
Katika enzi za utandawazi na ushindani wa kiuchumi, usafiri wa anga umeendelea kuwa mhimili muhimu unaounganisha watu, masoko na mataifa.
Tanzania, kama nchi inayojipambanua kuwa kitovu cha uchumi wa kikanda, imewekeza kwa kiasi kikubwa katika kukuza miundombinu ya anga na kuvutia shughuli za biashara na utalii.
Mathalani, zaidi ya Sh 93.36 bilioni zimetengwa na Serikali kwa mwaka wa 2025/2026 kwa ajili ya miradi ya ujenzi wa viwanja vya ndege vya Mwanza, Arusha, Mtwara, Kilimanjaro, Serengeti, Bukoba, ukarabati na upanuzi wa viwanja vya ndege vya Lindi, Moshi, Musoma, Mafia, Shinyanga na Sumbawanga bila kusahau uboreshaji na upanuzi wa jengo la pili la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).
Hata hivyo, utekelezaji wa miradi yote hiyo hutegemea kwa kiwango kikubwa uwepo wa amani na utulivu wa ndani ya nchi, misingi ambayo ndiyo kichocheo cha ustawi wa watumiaji wa miundombinu hiyo na ukuaji wa sekta ya anga kwa ujumla.
Amani na umoja ni miongoni mwa misingi iliyobainishwa katika dira ya maendeleo 2050. Dira hiyo inatambua umuhimu wa kila mwananchi kudumisha amani, umoja na mshikamano kama msingi wa maendeleo.
Aidha, ni muhimu kuhakikisha watu wote wanaheshimiana na kuchangia katika kufanikisha malengo ya pamoja ya kitaifa.
Amani na utulivu hutengeneza mazingira salama na ya kuaminika yanayochochea uwekezaji katika viwanja vya ndege, miundombinu ya usafiri na teknolojia za kihuduma.
Mashirika ya ndege, wawekezaji na washirika wa kimataifa hufanya maamuzi yao kulingana na tathmini ya usalama wa nchi husika. Hadi kufikia machi 2025, daftari la usajili wa ndege nchini lina jumla ya ndege 467 kutoka katika mashirika ya ndege zaidi ya 60.
Pindi kunapokuwa na machafuko au kuyumba kwa hali ya usalama, sekta ya anga huwa miongoni mwa sekta za kwanza kuathirika, kwani shughuli zake hutegemea miruko ya safari za ndege, uhakika wa ratiba, na uimara wa mifumo ya usimamizi wa usalama.
Takwimu za kimataifa kutoka kwa mashirika yanayosimamia usafiri wa anga zinaonesha kuwa nchi zinazokumbwa na machafuko hupoteza kati ya asilimia 40 hadi 60 ya safari za kimataifa katika mwaka wa kwanza wa misukosuko.
Hii huathiri kwa kiasi kikubwa mapato ya serikali, ajira za moja kwa moja kwenye viwanja vya ndege, pamoja na sekta nyengine zinazotegemea usafiri wa anga kama utalii, kilimo cha biashara, usafirishaji wa mizigo na masoko ya kimataifa.
Kwa mantiki hiyo, uwepo wa amani thabiti ni kichocheo kikubwa cha kuimarika kwa uchumi kupitia nguvu ya sekta ya anga.
Kwa upande wa watumiaji wa huduma za anga, amani na utulivu ni zaidi ya masuala ya usalama wa kitaifa; ni msingi wa ustawi wao kama wateja. Abiria anahitaji huduma salama, za kuaminika na zisizo na misukosuko inayosababishwa na hali ya sintofahamu ya kitaifa.
Amani inapokuwepo, ratiba za safari huwa thabiti, gharama za tiketi hubaki katika viwango vinavyoweza kushindanishwa, na mashirika ya ndege pamoja na mamlaka za udhibiti huweza kuboresha ubora wa huduma na kuhakikisha haki za watumiaji zinalindwa kwa ukamilifu.
Akizungumza na gazeti hili, katibu mtendaji wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma ya Usafiri wa Anga (TCAA CCC), Innocent Kyara amesema,
“Kukosekana kwa amani na utulivu katika nchi huathiri moja kwa moja gharama za uendeshaji wa mashirika ya ndege, jambo ambalo husababisha ongezeko la bei ya tiketi kwa abiria,”
“Machafuko au hatari za kiusalama huifanya sekta ya anga kuonekana kuwa na kiwango kikubwa cha hatari, hivyo kampuni za bima huongeza malipo ya bima (premium) kwa mashirika ya ndege ili kufidia hatari hizo,” amesema kyara
Kadiri gharama hizi zinavyoongezeka, mashirika ya ndege hulazimika kuhamishia mzigo huo kwa watumiaji kupitia kupandisha viwango vya nauli ili kuendelea kujiendesha.
Matokeo yake ni ongezeko la gharama kwa abiria, kupungua kwa uwezo wa watu kusafiri kwa ndege, na kupungua kwa ushindani ndani ya soko la usafiri wa anga”
Aidha, utulivu wa ndani ya nchi hutoa nafasi kwa mashirika ya ndege kuwekeza katika teknolojia mpya, kuongeza idadi ya safari, na kuboresha huduma za ndani na za kimataifa.
Hii inachochea ushindani wa kibiashara unaowanufaisha moja kwa moja watumiaji kupitia huduma bora, ufanisi wa uendeshaji na upatikanaji wa chaguo nyingi za usafiri.
Kwenye ngazi ya uchumi mpana, sekta ya anga inachangia moja kwa moja ukuaji wa uchumi kupitia ajira kwa maelfu ya watu, uwekezaji wa ndani na nje ya nchi, na kuongeza mapato ya nchi kupitia utalii na biashara.
Serikali inapoweka mkazo katika kulinda na kudumisha amani, inalinda pia maslahi ya wananchi wanaotegemea sekta hii kwa shughuli zao za kila siku, biashara na harakati za kijamii.
Kwa kuzingatia hayo, ni dhahiri kuwa amani si tu suala la usalama wa taifa bali ni nyenzo ya msingi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Tanzania, ikiwa katika hatua muhimu ya kupanua miundombinu ya anga na kuongeza uwezo wa ushindani katika kanda, ina wajibu mkubwa wa kuendeleza utulivu uliopo ili kuimarisha nafasi yake katika ramani ya uchumi wa afrika mashariki na ulimwengu kwa ujumla.
Kwa hakika, bila amani hakuna jitihada za kuinua sekta ya usafiri wa anga zitakazoweza kuleta matokeo chanya. Amani ndio nguzo kuu inayofungua anga, inatoa ujasiri kwa watumiaji, inahamasisha uwekezaji, na hatimaye inatoa mwelekeo thabiti kwa uchumi kukua kwa njia endelevu.
Kwa mawasiliano na elimu zaidi, wananchi wote wanaweza kutembelea tovuti yetu (www.tcaa-ccc.go.tz) au kuwasiliana nasi kupitia mitandao yetu ya kijamii ya instagram (@tcaa_ccc), mtandao x (@tcaa_ccc1), youtube (@tcaa_consumerconsultativecouncil) au kupiga simu ya bure 0800 110 190 au kuwasiliana nasi kupitia anuani iliyoainishwa hapa chini;-
Katibu Mtendaji,
Baraza la Ushauri la Watumiaji Huduma za Usafiri wa Anga (TCAA CCC),
Majengo ya TBA Na. L1, Kiwanja Na. 6/2,
Mtaa wa Kilimani, Barabara ya Ali Hassan Mwinyi,
S.L.P. 12242,
14110 DAR ES SALAAM.