Afrika Kusini. Muziki umeendelea kuwa lugha ya pekee duniani inayoweza kuunganisha watu bila hata kutamka neno, ukivuka mipaka ya tamaduni, vizazi na hata hisia. Kawaida muziki umekuwa kimbilio la wengi hasa pale ambapo maneno ya kawaida hushindwa kueleweka.

Uhalisia wa hili huonekana hata pale ambapo watu huimba nyimbo za lugha fulani ambazo hata hawazifahamu. Kama ilivyo sasa kwa wimbo ‘Africa for Jesus’ (Makomborero) ulioimbwa na  bendi ya Worship House. Fahamu zaidi

Kwa zaidi ya miaka ishirini, kundi la Worship House kutoka Limpopo, Afrika Kusini limeendelea kuwasha moto wa injili barani Afrika kupitia muziki wa injili. Wakipendelea kufanya zaidi ibada za moja kwa moja (live worship).

Kundi hili ambalo linatikisa sasa kwa wimbo wao ‘Africa for Jesus’ (Makomborero), lilianzishwa mwaka 2003 chini ya uongozi wa mchungaji na mwongozaji wa ibada, Bishop Isaac Dagada, kama mradi wa kukuza vipaji vya vijana katika eneo la Shirley Village, Limpopo. 

Wazo lake lilikuwa kuunda jukwaa la kuibua waimbaji na wapiga vyombo wenye uwezo wa kuipeleka injili kwa njia ya muziki wa kisasa. Lakini wenye mizizi ya Kiafrika ndiyo maana lugha mbalimbali hutumika. 

Ndani ya muda mfupi, mambo yalijipa kundi lilikusanya mamia ya waimbaji, kuanzia vijana wadogo hadi watu wazima, wote wakiwa na lengo moja la kumuabudu Mungu.

Moja ya sifa kuu zinazowatofautisha Worship House na makundi mengine ya nyimbo za injili ni utaratibu wao wa kutoa albamu za live worship. Badala ya kurekodi studio, wao huandaa ibada halisi katika viwanja au makanisa makubwa, wakirekodi kila tukio.

Hii imekuwa sababu ya mafanikio yao, kwani msikilizaji hata kama akiwa anatazama kwenye runinga au anasikiliza huhisi kama yupo pamoja na waumini wengine.

Albamu zao
Katika safari yao, Worship House wamefanikiwa kutengeneza zaidi ya albamu 10 na nyimbo ambazo zimeendelea kushika nafasi ya juu katika makanisa na majukwaa ya injili.

Nyimbo kama Modimo wa Lefase, Ke Boha, Ndza Ku Vona, Nara Ekele na By Fire By Force zimepata mashabiki wengi Afrika Mashariki, hususan Tanzania, ambapo kundi hili linapendwa kiasi cha kutumika katika nyumba za ibada, nyumbani hata kwenye matukio ya kijamii kama vile harusi.

Moto wa Makomborero
Licha ya kuwa na nyimbo nyingi lakini hakuna wimbo uliyoigusa Afrika kama ‘Africa for Jesus’ , unaopatikana katika albamu yao mpya ‘Makomborero 21 (Live)’. Makomborero ni neno la Kishona (Zimbabwe) kwa maana ya baraka. 

Ndani ya wimbo huu, Worship House wanatangaza imani kuwa Afrika ni bara lenye kusudi, nuru na linapaswa kutengwa kwa ajili ya Yesu. 

Ingawa Worship House ni kutoka Afrika Kusini, wimbo huu umetumia lugha ya Kishona, Kiingereza na lugha za Afrika za Kusini. Hii ni kawaida kwao hutumia mchanganyiko wa lugha mbalimbali za Afrika.

Hata hivyo nchini kwa sasa kila mtu ana tafsiri yake kutokana na wimbo huu. Huku baadhi wakiuita wimbo wa kikombozi lakini uhalisia ni kwamba wanaimba Mungu ametujaza baraka nyingi za uhai, familia, ulinzi, neema na kutuvusha kwenye magumu. Unakiri kwamba baraka zote zinatoka kwa Mungu.

Mbali na aina ya uimbaji wa kundi hili hata wasanii wa muziki wa injili nchini kwa sasa wanaonekana kuhamia katika utamaduni wa kuimba na kurekodi moja kwa moja kutoka kwenye majukwaa tofauti na awali wengi walikuwa wakiingia studio kurekodi wimbo. Na nyimbo zilizotumia mtindo huo kawaida mapokezi huwa mazuri

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *