Dar es Salaam. Zimesalia siku 25 tu kuumaliza mwaka 2025. Mwaka ambao umebadilisha ramani na taswira ya muziki wa Singeli. Kutoka kuonekana wa kihuni hadi kuwa biashara na utambulisho kwa Tanzania.
Licha ya kuanza kufanyika kwa muda mrefu lakini muziki huo umepata mapokeo makubwa kwa mwaka 2025. Huku ukizalisha wasanii wapya wengi wanaofanya vizuri katika kiwanda hicho.
Ubora wake na upekee ukapelekea Singeli kuingia kwenye mikakati ya kutambulika kama urithi wa dunia. Twende pamoja…
Kutambulika urithi wa dunia
Kutokana na upekee wa aina hiyo ya muziki Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Palamagamba Kabudi akiwa Bungeni, jijini Dodoma Mei 7, 2025 alipokuwa akiwasilisha makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/26, alisema muziki wa singeli upo mbioni kutangazwa rasmi na UNESCO kuwa sehemu ya orodha ya urithi wa dunia.
“Muziki wa Singeli, unatumia vionjo vya ngoma za asili ikiwamo midundo na mikong’oso. Midundo ya Singeli imeendelea kuzalishwa kwa wingi kupitia kivunge cha mtozi kilichotengenezwa na BASATA.
“Upekee wa Singeli umeifanya kuwa kivutio kikubwa katika matamasha makubwa ya kimataifa kama vile “Nyege Nyege” Festival nchini Uganda, DUO Festival nchini Ubelgiji, Primavera Sound Festival Nchini Hispania, Apporlibation Festival nchini Ujerumani na Cora Festival nchini Ufaransa,”alisema Kabudi.
Hakuishia hapo alisema wizara iliandaa nyaraka muhimu za uteuzi (Nomination Dossier) na kuziwasilishwa UNESCO Makao Makuu Paris, Ufaransa kwa ajili ya hatua za kuidhinishwa kwa singeli kuwa sehemu ya Orodha ya Urithi wa Dunia.
“Hivi sasa kinachosubiriwa ni kukamilika kwa taratibu za UNESCO ili hatimaye kutangaza rasmi kuwa sehemu ya Orodha ya Urithi wa Dunia, hatua ambayo itaimarisha zaidi hadhi ya utamaduni wa Tanzania Duniani,”alisema.
Wasanii wapya kwenye Singeli
Kutokana na mwamko mkubwa kwa jamii dhidi ya muziki huo. Mwaka 2025 vimetambulika vipaji vingi, licha ya wasanii hao kujitafuta kwa muda mrefu. Hilo limejionesha kwa wasanii kama Dogo Paten, Dogo Sajent, K Zungu, Dogo Elisha, Pacheko Midundo na wengine wengi
Dogo Paten
Msanii huyo wa singeli, nyota yake inazidi kung’ara kila uchao tangu Zuchu alipomshika mkono. Kabla ya hapo Dogo Paten hakuwa ametoa ngoma rasmi alirekodi vipande tu vya wimbo ‘Afande’ na kuvipakia kwenye mitandao ya kijamii hasa TikTok na Instagram ambako huko Zuchu alivutiwa nao.
Baada ya kuupenda msanii huyo wa WCB, akatangaza kufanya naye remix ili kumpa dogo huyo sikio kwa wapenda muziki. Na kweli wakafanya ngoma hiyo ambayo ilipigwa kila mtaa na kumfanya Paten kujipatia mashabiki wengi watoto, vijana hadi wazee.
Mdogo Sajent
Utakumbuka awali Mdogo Sajent na Paten walikuwa wakifanya muziki pamoja, hadi kufanya remix ya wimbo wa Marioo ‘Salio’. Lakini wawili hao walifarakana na kila mmoja akaanza kufanya kazi kivyake.
Hivyo basi Sajent akapita njia yake na kukutana na Chino Kidd ambaye hadi sasa anamsimamia kimuziki. Akiwa chini ya Chino amefanikiwa kuachia ngoma kama vile, Mapenzi Basi, pamoja na EP yenye nyimbo tatu Mlegezo, Far na I miss you.
Pacheko Midundo
Huyu ni DJ wa singeli ambaye amefahamika zaidi 2025, baada ya kuibua kipaji cha Mama Amina msanii mwenye ulemavu katika mfumo wake wa uongeaji. Popote itapopigwa ngoma ya Pacheko na Mama Amina watu huruka na kusahau shida zao.
Huyu ni msanii wa singeli ambaye aliianza kuimba tangu akiwa shule ya msingi. Darasa la saba alipata nafasi ya kushiriki Singeli Search na kuibuka mshindi. Tangu hapo hakuweza kupata sikio kwa ukubwa kama ilivyokuwa 2025.
Kwa sasa ameachia wimbo mpya uitwa ‘Kuna Wakati’. Akizungumza na Mwananchi alisema
“Kuna siku Mzee wa Bwax alikuja studio kurekodi, basi wakati wameplay beat mimi nikawa naimba kama masihara.
“Wakaanza kuniambia mbona nzuri hiyo ngoja nikuchukue clip. Basi wimbo huo ukaanzia hapo, nikaurekebisha kidogo na ndio huo ambao watu wanatamba,” alisema.
Aidha wasanii wa muziki huo wameendelea kujipatia maokoto kutokana na matamasha mbalimbali yaliyofanyika 2025. Huku kukiwa na lile kubwa la Agosti 2.
Tamasha hilo ni lile la muziki wa singeli lililofanyika katika michuano ya CHAN. Julai 31, 2025 Gerson Msigwa akiwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo alisema kwa sasa Tanzania hakuna muziki unaopendwa na watu wengi, wenyeji na wageni kama Singeli.
“Tumegundua hakuna ‘vibes’, linalofikia muziki wa singeli katika muziki wote Tanzania. Wazungu wanachanganyikiwa ukipigwa, wanacheza na kuimba huku hawajui wanaimba nini.
“Ni muziki unaozalisha ajira kwa vijana, lazima tuupromote, tuulinde na maeneo wanayofanya vibaya tutawarekebisha ili dunia ijue kuwa asili ya singeli ni Tanzania,” alisema Msingwa.
Wanachosema wasanii
Akizungumzia maendeleo ya Singeli mzalishaji wa muziki huo DJ Mushizo ameiambia Mwananchi ni wakati wa wasanii kuongeza juhudi.
“Nadhani sisi wasanii tunatakiwa kuwekeza juhudi na kuufanya muziki wa singeli kwa umakini zaidi. Kwa sababu hadi watu wakubwa wanaona muziki katika jicho la tatu hii ni fursa yetu kukaza zaidi. Ombi langu waanze kwa kugusa kwenye uwekezaji”, alisema Mushizo.
Naye msanii wa muziki huo na mshindi wa Tuzo za TMA mara nne Dulla Makabila alisema singeli ndiyo muziki unaoweza kuleta tuzo ya aina yoyote nchini.
“Singeli ni utamaduni wa Tanzania na ndiyo kitambulisho na una nguvu ya kuleta tuzo yoyote kwenye hii nchi. Ni watu tu wanafanya kazi ya kudandia miziki ya watu.
“Lakini ni kitu kikubwa ambacho hatujaamua kukiwekea nguvu na kufanya uwekezaji mkubwa. Serikali ianze kugusa wasanii wenyewe wa singeli,” alisema Makabila.
Historia ya Singeli
Akielezea historia ya muziki wa singeli, Selemani Msonjele ‘Msaga Sumu’ anasema muziki huo umetokana na vigodoro na ngoma za asili.
“Huu muziki ni wa Kitanzania chimbuko lake ni hapa hapa na umetokea kwenye asili ya vigodoro, enzi hizo pamoja na ngoma za asili. Kadiri siku zinavyokwenda unabadilika mfano zamani ulikuwa sio wa kasi, ulikuwa unapigwa taarabu.
“Sisi tunachukua biti tupu ya taarabu tunaingizia maneno yetu lakini kwa sasa, vizazi vipya vinazidi kuja muziki huo unabadilika,”anasema Msaga Sumu ambaye ni kati ya waasisi wa muziki huo.
Anasema muziki huo unachukuliwa wa kihuni kutokana na kukubalika na vijana wengi.
“Muziki ulikuwa unachukuliwa wa kihuni kutokana na ulipotokea. Umetokea uswahilini zamani muziki huu ulipokuwa unapigwa sehemu yoyote waliokuwa wanahudhuria wengi ni vijana wa kike na kiume ndio maana unaambiwa wa kihuni, lakini muziki huu hauna uhuni wowote,” anasema Msaga Sumu.
Mbali na Msaga Sumu, Mrisho Kulwa ‘Dj Mrisho’ ambaye ni kati ya waasisi wa muziki huo amewahi kueleza kuwa awali walikuwa wakiufanya muziki huo kwa kupenda bila kujua baadaye utaleta mafanikio.
“Zamani wakati naanza kuurekodi ilikuwa wanaoimba muziki huu ni wachache Msaga Sumu, Khalid Kapala, Majid Bigoma. Hao ni wasanii wa zamani ambao tulikuwa tunafanya nao na tulienda mpaka chimbuko la wasanii wengine wakaanza kuja,” anasema.
Anasema singeli ni biti inayokimbia kwa sasa wanaita bakora na muziki unaoenda taratibu unaitwa ladha.
“Kuna kijana alikuwa anaitwa Dulla Six Bullet ni msanii anayeimba nyimbo za haraka, alikuwa na dansa wake anaitwa Kisingeli. Alikuwa akipanda jukwaani kuimba anamuita Kisingeli njoo.
“Na yule alikuwa akipanda pale anacheza style zake pale jina liliondoka watu wakaanza kuuita muziki kisingeli lakini hilo ni jina la mtu. Zamani tulikuwa kama tuna ukanda wasanii wa Tandale walikuwa wakiimba muziki wa taratibu kina Msaga Sumu lakini wa Mburahati waliimba wa haraka na hao waasisi walikuwa Makaveli, Dulla Six Bullet hiyo ilikuwa ni kati ya mwaka 2005 , 2007, “anasema.