
Dar es Salaam. Alizaliwa akionekana msichana. Hati zake zote za utambulisho zikaandikwa majina ya kike na jinsia ya kike.
Lakini tangu akiwa na umri wa miaka mitatu, hakuwahi kujihisi hivyo wala kuona nafsi yake ndani ya nafasi ya kike aliyopewa. “Nilijiona na kujihisi kabisa kama mwanaume ingawa maumbile yangu yalikuwa tofauti,” anaanza kusimulia kijana huyo mwenye umri wa miaka 24 (jina linahifadhiwa).
Akiwa mdogo, alijaribu hata kuwaambia wazazi wake wampeleke kwa wachungaji au mapadri “kumbadilisha” kwa vile aliamini wao wana uwezo huo. “Waliona kama ni utoto,” anaongeza.
Changamoto shuleni
Kijana huyo, mwanaharakati na mfanyabiashara za kimataifa, safari yake ya elimu ilikuwa yenye mkanganyiko. Alisoma shule za wasichana za bweni kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne na kidato cha tano na sita.
Maisha yake ya shuleni hayakuwa tu ya masomo. Alikuwa kiongozi. Aliwahi kuwa Rais wa shule ya sekondari. Hapo ndipo mbegu za uanaharakati zilianza kuchipuka, hali ambayo baadaye ilimwelekeza katika kuandika kitabu chake ‘Root of Resistance’, kinachoelezea safari yake ya ukuaji na uongozi.
Kadiri alivyoendelea kukua, mwili wake ulianza kuonyesha sifa za kiume na mwonekano kuwa wa kiume kuliko ule uliokuwa kwenye nyaraka zake.
“Watu wakawa hawanielewi shuleni, nikasoma vizuri nikafika mpaka kidato cha sita pale ndipo ikawa ngumu kidogo. Nilikuwa na urafiki wa zaidi na msichana mmoja, wazazi wangu waliitwa shule wakaambiwa labda nikapimwe waelewe kweli jinsia yangu ni ipi.
“Hali hiyo kwa kweli ilinivuruga. Nilifanikiwa kufaulu, lakini si kwa kiwango cha juu nilichokuwa najua hapa lazima nipite, sababu ya changamoto nilizokuwa nazipitia shule,” anasimulia kijana huyo anayekiri alizaliwa na jinsi za kike, lakini maumbile yake ya mwili yakabadilika na kuwa mwanaume, ikiwemo kuota ndevu na sauti yake kuwa nzito.
Mchakato wa pasi ya kusafiria
Baada ya kujiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) aliendelea na masomo huku akianza kusafiri kibiashara, alihitaji pasipoti. Hicho ndicho kipindi kilichogeuka kuwa chanzo kikubwa cha maumivu na unyanyasaji.
Anasimulia kuwa alifika ofisi za uhamiaji akiwa amejipanga vyema, lakini akakutana na simulizi ya kushangaza.
Kulikuwa na mkanganyiko wa taarifa; baadhi ya vyeti vyake vinaonyesha yeye ni mwanamke “F”, lakini katika usajili wa Nida alisajiliwa kama mwanaume “M” baada ya mpigapicha kuandika kwa mkono kuwa “he is supposed to be a man.” Mchanganyiko huo ukawa chanzo cha mahojiano.
“Waliniuliza maswali mengi hata ya faragha sikuyapenda. Nilijisikia vibaya sana. Ilikuwa traumatizing, hadi sasa nikienda kwenye sekta yoyote ya uhamiaji najisikia kutotulia,” anasema.
Askari wa uhamiaji walimpeleka hadi hospitali kwa mbinu ya kushtua akiwa amezungukwa na askari wanne, waliingia Hospitali ya Taifa Muhimbili bila hata kukaguliwa getini. “Nilijiuliza, hivi hili ni kosa la jinai?” anakumbuka.
Alipofika Muhimbili, aliambiwa kutumia bima yake kama vile ni yeye aliyehitaji kupimwa. “Nilitaka mambo yaende ili nisafiri. Sikuwa na njia nyingine.” Bahati ilitokea pale tu alipomuita daktari anayemfahamu, aliyemtaja kwa jina la Dk Wangwe, ambaye alitoa elimu na maelezo kwa wahusika, ndipo akaachiwa aondoke.
Anasema akini safari ilishapotea, pasipoti hakupata, muda ukawa umekwisha.
Mwaka 2019, bado akiwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza, alirudi tena kufuata pasipoti kamili. Ndipo akakutana na kadhia iliyomuumiza zaidi.
Ofisa mmoja alimwambia: “Haturuhusu kuchukuliana pasipoti, huyu kwenye picha ni msichana mdogo ila hapa umeonekana kama mwanaume.”
Anasimulia kwamba baada ya hapo yalifuata mahojiano, kushangaliwa na kupigwa picha na maofisa waliokuwa wakigawana habari kuhusu mwili wake kana kwamba ni maonesho.
Kisha akapewa masharti: “Ili tuprint pasipoti yako, unyoe ndevu. Kata nywele. Nunua nguo za kike na uzivae. Ukiweza hata kodi hapo nje.”
Anasema: “Nilihisi maumivu kwa sababu sikutaka kuishi sura ambayo si mimi. Hata hivyo, kwa kuwa safari yangu ya kwenda Afrika Kusini ilikuwa wiki moja tu, nikalazimika kukodi dera nje ya ofisi. Wakati ninarudi ndani watu walinishangaa, kijana aliyevaa rasmi anaingia tena akiwa amevaa dera. Picha ya mwanzo wakaifuta, wakapiga ya ‘mtu wanayemtaka wao’.”
Kijana huyo anasema walidhani wamesuluhisha tatizo, kumbe wamemsababishia mateso makubwa.
“Tangu wakati huo, kila napopita airport hukaguliwa kupita kiwango, naulizwa maswali ya kuudhi kuhusu mwili wangu. Inaondoa molari ya kusafiri.
“Mwaka 2023, nilipokuwa nakwenda Nairobi, ofisa mmoja aliniambia: ‘Ilibidi wakupige pasipoti kama unavyoonekana, siyo hii waliyokupa imekuwa chanzo cha matatizo.’”
Anasema hali hiyo ilimfanya akakosa visa pia kwa sababu ya pasipoti hiyo hiyo.
Sheria na uelewa wa jamii
Anasema elimu kwa watendaji ni muhimu: “Watu kama sisi wapo na hatustahili kufanyiwa udhalilishaji wa aina yoyote.”
Anapendekeza marekebisho ya sheria na utambuzi rasmi wa watu wenye jinsia tata kama ilivyo Kenya. “Kwa sababu sisi hatufiti kwenye ‘mwanaume’ wala ‘mwanamke’.”
Kwa upande wa afya, anaeleza tatizo lake ni la kibaolojia, hivyo ni muhimu wazazi kuwaacha watoto waamue wenyewe.
“Wengine hawana ovari, hawana matiti, hawaingii hedhi, na wengine wana viungo vyote viwili. Ukiwafanyia upasuaji wakiwa watoto unawaathiri; waachwe wakue waamue wenyewe.”
Malengo na ujumbe wake
Kuhusu uhusiano binafsi, anasema si kipaumbele chake sasa.
“Mahusiano si kitu kibaya, lakini nitayaeleza kwenye kitabu changu Aprili 2026.”
Anasema amechagua maisha ya uanaharakati kupambana na ukatili aliouona tangu akiwa mdogo.
“Ningeshajitoa uhai, lakini ninaona nimeletwa duniani kurekebisha matatizo ya wengine. Lengo langu ni kutatua matatizo yanayowakabili wengine.”
Alichokisema daktari
Daktari mkunga mshauri katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na Mhadhiri mwandamizi Chuo Kikuu cha Muhas, Peter Wangwe anasema licha ya kufahamu changamoto anayoipitia kijana huyo, kwa watu wenye jinsi tata wamekuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi kisheria.
Anasema sheria za nchi zinazungumzia mtu mwanaume na mwanamke, na wanaozaliwa na jinsi tata hakuna sheria inayoelekeza waachwe wakue ili waamue jinsia.
“Hii imeondoa haki ya msingi kama kupata pasipoti, cheti cha kuzaliwa na vilevile hata usaili kuhusu kazi. Tunahitaji mabadiliko katika hili, lazima tuwe na tatizo ndipo tutengeneze miongozo.”
Dk Wangwe anasema jinsi tata ni pale unaposhindwa kutambua huyu ni wa kike au wa kiume, mpaka uende kiundani kuchunguza vinasaba ujue kiungo gani kimezidi, kama ni X anakuwa wa kike na ikizidi Y unajua huyu ameelekea wa kiume.
Wakili wa kujitegemea kutoka Human Voice of Humanity, Peter Majanjala anaishauri Serikali kuona haja ya kuonana na makundi ya wenye jinsi tata ambao wana maombi mengi kisheria, kuangalia namna wanavyoweza kupata haki hasa kubadilisha vyeti vya kuzaliwa na pasi za kusafiria.
“Pia wao wenyewe wana haki ya kupata taarifa kutoka katika taasisi za kiserikali kuwaelewesha haki zao kisheria na kukabiliana na matatizo yatokanayo na unyanyapaa,” anasema Wakili Majanjala.