Marekani. Mwigizaji wa Marekani, Leonardo DiCaprio (57), amesema hana majuto yoyote kuhusu uamuzi wake wa kuikataa nafasi ya kuigiza katika filamu ya Boogie Nights (1997) na badala yake kuichagua Titanic (1997) ambayo ilimtambulisha kimataifa.

Katika mahojiano na Deadline hivi karibuni, DiCaprio alikanusha madai kwamba yeye mwenyewe alimtamka kuwa kutokushiriki katika filamu ya Boogie Nights ni jambo analolijutia zaidi katika kazi yake ya sanaa.

DiCaprio alisema kauli hiyo ilitafsiriwa vibaya, kwani ilikuwa katika muktadha wa mazungumzo ya kirafiki na Paul Thomas Anderson ambaye ndiye mtayarishaji wa Boogie Nights.  

Alisema alikuwa akieleza jinsi alivyoipenda kazi ya Anderson, na kwamba Boogie Nights ilikuwa filamu iliyokuwa tukio la kipekee kwake kwa namna ilivyoibua mwelekeo mpya wa sinema duniani.

“Naam, nadhani hilo lilikuwa jibu langu kwa swali lililokuja wakati nikizungumza na Anderson. Ni jibu lililokuja bila kuingia sana katika maisha yangu binafsi, swali lilikuwa, ‘Ni jambo gani unalolijutia zaidi?’”

“Tulikuwa tumeketi tukizungumzia filamu, hivyo jibu lilitoka katika mtazamo wa kuwa shabiki wa kazi zake kwa muda mrefu,” DiCaprio alifafanua kauli hiyo iliripotiwa na Jarida la Esquire toleo la Mavericks of Hollywood.

Kwa mujibu wa taarifa, nafasi ya Eddie Adams/Dirk Diggler katika Boogie Nights alipewa kwanza DiCaprio, lakini aliikataa kwa sababu tayari alikuwa amesaini mkataba kuigiza Titanic chini ya James Cameron.

Hatimaye Mark Wahlberg akaja kuchukua nafasi hiyo na kuitendea haki, kitu kilichompa umaarufu mkubwa katika ulimwengu wa filamu miaka hiyo.

“Nakumbuka tuliitazama filamu hiyo (Boogie Nights) na kushangazwa sana, ilikuwa kama ujio wa gwiji mpya wa sinema. Sasa, sidhani kama kuna mtu angefanya kazi bora kuliko Wahlberg katika filamu hiyo, kwa hiyo niliyasema hayo katika mtazamo wa kuwa shabiki,” alisema.

“Hakuna majuto, kwa sasa nikitazama nyuma, ninashukuru kuwa sehemu ya Titanic, ni nafasi iliyonipa kujiamulia mwelekeo wa kazi yangu kwa miaka yote iliyofuata. Nilitamani kufanya filamu zote mbili, lakini kwa wakati ule hilo lisingewezekana,” alisema DiCaprio.

DiCaprio alihitimisha kwa kusema kuwa bila Titanic, hawezi kujua kama kazi yake kwa sasa ingekuwa katika nafasi iliyonayo duniani wakati huu, na hilo ndilo linamfanya awe mwenye shukrani kubwa kwa kupata fursa hiyo.

Ikumbukwe filamu ya Titanic (1997) inazungumzia mapenzi, maisha ya tabaka tofauti, na janga la kihistoria la kuzama kwa meli ya Titanic lililotokea mwaka 1912.
Inasimulia hadithi ya kijana maskini, Jack Dawson na msichana wa kishua, Rose DeWitt Bukater ambaye tajiri Cal Hockley anataka kumuoa.

Jack na Rose wanakutana ndani ya meli ya kifahari ya RMS Titanic, na licha ya tofauti zao za kimaisha, wanaanzisha uhusiano uliokuwa kinyume na matarajio ya jamii. Wakati uhusiano wao ukikua, meli inapigwa na barafu na kuanza kuzama..!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *