Rais wa Burkina Faso, Kapteni Ibrahim Traoré, amepongeza mafanikio liliyopata jeshi hivi karibuni ya kukomboa maeneo kadhaa na kusisitiza kwamba, nchi hiyo sasa imekuwa kigezo na mfano kwa mataifa ya bara la Afrika.

Akihutubia taifa wakati wa maadhimisho ya miaka 65 ya uhuru wa Burkina Faso, Kapteni Traoré ameashiria mafanikio ya operesheni za kijeshi zilizotekelezwa hivi karibuni na kueleza: “maeneo kadhaa yamekombolewa katika muda wa mwezi mmoja … Upinzani wote wa adui uliofanywa dhidi ya vikosi vyetu umesambaratishwa, na hatujapoteza maisha ya askari yeyote wakati wa mashambulizi haya, ni wale waliopata majeraha madogo tu”.

Kamanda Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Burkina Faso ameyashajiisha majeshi ya nchi hiyo kushadidisha mapigano akisema, wahalifu “wameondolewa kutoka maeneo kadhaa na wanaikimbia Burkina Faso,” akiwapa machaguo mawili ya ama: kukimbia au kufa.

Kiongozi huyo wa kijeshi wa Burkina Faso amesisitiza kwamba, harakati za kuifanya nchi iwe na mamlaka kamili ya kujitawala zinaendeshwa na Mapinduzi ya Maendeleo ya Watu (RPP) yanayoendelea nchini humo.

“Burkina Faso leo ni onyesho, mfano,” ameeleza Rais Traoré na kuongezea kwa kusema: “tunaangaliwa, watu wanatufuata, na hatuna chaguo isipokuwa kufanikiwa. Tuko kwenye njia sahihi, na tutafanikiwa.”

Aidha, amewasihi waendeshaji wa uchumi kubadilisha mbinu zao kwa kuweka kipaumbele katika ukuaji wa viwanda nchini, kwa maana ya kusindika malighafi ndani ya nchi ili kuandaa ajira na kuhakikisha Burkina Faso inajitawala kiuchumi.

Traoré amesifu pia juhudi za walimu, wafanyakazi wa afya, na sekta ya kilimo kwa mchango wao katika mapambano ya kilimo, ambayo yanalenga kufikia kwenye utoshelevu wa chakula na huduma za afya. “Mtu yeyote anayezungumzia kujitawala hawezi kuomba chakula,” ameeleza kiongozi huyo wa Burkina Faso.

Akihitimisha hotuba yake, Kapteni Ibrahim Traoré ametoa wito kwa Burkina Faso kuwa mfano wa kutia moyo kwa bara zima la Afrika, akithibitisha tena kujitolea kwake kupambana na ubeberu, na akasema: “Waafrika wanaitazama Burkina Faso, ambayo imetoa mfano, na kwa hivyo mfano huu lazima uwashajiishe watu wengine kujiunga na mapambano ya mapinduzi, ili Afrika iwe huru, iwe yenye kuheshimika, na yenye ustawi”…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *