Namungo FC imezoa tuzo mbili za Ligi Kuu Tanzania Bara mwezi Novemba ikibebwa na mwenendo mzuri iliokuwa nao mwezi huo.

Taarifa iliyotolewa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) leo, imeeleza kuwa Namungo imeshinda Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwezi Novemba na ile ya Kocha Bora wa mwezi huo.

Walioshinda ni mshambuliaji Fabrice Ngoy na Kocha Juma Mgunda.

“Mchezaji huyo (Ngoy) aliwashinda Saleh Karabaka wa JKT Tanzania na Andrew Chamungu wa Namungo alioingia nao fainali katika mchakato wa Tuzo za Mwezi uliofanywa na Kamati ya Tuzo za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

“Kwa upande wa Mgunda (Juma) aliyeingia fainali katika mchakato huo na Ahmad Ali wa JKT Tanzania na Francis Baraza wa Pamba Jiji, aliiongoza timu yake kushinda michezo miwili na kutoka sare mmoja na kupaa kutoka nafasi ya 13 hadi ya nne kwenye msimamo wa ligi hiyo, huku Namungo ikizifunga Dodoma Jiji (2-0), Mbeya City (0-1) na ikitoka 1-1 na Azam FC,” imefafanua taarifa ya TPLB.

Wakati huohuo Meneja wa Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Said Mpuche, amechaguliwa kuwa Meneja Bora wa Uwanja kwa mwezi Novemba.

Katika hatua nyingine golikipa wa Geita Gold, Deogratius Munishi, amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mwezi Novemba wa Ligi ya NBC Championship 2025/26, huku Zuberi Katwila pia wa Geita Gold akichaguliwa kuwa Kocha Bora wa mwezi huo.

Munishi aliyeingia fainali katika mchakato huo na Joseph Mahundi wa Kagera Sugar na Brown Mwankemwa wa Mbeya Kwanza alionesha kiwango chenye mendelezo ikiwa ni pamoja na kucheza dakika 360 za michezo minne bila kuruhusu bao.

Kwa upande wa Katwila aliyeingia fainali na Juma Kaseja wa Kagera Sugar na Mwaka Mwalwisi wa Mbeya Kwanza aliwezesha timu yake kushinda michezo yote minne iliyocheza mwezi huo na kupaa kutoka nafasi ya nne hadi ya kwanza kwenye msimamo wa ligi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *