Ulaya. Wakati Luis Suarez (38) akisifiwa duniani kote kwa mafanikio yake katika soka, sehemu kubwa ya safari yake imejengwa juu ya nguvu na msaada kutoka kwa mkewe, Sofia Balbi (36), ambaye walifahamiana kitambo.

Kulingana na historia yake, Sofia ni mwanamke mwenye ustaarabu na uvumilivu, na sasa akisimama si tu kama mke wa mwanasoka maarufu, bali pia kama mfanyabiashara, mama na mfano wa kuigwa.

Ameona maisha ya familia ya Suarez kabla ya umaarufu na mafanikio. Mara kwa mara, Suarez amekuwa akisema kuwa Sofia ndiye aliyekuwa nguzo yake wakati wa vipindi vigumu, haswa mwanzoni mwa soka lake.

Suarez alikulia kwenye umasikini akikumbana na changamoto nyingi, mathalani katika umri wa miaka tisa tu, tayari alishafanya kazi ya kufagia mitaani ili kusaidia familia baada ya baba kuondoka nyumbani.

Akiwa katika kipindi kigumu zaidi huko Montevideo, Suarez mwenye umri wa miaka 15 wakati huo, ndipo akakutana na Sofia, msichana wa miaka 13 ambaye alibadilisha historia ya maisha yake.

Ni kama Sofia aliingiza mwanga kwenye maisha ya Suarez yaliyokuwa na misukosuko, akimpa msaada hasa wa kifedha kila mara pamoja na kumnunulia vitu vizuri.

Mwaka 2003, Sofia alihamia Barcelona, Hispania kuendelea na masomo yake, jambo lililomuumiza sana Suarez, na pia kuleta mtazamo tofauti kuhusu hatima ya maisha yake ya baadaye.

“Sofía alipoondoka, niliacha kucheza soka. Lakini baadaye nikagundua kuwa nahitaji kujitoa kikamilifu kwenye mchezo huu mzuri,” Suarez alikumbushia.

Baada ya kuifungia timu yake ya Nacional magoli manne katika mechi moja, klabu ya Groningen ya Uholanzi ilimsajili, jambo lililomfungulia mlango wa kutamba katika soka la kulipwa barani Ulaya.

Sofia alijiunga naye muda mfupi baadaye nchini Uholanzi, na hivyo kumaliza maumivu ya uhusiano wa mbali, na kuzikaribia ndoto zao.

Baada ya kuungana tena na kipenzi chake, kazi ya mchezaji huyo ilitambulika na wengi kutoka Groningen kwenda Ajax, Liverpool, Barcelona hadi Atletico Madrid.

Suarez aligeuka kuwa mmoja wa washambuliaji bora zaidi katika historia ya soka. Katika kila mafanikio yake, Sofia alisimama upande wake, akimkumbusha alikotoka na alichopigania.

Baada ya milima na mabonde kwenye safari yao ya mapenzi, hatimaye mwaka 2009, Suarez na Sofia walifunga ndoa, na kwa sasa tayari wana watoto watatu, Delfina (2010), Benjamin (2013) na Lautaro (2018),

Mwaka 2019, baada ya miaka 10 ya ndoa, walihuisha viapo vyao katika sherehe kubwa nchini kwao Uruguay iliyohudhuriwa na mastaa wengi akiwemo Lionel Messi na mke wake, Antonela.

Akizungumza na gazeti la Uingereza, Sportsmail mnamo Aprili 2013, wakati huo akiichezea Liverpool, Suarez alisema kuwa mke wake ndiye mtu anayemkosoa zaidi katika kazi yake.

“Sofia anaweza kuwa mkali kwangu. Hunisema sana ninapokosea uwanjani. Napenda nikikosolewa na Brendan Rodgers kuliko mke wangu. Brendan huwa makini zaidi kuliko mke wangu anavyoongea.

“Yeye kila mara huja uwanjani kunitazama. Huuliza ninafanya nini, kwa nini nabishana na mwamuzi. Baadaye husema, ‘Hujafanya chochote zaidi ya kubishana, kwa nini usijikite kwenye kucheza mpira?'” alieleza Suarez.

Mwaka 2014, Suarez alijiunga na Barcelona, hatua iliyomwezesha kuishi karibu na familia ya Sofia. Kuhusu uhamisho huo akitokea Liverpool, Suarez kupitia makala yake (Crossing the Line – My Story) alisema;.

“Liverpool walifanya kila wawezalo nibaki, lakini kucheza na kuishi Hispania ambako familia ya mke wangu inaishi ni ndoto ya maisha na matarajio yangu. Ninaamini sasa ndiyo wakati sahihi,” alisema Suarez wakati huo.

Akiwa tayari katika orodha ya wake na wapenzi wa wachezaji maarufu (WAGs), Sofia alipofika Barcelona, alipata marafiki kama Antonela Roccuzzo (mke wa Messi), Shakira (mke wa zamani wa Gerard Pique) na Elena Galera (mpenzi wa Sergio Busquets).

Ingawa watu wengi wanamfahamu kama mke wa Suarez, Sofia ana utambulisho wake binafsi, ambapo ni mfanyabiashara katika sekta ya urembo na mitindo.

Huyu ni mmoja wa waanzilishi wa duka la viatu vya kifahari linaloitwa Sarkany, akiwa pamoja na Antonela Roccuzzo. Biashara hiyo ilizinduliwa mwaka 2017 huko Barcelona na mara moja ikavutia wengi kwenye tasnia ya mitindo.

Kutokana na ujuzi wake wa mtindo na uelewa wa biashara, mara nyingi Sofia hualikwa kwenye matukio ya mitindo na uzinduzi wa bidhaa zake.

Uwepo wake katika ulimwengu wa mitindo unaonyesha safari tofauti na ile ambayo wake wengi wa wanasoka wameizoea. Sofia ameonyesha dhamira ya kujitengenezea mafanikio binfasi huku akiyebabea vizuri majukumu ya kifamilia.

Akiwa mama wa watoto watatu, ameweka kipaumbele kuhakikisha watoto wote wana mazingira tulivu na ya faragha, na kudumisha mahitaji ya hadhi ya juu yanayoendana na umaarufu wa mumewe.

Mara kwa mara katika ukurasa wake wa Instagram wenye wafuasi zaidi ya milioni 2, huposti matukio kutoka ndani ya familia yake hasa akiwa na watoto wao uwanjani wakimuunga mkono Suarez kwenye mechi zake.

Kwa sasa akiichezea Inter Miami inayoshiriki Ligi Kuu Marekani (MLS), Suarez anaendelea kuheshimika kama mmoja wa wachezaji bora katika kizazi chake, na mmoja wa washambuliaji hatari zaidi katika historia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *