Dar es Salaam. Kama ambavyo umekuwa ni utamaduni wa wanamuziki wengi kuondoka ndani ya lebo zilizowapa majina makubwa katika tasnia, ndivyo hivyo imekuwa ni rahisi kubaini kitakachofuata baada ya hapo.
Ndani ya Bongofleva inaonekana wengi baada ya kusepa katika lebo wanakimbilia kutoa Extended Playlist (EP) kwa lengo la kuonyesha uwezo wao ulivyo nje ya lebo na hata kusaka mashabiki wapya.
Ikumbukwe EP ni mfano wa albamu fupi ambayo mara nyingi inapendekezwa kuwa na nyimbo kuanzia nne hadi nane ambazo kwa ujumla huwa na urefu wa dakika kati ya 10 hadi 30 za kusikiliza.
Na kwa upande wa albamu yenyewe, hii hujumuisha nyimbo kuanzia nane na kuendelea ambazo kwa ujumla zinapendekezwa ziwe na urefu wa dakika kati ya 30 hadi 80 hivi.
Waimbaji kama Rayvanny, Angella, Mbosso, Lava Lava na Yammi, ni miongoni mwa wale waliotoa EP mara baada ya kuondoka katika rekodi lebo ambazo zilikuwa zinawasimamia kimuziki.
1. Rayvanny – Unplugged Session
Baada ya kufanya kazi pamoja kwa takribani miaka saba, mnamo Julai 2022, Rayvanny aliaga rasmi ndani ya WCB Wasafi akiwa tayari ameanzisha lebo yake, Next Level Music (NLM) ambayo ilimtoa Mac Voice.
Miezi minne baada ya kuaga WCB Wasafi, Rayvanny akatoa EP mpya, Unplugged Session (2022) yenye nyimbo nane ikiwa ni ya nne baada ya kuachia – Flowers (2020), New Chui (2021) na Flowers II (2022).
Unplugged (2022) ni EP yenye mtiririko wa muziki tulivu wa live na wa kihisia, ambapo Rayvanny anaimba kwa utulivu bila makeke mengi ya studio yanayoweza kuchangiwa na vifaa vya kisasa vya muziki.
Mradi huu wa kwanza chini ya NLM, unamlenga msikilizaji ambaye anapenda sauti (vocals) za moja kwa moja zenye hisia za kweli, na ujumbe uliojikita katika maisha, ukuaji binafsi, mapenzi, maumivu na utu.
2. Anjella – The Black Queen
Alikuwa ndiye mwimbaji pekee wa kike katika lebo ya Konde Music Worlwide, ambapo alianza kusikika katika ngoma ya Harmonize, All Night (2021), kisha zikafuata zake binafsi ambazo zilimtambulisha vizuri.
Baada ya kuachana na Konde Music hapo Novemba 2022, mwaka mmoja na nusu baadaye aliachia EP yake, The Black Queen (2024) yenye nyimbo saba.
The Black Queen (2024) yenye ladha ya Bongofleva na R&B, ni EP yake ya kwanza inayolenga kutoa shukrani na heshima kwa mashabiki wake waliomwamini na kumuunga mkono tangu siku ya kwanza.
Angella akiwa ameimba kwa sauti laini juu ya midundo mizuri, kupitia EP hii anazungumzia mapenzi, maumivu, kiu ya uhuru na kujithamini akiwa kama mwanamke msanii aliyeanza safari mpya kimuziki.
3. Mbosso – Room Number 3
Baada ya miezi mitano tangu alipoondoka WCB Wasafi, ndipo Mbosso akaachia EP yake ya pili, Room Number 3 (2025) yenye nyimbo saba, huku ukiwa mradi wa kwanza chini ya lebo yake, Khan Music.
Ikumbukwe EP yake ya kwanza akiwa bado WCB Wasafi, Khan (2022) ilifanya vizuri hadi kushinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) 2022 kama Msanii Bora wa Kiume wa Bongofleva.
Room Number 3 (2025) ni EP inayolenga kuonyesha safari ya muziki ya Mbosso na ukuaji wake, ikiwakilishwa vipindi vitatu tofauti – Yamoto Band, WCB Wasafi na Khan Music akiwa kama msanii anayejitegemea.
Ina mchanganyiko wa Bongofleva, R&B, Afrobeats na Amapiano, ambapo muziki wake unazungumzia maisha ya kawaida ukiakisi umbali aliotoka Mbosso akiwa na shauku na dhamira ya kweli ya kutimiza ndoto zake.
4. Lava Lava – Time
Kuanzia jina hadi umaarufu wa kimuziki, Lava Lava alivipata WCB Wasafi akiwa ni msanii wa tano kusainiwa hapo 2017 lakini mwaka huu yeye pamoja na lebo hiyo wakasema imetosha, kila mmoja ashike njia yake.
Takribani miezi saba tangu kuachana na WCB Wasafi, Lava Lava akaachia EP yake, Time (2025) yenye nyimbo sita, ikiwa ni ya pili baada hapo awali kutoa Promise (2025).
Time (2025) ni mradi wa kwanza chini ya lebo yake mpya, Bite Gang, EP hii inazungumzia mapenzi na starehe kwa sehemu kubwa ambapo kila wimbo una ladha na ujumbe wake wa kipekee.
Utolewaji wa EP hii unaashiria sura mpya katika safari ya muziki wa Lava Lava, na unaweka mwelekeo wa kile kinachotarajiwa chini ya Bite Gang, ikiwa kama lebo changa inayotaka kusimamisha himaya katika muziki.
5. Yammi – After All
Akiwa msanii wa kwanza kusainiwa na The Africa Princess, Yammi alifanya vizuri ila kufikia Machi 2025, lebo ilitangaza kusitisha mkataba kwa makubaliano ya pande zote ikiwa ni baada ya miaka miwili ya ushirikiano.
Yammi, mkali wa kibao cha Tiririka (2023), baada ya miezi mitano nje ya The Africa Princess, akaja na EP yake, After All (2025) yenye nyimbo sita, ikiwa ni ya pili baada ya awali kutoa, Three Hearts (2023).
After All EP (2025), inaonyesha ukuaji wa kisanii wa Yammi na uwezo wake wa kuungana na wasikilizaji kupitia mashairi ya kugusa moyo na midundo yenye roho.
Kila wimbo una simulizi yake ya pekee – kuanzia mapenzi na maumivu hadi furaha na sherehe, hivyo kuifanya EP hii kuwa yenye utofauti kwa sababu ina uhusiano wa moja kwa moja na maisha ya wengi.