
Rwanda imeyatuhumu majeshi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Burundi kuwa yamekiuka usitishaji mapigano kwa mujibu wa makubaliano ya amani yaliyofikiwa karibuni huko Washington kwa lengo la kuhitimisha hali ya mchafukoge mashariki mwa Kongo.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Rwanda jana ilisema katika taarifa yake kwamba Rwanda haiwezi kubebeshwa dhima kwa ukiukwaji wa usitishaji mapigano, mashambulizi na mapigano yanayoendelelea kushuhudiwa katika jimbo la Kivu Kusini.
Rwanda imeyatuhumu majeshi ya Kongo na Burundi pamoja na muungano wao unaowajumuisha wanamgambo na mamluki wa kigeni kwa kutekeleza mashambulizi yaliyoratibiwa dhidi ya vijiji vya raia vilivyo karibu na mpaka wa Rwanda kwa kutumia dege za kivita na ndege zisizo na rubani, ambazo (muungano wa waasi) waAFC/M23 umesema umelazimika kukabiliana nazo.
Rwanda jana Jumatano ilitoa taarifa hii kufuatia hotuba ya Rais Felix Tshisekedi wa Kongo bungeni siku ya Jumatatu ambapo aliituhumu Rwanda kuwa inakiuka makubaliano ya amani yaliyosimamiwa na Marekani.
Wakati huo huo taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Rwanda imebainisha kuwa jeshi la Burundi linadaiwa kukusanya takriban wanajeshi 20,000 katika mkoa wa Kivu Kusini ili kuisaidia serikali ya Kongo, na hasa kuzingira vijiji vya Banyamulenge huko Minembwe katika hatua ya makusudi ili kuwaua kwa njaa wakazi wa vijiji hivyo.
Tarehe 4 mwezi huu wa Disemba Marais wa Kongo na Rwanda walisaini makubaliano ya amani na uchumi kwa lengo la kuhitimisha mapigano huko mashariki mwa Kongo.
Hata hivyo Rwanda inadai kuwa Kongo imetamka wazi kuwa haitaheshimuusitishaji vita wowote, na kwamba ilikuwa ikipambana kuyatwaa maeneo yaliyoangukia mikononi mwa waasi wa AFC/M23 hata kama mchakato wa amani utaendelea.