioni 41, kutokana na maendeleo ya kidijitali mwaka 2023 ikaboreshwa tena ili kuvutia zaidi watazamaji.
Ikang’arishwa tena na kuonekana kama imeigizwa kipindi hiki ilhali tayari SRK na waigizaji wengine wameshaongezeka umri na ikapata watazamaji zaidi ya milioni 215
Filamu nyingine ni Ladki Badi Anjaani Hai, Tujhe Yaad Na Meri Aayee, Saajanji Ghar Aaye, Hey Uncle na nyinginezo zaidi ya 20 zilizowakutanisha wawili hao.
UDIT MWENYEWE
Udit Narayan alizaliwa Desemba 1, 1955 nchini Nepal. Lakini alipata umaarufu India akiwa kama mmoja wa waimbaji wa nyuma ya filamu (playback singers) ambao wanatamba katika historia ya Bollywood.
Alianza kuimba mwaka 1980, lakini alipata mafanikio makubwa mwaka 1988 kupitia filamu ya ‘Qayamat Se Qayamat Tak’. Katika filamu hiyo, aliimba wimbo wa ‘Papa Kehte Hain’, ambao ulimtambulisha rasmi kama mmoja wa waimbaji bora wa kizazi hicho.
Mbali na muziki, mchango wake katika filamu za India ni mkubwa kwani kupitia sauti yake amefanikisha kusukuma filamu hasa zile za mapenzi na kuzifanya zitambulike zaidi ikiwamo Kuch Kuch Hota Hai, Dilwale Dulhania Le Jayenge, Raja Hindustani, Lagaan nk.
Kupitia kipaji chake amefanikiwa kunyakuwa tuzo za heshima ikiwa ni pamoja na ‘National Film Awards’ mara tatu na ‘Padma Bhushan’, ambayo ni moja ya tuzo za juu zaidi nchini India.
Sauti ya Udit imewahi kutumika na mastaa zaidi ya 100 katika filamu zao ikiwa ni pamoja na Aamir Khan ‘Qayamat Se Qayamat Tak (1988)’, Shah Rukh Khan ‘Dilwale Dulhania Le Jayenge’, Salman Khan ‘Hum Aapke Hain Koun’, Akshay Kumar ‘Dastak’, Govinda, Hrithik Roshan, Saif Ali Khan na wengineo.
Pia amefanya kolabo na wasanii wa kike akiwamo Lata Mangeshkar, Alka Yagnik, Kavita Krishnamurthy, Sadhana Sargam, Anuradha Paudwal na kadhalika.
Ili kuendeleza kipaji chake Udit alimwingiza mtoto wake wa kiume Aditya Narayan kwenye tasnia ya muziki unaotumika katika filamu akiwa na miaka 5. Aditya sauti yake ilisikika katika filamu ya Masoom (1996) kupitia wimbo wake wa ‘Chhota Baccha Samajh Ke’.
Aidha, dunia ilimtambua kijana huyo wakati alipokuwa na miaka 8 baada ya kuimba na baba yake katika wimbo wa ‘I Love You Daddy’ kupitia filamu ya ‘Akele Hum Akele Tum (1995)’, wimbo ambao ulisaidia filamu hiyo kutambulika zaidi duniani.
Mpaka kufikia sasa, Udit ameimba zaidi ya nyimbo 25,000 katika lugha 36 kama Hindi, Nepali, Bengali, Kannada, Tamil, Telugu, na nyinginezo, huku akifanikiwa kuachia album yake ambayo imejaa masongi yanayokubalika zaidi.
Mbali na sauti yake ambayo imekuwa ikiwavutia zaidi mashabiki mbalimbali pia ameonekana katika filamu kama Kanoon (1994), Kusume Rumal 2 (2009) na Megha (1996).