Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesema, serikali ina wajibu wa kufanya juhudi za kuzatiti mamlaka ya kujitawala na uhuru wa Lebanon, na Muqawamwa kwa upande wake umeisaidia kutekeleza makubaliano ya kusitisha mapigano.

Sheikh Naim Qassem, ameyasema hayo alipohutubia kongamano la Faat’imiyyuun lililofanyika kwa manasaba wa kuadhmisha mazazi ya Bibi Fatimatu-Zahra SA na kubainisha kwamba, wanawake wa Muqawama wakiwa kama mabinti, wake na akina mama wametoa mchango kwa mafanikio yaliyopatikana katika Muqawama.

Katika sehemu moja ya hotuba yake, Katibu Mkuu wa Hizbullah amesema, serikali ina wajibu wa kufanya juhudi za kuzatiti mamlaka ya kujitawala na uhuru wa Lebanon; na Muqawamwa kwa upande wake umeisaidia kwa kufanya kila ulichoombwa katika kutekeleza makubaliano ya kusitisha mapigano.

Sheikh Naim Qassem amesema, katika mapambano ya Ulil-ba’si, tulifelisha malengo ya adui. Adui mzayuni alikiri kwamba hakupata mafanikio yoyote katika vita dhidi ya Lebanon.

Huku akikumbusha kuwa, kuwepo wa Muqawama kunamaanisha kwamba maisha yanaendelea, Katibu Mkuu wa Hizbullah amesema: “wanaoitumikia Israel ndani ya Lebanon wanaushajiisha utawala huu uanzishe vita dhidi ya nchi yao”.

Ameongezea kwa kusema: utawala wa kizayuni hautaingia vitani bila ya uamuzi wa Marekani.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Sheikh Naim Qassem amesisitiza kwa kusema, “Marekani inapaswa ielewe kwamba, sisi hatutaweka chini katu silaha zetu, hata kama mbingu itashuka ardhini. Sisi ni watoto wa Imam Hussein AS na kamwe hatutasalimu amri, hatutaukubali udhalilifu katu”.

Halidhalika, Katibu Mkuu wa Hizbullah ametoa indhari kwamba, kwa kuwepo Israel, Waislamu na Wakristo hawatakuwa na mahali popote ndani ya Lebanon na kama Lebanon itasalimu amri itafutika moja kwa moja…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *